22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa aanza kivingine

LOWASANA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

WAKATI mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, akizindua kampeni zake juzi jijini Dar es Salaam kwa mkutano wa hadhara, mpinzani wake mkubwa ambaye ni mgombea wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ameanza kwa mtindo wa aina yake wa kuwafuata wananchi mitaani.

Katika hali ambayo haijazoeleka katika siasa za Tanzania, jana Lowassa alifika kwenye kituo cha daladala kilichopo eneo la Gongo la Mboto, Ilala jijini Dar es Salaam saa 1:50 asubuhi, na kusalimia wasafiri na wafanyabiashara mbalimbali wanaofanya shughuli zao eneo hilo.

Takribani dakika 21 ambazo Lowassa alizitumia kwenye eneo hilo, zilitosha kujaza mamia ya wananchi kila mmoja akitaka kumsalimia.

Lowassa anayewania nafasi hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aliwasili kituoni hapo akiwa na gari aina ya Noah yenye namba T 607 DDR.

Mara baada ya gari hilo kusimama kituoni hapo na Lowassa kushuka, baadhi ya watu waliokuwa eneo hilo walionekana kupata mshangao kutokana na ziara hiyo ya kushtukiza, wakiwa hawaamini wanachokiona, huku wengine wakishangilia.

Muda mfupi baada ya Lowassa kufika akiwa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji, baadhi ya watu waliacha shughuli zao na kufurika kwenye eneo hilo.

Kwa madereva wa bodaboda na daladala, walisitisha shughuli zao na kusogea eneo hilo huku wakishangilia kwa kusema ‘rais… rais… Lowassa… Lowasssa’ na kupiga miluzi.

Kadiri Lowassa alivyokaa kwenye eneo hilo, watu waliendelea kufurika huku baadhi yao wakisema tangu taifa hili lipate uhuru, hawajawahi kushuhudia kiongozi mkubwa akiwatembelea kwenye maeneo yao.

“Hata waziri mwenyewe hajawahi kuja huku,” alisikika mmoja wa wananchi wa eneo hilo akisema na kuongeza: “Baba wewe ndiye unafaa, na miaka yote tulikuwa tunamhitaji mtu wa aina yako.”

Pia baadhi ya wananchi walisikika wakimweleza kwamba akifanikiwa kuwa rais, wanaitaka Katiba ya Jaji Joseph Warioba.

Katika hali ya kushangaza, mwanafunzi mmoja aliibuka na kumfuata Lowassa, huku akimwambia kuwa anacho kichinjio – kitambulisho cha kupigia kura.

 

APANDA DALADALA

Ilipotimia saa 2:11 asubuhi, Lowassa alipanda daladala yenye namba za usajili T 917 CWS inayofanya safari zake kati ya Buguruni na Nzasa na kwenda nayo hadi eneo la Pugu Shule ambako alifika saa 2:24 asubuhi.

Wakati anapanda ndani ya daladala hiyo, wananchi walijazana eneo hilo walizidi kupatwa na mshangao, wengine wakisema hawaamini wanachokishuhudia.

Kitendo hicho kilisababisha baadhi wa wananchi kuvamia daladala hiyo na kupanda, huku wengine wakipitia madirishani kutokana na msongamano wa kugombania ulivyokuwa mlangoni.

Wananchi hao walijaa kwenye daladala hiyo hadi wengine wakaning’inia mlangoni na kisha kuanza safari yake kuelekea Pugu.

Kitendo cha daladala hiyo kuondoka eneo hilo, vijana waendesha bodaboda walianza kuifuata kwa nyuma na  wengine wakitangulia mbele yake.

Baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye kituo hicho, nao waliifuata daladala hiyo wakikimbia hadi Pugu, takribani umbali wa mita 400.

Akiwa ndani ya daladala hiyo, Lowassa aliyekuwa ameketi kiti kimoja na mwanafunzi, alitoa Sh 2,000 kwa ajili ya nauli yake na abiria waliokuwa karibu naye.

Baada ya kufika katika eneo hilo la Pugu Shule, Lowassa alishuka na kupanda kwenye gari lake ambapo msafara uliendelea hadi Mbagala Rangi Tatu.

 

DEREVA WA DALADALA ANENA

Akizungumza na MTANZANIA, dereva wa daladala hiyo, Steven Zunga, alisema amefurahi sana kwa kitendo cha mgombea huyo wa Ukawa kupanda gari lake.

“Furaha niliyonayo siwezi kuelezea, nimefurahi sana… sijui kama leo nitalala, sikutegemea kama siku moja ningemwendesha Edward Ngoyai Lowassa. Imeingia katika historia yangu na nitaiandika kwenye kumbukumbu zangu,” alisema dereva huyo.

 

AWASILI MBAGALA RANGI TATU

Lowassa ambaye pia aliongozana na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gudluck Ole Medeye na Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Rajab Katimba, aliwasili katika eneo la Mbagala Rangi tatu saa 4:06 asubuhi.

Kabla ya kuwasili Lowassa, eneo hilo lilijaa umati wa watu kutokana na madereva wa bodaboda ambao walikuwa wakiwasiliana na wenzao kwamba waziri mkuu huyo wa zamani atafika katika eneo hilo.

Baadhi ya wananchi walimwomba Lowassa ashuke kwenye gari angalau aseme neno moja tu waridhike na baada ya kelele hizo kuzidi, alishuka na kuwapungia mkono.

Kitendo hicho kiliwafanya wazidi kulipuka wakisema wanataka kusikia chochote kutoka kwake.

 

JUMA DUNI ALIPUKA

Kutokana na ombi hilo la wananchi hao, saa 4:12 asubuhi Duni alishuka ndani ya gari na kupewa kipaza sauti na kuwaambia wananchi hao kuwa wamepita kuwasalimia na kuwapa pole malofa na wapumbavu wenzao.

“Sisi tumepita kuwasalimia ninyi malofa na wapumbavu wenzetu, leo tumeamua tuamke asubuhi na mapema kuja kuwasalimia. Tusije tukaambiwa tumeitisha mkutano ambao hauna ruhusa.

“Tumepita kuwasalimia ninyi wanyonge wenzetu mnaoitwa kila aina ya majina, mara vibaka na wahuni. Sasa sijui masikini anayetafuta riziki kuitwa majina hayo, lakini tunaomba mtuache leo tutakutana Jumamosi pale viwanja vya Jangwani,” alisema Duni huku alishangiliwa na umati huo wa watu.

Pamoja na hilo, pia aliwaambia kwa muda huo wakutane Dar Live kwani Lowassa angeendelea kuwatembelea wafanyabiashara na kero wanazozipata abiria katika vituo vya daladala.

Kitendo hicho kilisababisha wananchi hao kukimbilia msafara huo huku wengine wakiacha shughuli zao, lakini ilishindikana Lowassa kusimama katika eneo hilo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa mazingira hayakuruhusu.

 

MSEMAJI WA LOWASSA ANENA

Msemaji wa Lowassa, Abubakari Liongo, alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza kuhusu kero ambazo wanazipata wafanyabiashara, abiria pamoja na foleni katika Jiji la Dar es Salaam.

“Lengo la ziara hii ni kuangalia uhalisia wa tatizo la usafiri Dar es Salaam, wafanyakazi wanaamka asubuhi wanachelewa kufika kazini, wanafunzi nao vivyo hivyo, ndiyo maana ametoka Gongo la Mboto hadi Mbagala kujionea hali ilivyo, lakini pia ametumia fursa hii kuzungumza na wananchi na wafanyabishara ndogondogo ili awasikilize shida zao,” alisema Liongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles