27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE WAITARA ATOA SABABU TATU KUHAMA CHADEMA

KARIBU KWETU: Aliyekuwa Mbunge wa Ukonga Mwita Waitara (CHADEMA) akifurahia jambo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, baada ya kuhamia chama hicho jana. PICHA SILVAN KIWALE

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM              |           


MBUNGE wa Jimbo la Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), ametangaza kujiuzulu uanachama wa chama hicho na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM),  huku akitaja sababu tatu zilizomsukuma kuchukua uamuzi huo.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni ugomvi  baina yake na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, baada ya kuonyesha nia ya kutaka kugombea nafasi hiyo lakini pia kile alichodai kuwapo kwa matumizi mabaya ya fedha za ruzuku ndani ya chama hicho.

Sababu nyingine ni kikwazo cha kushirikiana na viongozi wa Serikali katika kutekeleza shughuli za maendeleo.

Waitara ambaye alitangaza uamuzi huo jana katika ofisi ndogo ya CCM Lumumba, akiwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, kujizulu kwake huko kwa kushtukiza kumekuja katikati ya ziara aliyokuwa akiifanya wiki hii katika jimbo alilokuwa akiliongoza.

Anakuwa mbunge wa nne kuhama chama tangu  kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na wa pili wa Chadema baada ya Desemba 14, Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel kutangaza kuachana na chama hicho kabla ya kurejea tena katika nafasi hiyo, lakini safari hii akiiwakilisha CCM.

Wabunge wengine waliohama ndani ya vyama vyao ni aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu na aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni kupitia CUF, Maulid Mtulia, ambaye sasa ni Mbunge wa jimbo hilo hilo akiiwakilisha CCM.

Tofauti na wabunge wengine waliohama isipokuwa Nyalandu, ambao walieleza sababu ya kuchukua uamuzi huo kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli, Waitara yeye ameelekeza lawama zake nyingi kwa uongozi wa Chadema.

Akifafanua sababu hizo, alisema mfumo wa uongozi wa Mbowe unawafunga wanachama kuhoji masuala ya msingi ambayo yakifanyiwa kazi yanaweza kuboresha taasisi hiyo.

“Ukiwa kwenye chama huruhusiwi kuhoji chochote na hili ni jambo kubwa sana popote, ugomvi wangu mkubwa na Mbowe sasa hivi ni kwa sababu kuna uchaguzi wa ndani ya chama.

“Tukiwa kwenye vikao vya chama nilisema huyu mtu ameongoza chama miaka ishirini sawa na  umri wa mtu mzima na chama kinaitwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, lakini kwa hili demokrasia siioni,” alisema Waitara ambaye alikuwa mbunge wa saba kati ya wabunge kumi waliopata kura nyingi zaidi ya 90,000 katika uchaguzi wa 2015.

Alisema mwenendo wake wa kuhoji mambo ndani ya Chadema ulimfanya  Mbowe aahidi kumshughulikia ndipo alipoamua kutafuta mahali ambako atafanya siasa akiwa salama.

Alisema mbali na hilo, Chadema pia kimekuwa na matumizi mabaya ya fedha za ruzuku ambazo ni Sh milioni 236 kwa mwezi.

“Chama kinaingiza Sh milioni 236 kila mwezi lakini hakina ofisi ya makao makuu, kanda, mkoa, hakuna ofisi za jimbo wala watumishi,” alisema Waitara.

Alisema kutokana na hali hiyo ufanyaji wa kazi za chama umekuwa mgumu kwani wanalazimika kuwalipa watu kwa ajili hiyo.

Mbunge huyo aliyejiunga na CCM mwaka 1998 kabla ya kurejea jana,  alisema wakati anawaza kuhama alilazimika kutafuta chama ambacho kipo juu zaidi  kisiasa  na kuamua  kujiunga na CCM.

Waitara ambaye alijiunga na Chadema mwaka 2008 akitokea CCM  baada ya kuvuliwa cheo akiwa Tanga na kutakiwa kurudi Makao Makuu ambako alikataa kuwa msadizi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho, Emmanuel Nchimbi, akidai kuwa hawezi kufanya kazi ya kumkorogea chai, alidai kuwa sasa amekuwa na mawazo tofauti.

“Inawezekana watu wa Ukonga watashtuka sana lakini nina nia njema kabisa na Polepole hajawahi kunipa hata shilingi mia, lakini nimefanya uamuzi huu baada ya kuona nafanya kazi ambazo  mbele naona kuna giza.”

Waitara pia alisema akiwa mbunge kuna vitu vya kimaendeleo ambavyo alikuwa anashindwa kuvitekeleza kwa sababu ya kukosa ushirikiano na viongozi wa Serikali, hali ambayo ilikuwa inasababishwa na  viongozi wa Chadema.

“Wananchi wanahitaji maendeleo, maji, barabara, vituo vya afya ambavyo vyote vinahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa Serikali.

“Nilikuwa napata changamoto ya namna ambavyo  nafanya kazi na Serikali nikiwa Chadema, mfano jimbo langu linahitaji maji ikitokea nikaamua kuomba appointment (miadi) na Waziri wa Maji, chama kinanihoji mbona upo karibu na waziri sasa mimi maji nitayatoa wapi kama sijaonana na waziri,” alihoji Waitara.

Alisema hata wakati wa upitishaji wa bajeti  ya mwaka wa fedha 2018/19 pia aliulizwa kwanini hana kesi kwakuwa walio na kesi katika chama hicho ndiyo wanaoonekana majasiri.

“Mimi situkani, wao wanatukana halafu ukitukana ukikamatwa ukafunguliwa kesi unasema Magufuli anakuonea, hata mimi ningekuwa Rais ningewashughulikia kwa sababu sheria zipo, hazitaki mtu atukane mfano uje unipige ngumi nikikukamata useme CCM wanakuonea kweli?” alihoji Waitara.

Alisema Chadema kwa sasa imekuwa kampuni badala ya kuwa taasisi na ili kuendana na hali hiyo wanalazimika kuishi kwa maigizo.

Awali akimkaribisha Polepole alisema  wao kama CCM wanamwamini katika kusimamia ukweli na kwamba, katika kipindi hiki watashirikiana naye katika kampeni zinazoendelea.

Zaidi alisema CCM inamwandalia mapokezi na utambulisho rasmi katika eneo analoishi.

 MBOWE AJIBU

Tuhuma alizozitoa Waitara zimemwibua Mbowe ambaye kupitia mitandao ya kijamii, aliandika kuwa; ujenzi wa demokrasia ni safari ndefu yenye milima, mabonde, miiba, mawe na kila aina ya majaribu yenye vikwazo.

“Waasisi wa chama walifananisha na safari ya treni kutoka Dar kwenda Kigoma. Kwamba kuna watakaoshuka njiani kwa sababu mbalimbali, (halali na batili) hali kadhalika wengine wengi watapanda vituo mbalimbali kuungana na safari.

“Hampaswi kushangaa baadhi yetu kuishia njiani. Nina hakika na imani kuwa hatakuwa wa mwisho kutoka,” lilisomeka andiko la Mbowe.

Hakuishia hapo, aliendelea kuandika kuwa wapo maelfu ambao wanapanda treni yao kila siku hivyo si kila atokaye ni hasara kwa chama chao na kusisitiza kuwa kutoka kwingine kwaweza kuwa baraka.

“Wajibu huu wataka moyo Mkuu!! Shime wenye nia ya kufika Kigoma kwa umoja wetu tusonge mbele tukijiamini sana!,” aliandika Mbowe.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe, alishangazwa  na uamuzi wa mbunge huyo ambapo kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika ujumbe uliosomeka.

“Mbunge mwenzio yupo hospitali mwaka sasa kwa majeraha ya risasi kufuatia jaribio la kumuua, kiongozi wa chama chako karibu wote ngazi za Taifa wana kesi inayohatarisha kuwaweka jela. Watu wanauawa na kupotea kila siku, halafu unajiunga na hao wanaosababisha hayo, kweli Mwita,” aliandika Zitto.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Waitara kafanya maamuzi kwa mjibu wa katiba kama katishiwa na kiongozi wake mbowe anayo haki ya to mitigate usalama wake ,kwenye risk and disaster tunaamini kila taarifa usiipuuze hivo maamuzi yake WAITARA yaheshimiwe,aidha zitto unajuwa yaliyokukuta hadi kukihama CHADEMA, kipi leo unachooshangaa by NTOWE

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles