25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

LUPUS: UGONJWA USIO NA TIBA UNAOWATESA WANAWAKE

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


KWA kawaida kinga za mwili humlinda mtu husika dhidi ya magonjwa hata hivyo, wapo baadhi ambao kinga zao hushambulia mwili badala ya kuulinda.

Huo ni ugonjwa ambao kitaalamu huitwa ‘System Lupus Erythematosus (SLE). Hadi sasa bado wataalamu wa afya hawajabaini nini hasa husababisha kutokea kwake.

Mei 3, 2018, Onesmo Mhehwa aliyekuwa Daktari Bingwa wa Usingizi kwa Watoto na Wagonjwa mahututi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

 

Simulizi ya mgonjwa

Meneja Utawala, Huduma za Hospitali (HR) katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Costansia Lima anasema mwaka 2015 alianza kujihisi vibaya hasa kichwani.

“Nilianza kuhisi pia sehemu ya tumbo (eneo la chini) likiuma, nikaenda kuonana na Medical Director wa Muhimbili nikamweleza, akanipatia daktari bingwa wa mfumo wa fahamu, akanichunguza kwa vipimo mbalimbali ikiwamo MRI lakini hakuona tatizo.

“Siku zilivyoenda hali yangu ilizidi kubadilika, nikaanza kupata shida kwenye ngozi, nikawa napata mabaka meusi, nywele zikaanza kunyofoka nikichana, nikabadilika sura, nilikuwa na hali mbaya.

“Mkurugenzi wa Muhimbili akasema kama imeshindikana kugundulika wanipe rufaa, nikapelekwa India, kule nilipata Nimonia kali, lakini Mungu alinisaidia nikapata matibabu  baadae nikapata nafuu, nikarejea nyumbani nikiwa na dawa za kunisaidia.

“Sikuweza kuzungumza na wale madaktari nilikuwa na hali mbaya, nipo nchini naendelea na matibabu hapa nyumbani. Ni wakati sasa jamii ielezwe kwa kina kuhusu ugonjwa huu, inawezekana wanaumwa lakini hawajui kama ni ugonjwa, mimi ilinichukua muda mrefu kugundulika,” anasimulia Lima.

 

Mgonjwa mwingine

Tangu mwaka 2007 hadi sasa, Irene Kilumanga ambaye ni mke wa Balozi Chabaka Kilumanga, anasumbuliwa na ugonjwa huo na kwamba dalili zake zinafanana na za malaria.

Mumewe, Balozi Kilumanga anasema watu wanaougua ugonjwa huo unaweza kuona wanafanya makusudi kutokana na kuugua kwa muda fulani na muda mwingine kuoneka akiwa mzima.

“Kwa mtu ambaye hana imani anaweza kudhani amerogwa kwa sababu anaweza kuwa mzima na ghafla akajikuta ameanguka, mwili unaanza kuishiwa nguvu na kupata maumivu,” anasema.

Anaongeza: “Sisi tulimpeleka hospitalini akawa akitibiwa baada ya muda anaumwa tena, tukimrudisha hospitali tatizo halionekani.

 

Daktari

Kifo cha Dk. Mhehwa kimeipa pigo JKCI kwa kuwa ndiye alikuwa daktari pekee kwa upande wa matibabu ya watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi, anasema chanzo cha ugonjwa huo hakijulikani na hauna tiba.

Anasema dalili zake hufanana kwa ukaribu na za malaria.

“Wataalamu bado hawajabaini sababu, kinga za mwili sasa zinaugeuka mwili wenyewe, ghafla zinaanza kuushambulia kila mahali, kwenye figo, moyo, tumbo chochote wenyewe unadhani ni adui.

“Hauna tiba, mgonjwa akija hospitalini kama anasumbuliwa na bakteria tunampa antibiotics, ikiwa ni virusi nitakupa dawa ya virusi, lakini kwa kawaida mtu anapolalamika kuumwa moja kwa moja tunaangalia labda amepata malaria.

“Lakini akipimwa malaria haionekani, typhoid (homa ya matumbo) hana, hapo inabidi achunguzwe zaidi ndipo tunapogundua nini kinamsumbua. Tafiti zinaonesha wanawake ndiyo huathiriwa zaidi kuliko wanaume,” anasema.

 

Utafiti

Kulingana na mtandao wa Medical News Today, umeeleza kuwa Lupus ni miongoni mwa magonjwa sugu, ambapo kinga za mwili wa binadamu badala ya kumlinda hugeuka na kuanza kumshambulia.

Hali hiyo inapotokea mhusika huhisi maumivu makali, huvimba mwili, homa za mara kwa mara na baadae viungo vyake vya ndani ikiwamo moyo, figo na mapafu navyo huathiriwa.

 

Mtandao huo unaeleza, kwa kawaida mfumo wa kinga hutengeneza protini iitwayo ‘antibodies’ ambayo hulinda na kupigana dhidi ya ‘antigens’ kama vile virusi na bakteria.

 

Lakini, kwa mtu mwenye Lupus mambo huwa kinyume, yaani ule mfumo wake wa kinga wa mwili hushindwa kutofautisha kati ya ‘antigens’ na tishu zilizo bora.

 

Hali hiyo husababisha mfumo wa kinga kuziamuru ‘antibodies’ kuzishambulia tishu zilizo bora badala ya ‘antigens’ kama inavyopaswa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, kitendo hicho ndicho ambacho husababisha mhusika kupata maumivu makali, uvimbe na kuathirika kwa viungo vyake.

