Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MBUNGE wa Ludewa anayemaliza muda wake, Deo Filikunjombe (CCM), amesema hatua ya kuchaguliwa na wana Ludewa na kisha kuteuliwa na chama chake kwa mara ya pili ni kitendo cha heshima kwake na wapiga kura wake.
Hayo ameyasema jana alipokuwa akizungumza na MTANZANIA, ambapo alisema pamoja na kupata changamoto wakati wa kura za maoni lakini bado atazifanyia kazi hoja za waliokuwa washindani wake ili kuweza kumaliza kero za wana Ludewa.
“Ninawashukuru sana wananchi wa Ludewa kwa kunichagua kwa mara nyingine tena ili nikawe mwakilishi, mtumishi na mtetezi wao kwenye Bunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Tulikuwa wagombea watatu mimi nilipata kura nyingi zaidi, ambapo mgombea mwenzangu Kapteni Jacob Mpangala, alipata kura 156 sawa na asilimia 0.8, Mhandisi Zephania Chaula alipata kura 733 sawa na asilimia 3 na mimi Deo Filikunjombe nilipata kura 19,364 sawa na asilimia 96 ya kura zote.
“Lakini pia, ninaomba nitumie fursa hii kuwashukuru washindani wangu Mhandisi Chaula na Kapteni Mpangala, kwa hakika walinipa changamoto nyingi. Na mawazo yao yale mazuri nitayafanyia kazi,” alisema Filikunjombe.
Mbunge huyo alisema pia anawashukuru wananchi wa Ludewa kwa imani yao kubwa kwake ambapo aliahidi kutowaangusha.
“Sitawaangusha… ninawashukuru pia Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kutokata jina langu,” alisema.