|Suzan Uhinga, Tanga
Chama cha Wananchi (CUF), jijini Tanga kimewavua uanachama madiwani watatu wakiwamo wawili wa Viti Maalumu na mmoja wa Kata ya Mwanzange.
Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Daudi Mayeji, ametangaza hatua hiyo jana jioni baada ya kupokea baurua kutoka kwa uongozi wa chama hicho.
“Nimepokea barua kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Magdalena Sakaya iikeleza kuwafuta uanachama kwa madiwani wawili wa Viti Maalumu, Halima Juma na Fatuma Hamza na Diwani wa Kata ya Mwanzange, Rashid Jumbe,” amesema Mayeji.
Amezitaja sababu tatu zilizoainishwa katika barua hiyo kukivuruga chama, kukataa wito wa kamati ya maadili ya chama hicho na kukaidi kufika katika kikao cha Baraza la Uongozi Taifa la chama hicho.
Akizungumza baada ya uamuzi huo kutangazwa, Jumbe ambaye pia wa Mwenyekiti wa CUF wilaya, amesema hatambui waliomfuta uanachama kwa sababu si viongozi wala wanachama wa chama hicho.
Wakati huo huo, madiwani hao wa Viti Maalumu nao waliungana na Jumbe wakidai hawatambui uamuzi huo kwa sababu hawamtambui Sakaya wala Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba kwa sababu alishafukuzwa uanachama.
“Walioandika barua za kutufukuza sisi hatuwatambui, kiongozi tunayemtambua ni Katibu Mkuu wetu Maalim Seif Sharrif Hamad hao wengine hatuwajui,” wamesema.