Inaelezwa ugonjwa huo si wa kuambukiza na kwamba umegawanyika katika makundi mawili; Lupus Erythematosus (SLE) na Lipus Discoid (Cutaneous).

Mtandao huo unaeleza, Kulingana na Shirika la Lupus la nchini Amerika, watu wapatao milioni 1.5 hadi mbili nchini humo wanakabiliwa na aina mojawapo ya Lupus.

Kwamba silimia 72 ya Wamarekani wenye umri wa miaka kati ya 18 hadi 34 hawaufahamu kwa kina ugonjwa huo.

Mtandao huo unabainisha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wa Lupus ni wanawake, ambapo wengi wao ni wale wenye umri kati ya miaka 15 hadi 45.

 

Dalili zingine

Kulingana na mtandao wa Heath line, watu wenye Lupus figo zao huvimba hali iitwayo kitaalamu ‘nephritis’ huzifanya zishindwe kuchuja taka mwili na kujikuta wakipoteza damu.

Mtandao huo unaeleza, kwa mujibu wa Shirika la Lupus la Amerika, nephritis huanza kujitokeza ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu mtu apate ugonjwa huo.

Unaeeleza mtu mwenye Lupus ambaye figo zake zimeanza kushindwa kufanya kazi huvimba miguu, hupata shinikizo la damu, huona chembe chembe za damu kwenye mkojo wake.

Unaeleza wakati mwingine mkojo huonekana kuwa wa rangi nyeusi, huenda haja ndogo mara kwa mara hasa nyakati za usiku na hupata maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.

Wakati mwingine, mtu mwenye Lupus huugua homa ya matumbo ingawa si wote na wapo ambao hupata ukavu wa midomo au macho na kunyonyoka nywele.

Kwa mujibu wa mtandao huo, wagonjwa wengi wa Lupus hupata vipele usoni unaozunguka (butterfly rash).

 

Kwanini wanawake?

Mtandao huo wa Health Line unaeleza wanawake wanaokabiliwa na ugonjwa huo huonesha dalili pia kipindi cha hedhi na ujauzito.

Hali hiyo inawafanya wanasayansi kuamini kwamba huenda linachochewa zaidi na homoni ya kike (Estrogen) ambazo huchochea  kupata ugonjwa huo. Hata hivyo, bado tafiti zinahitajika kuthibitisha ukweli wa mtazamo huo.

Mtandao wa Medicine Net unaeleza mjamzito mwenye tatizo la Lupus hupaswa kufuatiliwa hali yake kwa ukaribu zaidi kwani tatizo hilo huweza kusababisha kuharibika kwa mimba.

 

Visababishi

Pamoja na kuwa bado chanzo chake hakijulikani wala tiba yake haijapatikana, wataalamu wa afya wanaamini kwamba huenda ugonjwa huo unatokana na sababu za mabadiliko ya vinasaba na za kimazingira.

Inadhaniwa vitu ambavyo huchangia mtu kupata Lupus ni pamoja na msongo wa mawazo, miale ya jua, matumizi ya dawa za kulevya, maambukizi ya virusi vya Epstein-Barr (kwa watoto) na yale yatokanayo na baadhi ya kemikali, mwanga wa ‘ultraviolet’, matumizi ya sigara na antibiotics.

 

Changamoto zingine

Mtandao wa Health Line unaeleza wagonjwa wa Lupus hukabiliwa pia na tatizo la kushindwa kuganda kwa damu, kuvimba kwa mishipa ya damu, shinikizo la damu, mabadiliko ya tabia, kushindwa kutunza kumbukumbuku, kuvimba mapafu, moyo na hatimaye kiharusi.

Kwa mujibu wa mtandao huo, tafiti zinaonesha watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo huweza kuishi nao kwa miaka 40 ikiwa watapata matibabu sahihi.

 

Mkakati

“Dk. Mhehwa (marehemu) amekuwa chanzo cha watu wengi kuanza kuujua ugonjwa huu baada ya kufariki na ndipo nilipoona Profesa  Janabi akiizungumzia nikaona nimtafute ili tushirikiane kuutangaza,” Dk. Kilumanga.

Anasema wanakusudia kuanzisha taasisi ambayo itakuwa ikitoa elimu kwa umma juu ya ugonjwa huo.

 

Anasema katika nchi zilizoendelea wanaujua ugonjwa huo wa SLE ambapo kuna siku maalumu ya kuadhimisha ambayo ni Mei 10 kila mwaka.

 

“Anasema matibabu dhidi ya ugonjwa huo ni ghali mno ambapo mgonjwa hupewa dozi ya mwezi mmoja na vidonge wanavyopewa si tiba bali husaidia kupunguza maumivu kwa sababu inapofikia hatua za juu (acute stage) unaanza kushambulia viungo vya mwili.

 

Ombi kwa serikali

Balozi Kilumanga anaishauri serikali ianze kuandaa wataalamu watakaobobea kutibu ugonjwa huo tofauti na ilivyo sasa.

Pia anaishauri kununua vifaa vya kupimia ugonjwa huo ili watu waweze kugundulika mapema tofauti na ilivyo sasa ambapo wanaenda kugundulika nje ya nchi.

Balozi Chabaka Kilumanga pia anaiomba serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuangalia kwa undani suala hili ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo kitakachoangalia ugonjwa huu.

“Pamoja na kuanzisha kitengo hicho, ni muhimu pia kuangalia namna ya kuwapata wataalamu ambapo wataushughulikia ugonjwa huu,” anatoa rai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles