MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema ikiwa atafanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano ataunda Baraza la Mawaziri ambalo litatakiwa kufanya kazi zaidi yake.
Pia ametangaza kumpiga kitanzi Waziri wa Ujenzi atakayemteua alisema kuwa atatakiwa kwenda na kasi katika utendaji kuliko yeye.
Amesema ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanapatikana Serikali ya awamu ya tano chini yake, itakuwa na kazi ya kupeleka maendeleo kwa wananchi kwa kasi zaidi na kutoa fursa ya kuimarisha uchumi kwa kila Mtanzania.
Kauli hiyo aliitoa mkoani Katavi jana, alipohutubia katika mikutano ya kampeni za urais.
Alisema hatua ya kuanza kampeni zake katika mkoa huo inatokana na jinsi anavyoguswa na suala la miundombinu ya barabara.
Dk. Magufuli alisema kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuomba kura inatokana na msukumo wa kuumwa na maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Watanzania kwa ujumla.
“Nimeanza kampeni zangu katika Mkoa wa Katavi na ninafahamu maeneo yana matatizo ya barabara na hapa kuna hilo tatizo. Nitaanza kwa barabara ya Mpanda kwenda Tabora kwa kiwango cha lami nitakapounda Serikali mpya ya CCM.
“Pamoja na hilo ninawahakikishia ndugu zangu nitaunda Baraza la Mawaziri imara lakini nitateua waziri wa barabara ambaye atatakiwa kufanya kazi zaidi yangu. Tutaanza na ujenzi wa barabara za Katavi kuimarisha uchumi wa Taifa letu,” alisema Dk. Magufuli.
“Ninaomba niwahakikishe ikiwa Oktoba 25, mwaka huu mtanichagua mimi John Pombe Magufuli, wabunge na madiwani wa CCM na nikafanikiwa kuunda Serikali sitawaangusha wana Mpanda na Katavi kwa ujumla.
Kikubwa ninawaomba mniamini Watanzania wenzangu,” alisema.
Alisema pia anatambua kuwa ana jukumu ambalo anatakiwa kuanza nalo la kuhakikisha anaijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mpanda-Uvinza yenye urefu wa kilometa 195.
Dk. Magufuli alisema tayari upembuzi yakinifu umekamilika na itaanza kujengwa kwa hatua za awali kwa kilometa 30.
“Barabara, barabara, barabara tunaijenga na itakuwa ni historia katika Mkoa wa Katavi.. kubwa ninawaomba mniamini ndugu zangu,” alisema Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi anayemaliza muda wake.
Aliahidi kuimarisha huduma za umeme vijijini na kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga zahanati katika kila kijiji nchini.
“Serikali ya awamu ya tano chini ya CCM itakuwa na kazi ya kuhakikisha wananchi wa maeneo yote ya mijini na vijijini wanafikiwa na huduma za umeme kulingana na sera ya Taifa, ili kukidhi mahitaji ya umeme nchini, kipaumbele zaidi kitatolewa kwa watu wote.
“… pia suala la huduma za afya kwa Watanzania ni kipaumbele kikubwa sana tangu CCM ilipoanza kuongoza nchini hii na mimi nitaimarisha zaidi kwa kuhakikisha tunajenda zahanati katika kila kijiji na kuimarisha uchumi kwa watu wote,” alisema Dk. Magufuli.
Katika mikutano yake ya kampeni aliyofanya katika iliyokuwa kambi ya wakimbizi Mishano na Katumba, Dk. Magufuli aliwahakikishia usalama watanzania hao pamoja na kuimarisha suala la umeme na ujenzi wa shule za sekondari.
Mgombea urais huyo wa CCM alizindua kampeni zake Dar es Salaam juzi na jana alitua Katavi na kufanya mikutano katika vijiji vya Majalila Mpakani, Vikonge, Mishano, Katumba na Mpanda Mjini.
Akiwa njiani msafara wake ulikuwa ukisimamishwa kila wakati na kulazimika kusalimia wananchi na kuomba kura.
Pinda aibuka
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hana shaka na Magufuli kwa vile ni mwanamume wa shoka ambaye amepikwa ndani ya CCM.
“Kwetu hapa tunasema Magufuli ni mwanamume wa shoka na CCM ina utaratibu wake wa kupata viongozi, na ndugu yangu Magufuli amepita huko amepatikana kwa misingi hiyo.
Sina shaka na utendaji wake, kila Mtanzania anaujua… ndugu zangu na hapa Mishamo ndugu zetu mliokuwa wakimbizi ni Serikali ya CCM ndiyo iliyosema nanyi muwe raia baada ya kufuata taratibu zote na sasa ni wenzetu. Tunawaomba tuwe sote pamoja kwa kuhakikisha tunaichagua CCM,” alisema Pinda.