Na Ashura Kazinja, Mvomero
MKUU wa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, Mohamedi Utally, amekemea tabia ya baadhi ya watumishi wilayani humo kutumia vigenge na mitandao ya kijamii kukosoana badala ya kutumia vikao.
Hayo aliyasema juzi kwenye kikao cha Baraza Madiwani , kilichokuwa kinajadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo alisema kuwa tabia hiyo haikubaliki na kuwataka kuiacha mara moja.
Alisema ni vema watumishi hao wawe na utamaduni wa kutumia vikao vya kisheria kwani ndiyo sehemu sahihi ya kukosoana na kuelekezana badala yakupigana vijembe kupitia mitandao ya kijamii.
“Tujitahidi kutumia njia ya vikao kukosoana badala ya njia ya vigenge na mitandao, faida ya kutumia vikao vyetu vya kisheria ni ili kupata ufumbuzi sahihi bila migongano,” alisema DC Utally.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Cliford Tandari, alitoa ushauri kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, kutumia fedha za maendeleo wanazopewa zitumike na sio kuziacha na kuzirudisha zilikotoka.
“Fedha zimeletwa ili zitumike, nyie mnaziacha bila kuzitumia, mnarudisha, kwa nini, hamjui ni makossa. Ni wazi ipi miradi mingi inahitaji fedha hivyo ni lazima fedha za serikali kwa kufuata utaratibu na si vinginevyo. Hizi si fedha za kula ila ni za maendeleo ya wananchi wetu” alisema Tandari.
Pamoja na hali hiyo aliipongeza halmashauri hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya na kuipelekea kufanikiwa kupata hati safi, ambapo aliitaka kuondoa dosari 27 alizozibaini CAG.