Na JANETH MUSHI – ARUSHA
MRADI wa kubaini kwa haraka vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) kwa wagonjwa wapya, umezinduliwa katika nchi za Jumuiya ya Mashariki (EAC).
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi, Kaimu Mkurugenzi wa Kuratibu Tafiti za Afya kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Paulo Kazyoba, alisema mradi huo wa miaka mitatu, unalenga kuboresha mfumo wa afya wa jinsi ya kugundua vimelea vya ugonjwa huo kwa nchi za Afrika Mashariki.
Alisema NIMR inashirikiana na mtandao wa kujengea uwezo tafiti za afya Afrika Mashariki katika kufanikisha mradi huo na kwamba wao watasaidia kufanya tafiti zitakazochangia kuboresha sera na utendaji kazi katika sekta ya afya.
“Mradi huu wa miaka mitatu utasaidia kwa kiwango kikubwa kutupa majibu ya namna ya kubaini vimelea vya kifua kikuu na ni muhimu kwa nchi yetu na nchi nyingine za Afrika Mashariki katika kuutokomeza ugonjwa huo,” alisema Dk. Kazyoba.
Awali, Profesa Sayoki Mfinanga kutoka NIMR – Muhimbili, alisema pamoja na taratibu nzuri za kutoa tiba ya wagonjwa wa TB, bado kunahitajika mkakati wa kuibua wagonjwa wa maradhi hayo walioko kwenye jamii na kuhakikisha wanapatiwa matibabu hospitalini.
“Tatizo la TB bado ni kubwa katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na ugonjwa huu upo wa mapafu na wa viungo. Hivyo basi ni lazima tuhakikishe tunatafuta jitihada zaidi za kufanya tafiti za matibabu ili ikiwezekana yawe chini ya miezi sita,” alisema.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Timoth Wonanji, alisema takwimu zinaonyesha katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu, wamefanikiwa kuibua wagonjwa wapya 3,180 waliopimwa na kugundulika kuwa wana maambukizi ya TB.