29 C
Dar es Salaam
Wednesday, September 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wafanyakazi, machinga waikana CCM

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano (COTWU T), kimesema hakijaridhishwa na mchakato wa kuwapata wabunge wa viti maalum kupitia kundi la wafanyakazi kwa kuwa mchakato huo ulikuwa wa kificho hivyo hakitambui uteuzi huo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa COTWU (T), Mathias Mjema alisema wao kama wanachama wameshangazwa na uteuzi wa wabunge  Angellah Kairuki (DSM) na Hawa Chakoma (Pwani) kwa kuwa hakukuwa na ushirikishwaji katika uteuzi huo.

Alisema wao ni wanachama halali wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),  lakini wanashangaa katika mchakato huo hawakupewa taarifa wala mwenendo wa kuwapata wawakilishi hao.

“Sisi kama wanachama wa TUCTA tunashangaa mchakato huu ulifanyika lini   na wapi ulipofanyika,” alisema  Mjema.

Alisema kitendo hicho kimeleta malalamiko kwa wanachama wa COTWU (T) kwa kuwa wengi walitaka kujaza fomu za kugombea lakini walikosa haki hiyo.

Mjema alisema    Agosti 21 mwaka huu, kamati ndogo ya COTWU (T)ilijadili suala hilo lakini baada ya kuwasiliana na ngazi za juu iliambiwa tayari mchakato huo umefanyika na wagombea wamepatikana.

Alisema kuna utaratibu ambao umekuwa ukitumika miaka yote ya kuwapata wagombea lakini safari hii imekuwa kinyume.

Imekuwapo kawaida ya kuwapata wawakilishi hao kwa kuwakutanisha wagombea kutoka mikoa 25 halafu baadaye wanachujwa na kupatikana wawili, alisema.

“Vigezo vilivyotumika bado vinatupa maswali mengi…tunashangaa lakini katika mchakato wa kuwapata wabunge wawakilishi wa Bunge la Katiba tulishirikishwa na mchakato ulienda vema bila manung’uniko,”alisema Mjema.

Naye Katibu wa Elimu, Ushirikishwaji na Utangazaji wa COTWU (T), Juliana Mpanduji alisema alipokea malalamiko ya wanachama kuhusu mchakato huo na kuyafanyia kazi katika ngazi zote.

Alisema aliamua kulifuatilia jambo hilo kwa undani kwa kuwa wengi walitaka kuchukua fomu lakini hawakupata majibu ya kueleweka kutoka TUCTA ambao  waliwajibu mchakato tayari umepita.

“TUCTA Taifa walituambia mchakato umepita na wagombea walichukua fomu kwa Makatibu wa CCM Mikoa na kinyang’anyiro hicho alishinda Angellah (DSM) na  Hawa  (Pwani) jambo ambalo sisi limetuachia maswali mengi,”alisema.

Wakati huohuo, makundi ya wafanyabiashara ndogondogo (machinga) na waendesha bodaboda, yameibuka na kuwakana waliojitambulisha kuwa wawakilishi wao.

Yakizungumza kwa nyakati tofauti    Dar es Salaaam jana, makundi hayo yalisema waliotoa salamu katika ufunguzi wa kampeni za CCM katika viwanja vya Jangwani juzi si wawakilishi wao na walichozungumza  ni mawazo yao binafsi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa muda wa madereva wa bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam,Said Kagomba alisema  taarifa iliyotolewa na mtu aliyejitambulisha ni kiongozi wao ni batili na kamwe hawamuungi mkono.

Alisema wao kama chama cha waendesha pikipiki hawafungamani na chama chochote cha siasa.

“Sisi kama madereva wa bodaboda hatuna chama cha siasa isipokuwa wanachama wetu wana itikadi zao, ” alisema Kagomba.

“Bodaboda tuna matatizo mengi  kama kukatazwa kuingia mjini,kukamatwa ovyo bila kufuata sheria na kupigwa faini kuanzia Sh 30,000 hadi Sh 400,000 bila risiti ya malipo na ukikosa fedha hiyo unapelekwa mahakama ya jiji na kupelekwa jela hivyo tuna vitu vingi vya kutafakari na si siasa,”alisema Kagomba.

Katibu wa  Chama cha Waendesha Pikipiki Ilala(CHAWAPILA),Michael Roswe,  alisema wanamtaka mtu huyo awaombe radhi jukwaani kwa kuwadhalilisha.

Naye Katibu Msaidizi wa Chama cha Chama cha Ushirika cha Waendesha Pikipiki (DABOSA), Almano Mdede alisema umefika wakati viongozi wa siasa waache  kutumia wanyonge kama ngazi ya kupatia uongozi.

Wamachinga kwa upande wao, walisema  hawamtambui mtu aliyesimama na kuwawakilisha katika kampeni hiyo.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Wafanyabiashara Ndogondogo cha Jua Kali kilichopo Machinga Complex, Dar es Salaam, Suleiman Dauda, alisema hawajawahi kuitwa na kujadiliana na mtu yeyote kuhusu kuunga mkono chama chochote cha siasa.

“Hatumjui   huyo aliyejiita kiongozi wetu kwanza tulimsikia jana katika jukwaa akijinadi kuwa anatuwakilisha, ni uzushi,” alisema Dauda.

Mfanyabiashara wa soko hilo, Nurdin Kilema, alisema mtu huyo inaonyesha ana maslahi yake binafsi kwa kuwa hawajawahi kuambiwa kuwa kuna mkutano wowote wa siasa.

Katika mlolongo huo, Chama cha Wasioona Tanzania (TLB), kimekana kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA),Amon Mpanju kwamba vyama vyote vya walemavu wanamkubali mgombea urais wa CCM, Dk. John  Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa TLB, Luis Benedicto alisema kauli aliyoitoa Mpanju katika uzinduzi wa kampeni za CCM Jangwani si msimamo wa TLB wala SHIVAWATA kwa sababu  wao hawafungamani na chama chochote cha siasa.

Alisema wao kama chama hawajawahi kufanya mazungumzo na kumwagiza na hawana uhusiano na chama chochote cha siasa.

Benedicto alisema mara nyingi wamekuwa wakimtaka kuwa makini na kauli zake hasa za kuonyesha mapenzi ya waziwazi kwa chama Fulani. Hata Bunge Maalum la Katiba alikuwa akifanya hivyo bila kujali.

“Tumesikitishwa na kauli aliyoitoa Mpanju pale Jangwani kwamba walemavu tunaunga mkono CCM… si kweli, mimi ni mjumbe wa bodi ya SHIVAWATA na mwenyekiti wa TLB ambako ndipo anatokea Mpanju lakini hata siku moja hatujawahi kukaa sehemu yoyote na kumwagiza azungumze.

“Hivyo kauli aliyoitoa katika jukwaa la siasa ni msimamo wake na hisia zake mwenyewe na si walemavu wote,”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles