Na MWANDISHI WETU-MIRERANI
JESHI la Polisi Mkoa wa Manyara, limewatia mbaroni watu watatu wakazi wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kwa tuhuma za kukutwa na kilo 7.53 za madini ya Tanzanite waliyokuwa wameyaficha chini ya unga uliokuwa kwenye ndoo.
Akizungumzia na waandishi wa habari jana kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni wakati wa upekuzi uliokuwa ukifanywa na maofisa madini, usalama wa taifa na polisi katika lango la kuingilia ndani ya ukuta unaozungumka migodi ya Tanzania.
Chaula alisema wakati wa upekuzi watu hao watatu walibainika kuficha madini hayo kwenye ndoo iliyokuwa na unga.
Alisema mwanamke aliyekamatwa akiwa na ndoo hiyo mkononi anajishughulisha na kazi ya kuchekecha mchanga na udalali wa madini.
“Madini waliyaficha kwenye ndoo iliyokuwa imewekwa unga wa mahindi,” alisema Chaula
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Judith Paulo, Midumbi Ojijo na Joshua Aguta.
Alipoulizwa kuhusu thamani ya madini hayo alisema bado haijajulikana na watuhumiwa wanashikiliwa na polisi katika kituo cha Mirerani kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Augustino Senga jana alilithibitisha MTANZANIA kukamatwa kwa wahumiwa hao na kwamba bado wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi.