Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kupeleka haraka asilimia 65 ya fedha za mauzo ya nje ya korosho ghafi kwa Bodi ya Korosho ili zitumike kama zilivyokusudiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Ado Shaibu, alisema kutokupeleka fedha hizo kutasababisha gharama za uzalishaji kwa wakulima kuongezeka kutokana na ununuaji wa pembejeo kutegemea kwa asilimia 100 katika fedha hizo.
Alisema jambo hilo lilitokea mwaka jana kupanda kwa dawa aina ya salfa (Sulphur) katika maeneo mengi kutoka Sh 16,000 hadi kufika Sh 70,000.
“Kwa mujibu wa sheria ya korosho namba 18 ya mwaka 2009 kifungu 17(A), inaitaka Serikali kuingiza fedha hizo Bodi ya Korosho lakini fedha hizo hazijapelekwa kwa miaka miwili sasa,” alisema Shaibu.
Alisema hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Korosho iliyotolewa na kamati ya Bunge ya Maji, Kilimo na Mifugo kwa misimu miwili ya mauzo ya korosho, bodi haijapokea fedha hizo na hivyo kuleta athari mbalimbali katika kilimo hicho.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo inadai kuwa Bodi ya Korosho haijapokea Sh bilioni 211 ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 wanadai Sh bilioni 91 na 2017/18 wanadai Sh bilioni 110.
“Kutopeleka fedha hizi kutaathiri Kituo cha Utafiti cha Naliendele kinachozalisha mbegu bora za korosho na dawa za kudhibiti magonjwa ambacho kinategemea fedha hizo kwa asilimia 90 kujiendesha kitashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi,” alisema Shaibu.
Aliongeza kuwa athari nyingine ni kuvurugika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu ya usimamizi wa mfuko huo kutegemea fedha hizo kwa asilimia 100.
“Mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima na maofisa ugani yamesimama kwa sasa kutokana na kukosekana kwa fedha hizo,” alisema Shaibu.
Alisema wanamwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kulitolea ufafanuzi suala hili ili kuondoa mkanganyiko unaojitokeza.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama hicho, Shaibu, alisema umefikia hatua ya majimbo na kitaifa utafanyika Agosti 25 hadi 27, mwaka huu jijini Mbeya.
Alisema chama hicho kinapinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga, aliyoitoa hivi karibuni bungeni kuwa suala la uanachama wa Sahara Magharibi lina utata wa kisheria katika Umoja wa Afrika na katika duru za kimataifa.
“Tunapinga kauli hii kwa kuwa Tanzania tumekuwa mstari wa mbele kuwasaidia kupata uhuru wa Sahara Magharibi chini ya chama cha ukombozi cha Polisalio,” alisema Shaibu.
Akizungumza hivi karibuni, Waziri Mahiga, alisema Polisalio ni chama cha ukombozi kilichopewa hadhi ya Serikali na uanachama wa Umoja wa Afrika tangu 1982, lakini suala hilo limeanza kuleta utata kisheria.