27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DAWA KUONGEZA NGUVU ZA KIUME HUATHIRI KISAIKOLOJIA

KWA tafsiri ya kawaida, nguvu za kiume ni ule uwezo wa mwanamume kuweza kushiriki tendo la ndoa.

Licha ya kwamba tendo la ndoa ni shirikishi kwa kuhitaji utayari kwa watu wa jinsia zote mbili, lakini kumekuwa kukitokea mazingira ambayo yanamfanya mwanamume au mwanamke kushindwa kushiriki tendo hili kwa namna ambayo pengine mtu binafsi mwenyewe angependa iwe na kumfanya afurahie tendo.

Leo tutazungumzia baadhi ya mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yamekuwa yakichangia kumfanya mwanamume ashindwe kushiriki tendo la ndoa na hivyo kulazimika kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume bila ya kufahamu usalama na matumizi sahihi ya dawa husika.

Sehemu kubwa ya mtu kuweza kushiriki tendo la ndoa inatokana na utayari wake binafsi kiakili au kisaikolojia. Mtu anapokuwa kajiandaa kiakili kushiriki tendo la ndoa, mwili wake huzalisha vitu mbalimbali au homoni ambazo zitasaidia kuufanya mwili uwe tayari kufanya tendo husika ikiwa ni pamoja na kuongeza mzunguko wa damu mwilini.

Kwa wanaume mzunguko wa damu huongezeka na kuwezesha uume kusimama na kumudu kushiriki tendo. Aidha, pamoja na utayari wa kisaikolojia, kuna baadhi ya mambo yanayoweza kumfanya mwanamume ashindwe kushiriki tendo la ndoa.

Mambo hayo ni pamoja na msongo wa mawazo (upo na mwenzako lakini mawazo yapo katika kufikiria wapi utapata fedha ya kulipa madeni, unawazia mtihani wa mwisho kesho, unawaza kufukuzwa kazini, hofu ya magonjwa na kadharika. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kumfanya mwanamume ashindwe kushiriki tendo la ndoa hata kama atakuwa kaandaliwa na mwenza wake.

Pamoja na sababu hizo tajwa, kuna baadhi ya magonjwa ambayo huathiri mishipa ya damu na hatimaye kupunguza uwezo wa damu kuzunguka kwa urahisi katika maumbile ya uzazi kwa mwanamume. Moja ya magonjwa hayo ni kisukari.

Kutegemeana na chanzo cha tatizo la mwanamume, kushindwa kushiriki tendo la ndoa, ufumbuzi wa tatizo au tiba inaweza kutofautiana.

Watu wengi wamekuwa wakiangukia katika kutafuta dawa za kuongeza nguvu za kiume pasipo kuelewa kuwa chanzo cha wao kushindwa kushiriki tendo hilo ni nini. Ni kweli kwamba zipo dawa ambazo hutumika ili kumsaidia mwanamume mwenye matatizo hayo, lakini dawa hizi hutolewa chini ya ushauri wa wataalamu.

Kwa mwanamume ambaye analo tatizo la kisukari, pamoja na magonjwa mengine ambayo huathiri nguvu za kiume, dawa za kitaalamu zimekuwa zikitolewa ili kumsaidia mhusika.

Dawa hizo hutumika kwa kuzingatia hali ya kiafya ya mtumiaji mfano, angalizo kwa watu wenye magonjwa ya moyo.

Kwa kuwa dawa hizi huongeza mzunguko wa damu mwilini, matumizi yake kwa watu wenye presha au shinikizo la damu ni muhimu kupata ushauri fasaha kabla ya kuamua kufanya matumizi ya dawa hizo.

Pia ufanyaji kazi wa dawa hizi za kuongeza nguvu za kiume, huenda sambamba na maandalizi ya kisaikolojia ya mtumiaji. Dawa hazitakuwa na msaada endapo mawazo ya mtumiaji yapo katika kuwaza kodi ya nyumba wakati mwenza yupo jirani, pia kwa usalama wa mtumiaji haishauriwi matumizi ya dawa yafanyike wakati haupo uhakika wa kukutana na mwenza.

Matumizi holela ya dawa hizi yamekuwa yakihusisha dawa za hospitali na mitishamba.

Miongoni mwa athari za matumizi holela ya dawa hizi ni pamoja na matatizo katika moyo na mzunguko wa damu, pia matumizi ya dawa hizi kiholela huathiri kisaikolojia na hatimaye kumfanya mtu hata kama anazo nguvu za kutosha, apoteze kujiamini na hatimaye kushindwa kushiriki tendo.

Dawa za kuongeza nguvu za kiume hazipaswi kutumika bila ya ushauri wa kitaalamu, jali afya yako kwa kuzingatia utulivu wa akili, lishe bora na ushauri wa wataalamu wa afya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles