25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI YA KUWA NA FAMILIA YENYE UTULIVU

Na Christian Bwaya


SOTE tunatamani kuwa na familia zenye utulivu. Utulivu una mambo matatu makubwa, kwanza; kuelewana. Kila mwanafamilia ni muhimu ajue mwenzake ana mahitaji gani, anapenda nini, hapendi nini, ana mipango gani na mambo mengine yanayomhusu.

Pili, Ushirikiano: Hapa tuna maana ya kila mwanafamilia kupigania lengo linalofanana. Yanapotokea mazingira ya kila mwanafamilia kupigania jambo lake binafsi, hatari ya kukosekana kwa utulivu inakuwa kubwa.

Lakini pia, kuna suala la kuaminiana kwa dhati. Hii ni ile hali ya kila mwanafamilia kutokuwa na wasiwasi na kile ambacho mwenzako anaweza kukifanya akiwa mbali na wewe. Unapomwamini mwenzako maana yake unakuwa na imani kuwa daima yuko upande wako na kamwe hawezi kuwa kinyume na wewe.

Ingawa ni kweli tunapenda haya yatokee, mara nyingine tunajikuta tukifanya mambo yanayopanda mbegu za mifarakano na hivyo kuondoa utulivu tunaouhitaji katika ngazi ya familia. Katika makala haya tunajadili siri tatu kubwa zinazojenga familia bora yenye utulivu.

 

Heshima

 

Familia huundwa na watu wenye nafasi tofauti tofauti. Wapo wazazi, baba na mama, wapo watoto kwa nafasi zao. Tukitaka kujenga familia bora yenye utulivu tuna kazi ya kuhakikisha si tu tunatambua wajibu unaotarajiwa kwetu kwa nafasi tulizonazo, lakini pia tuelewa mipaka yetu.

Kwa mfano, familia kama zilivyo taasisi nyingine lazima iwe na kiongozi anayeheshimika kwa nafasi yake. Huyu ni mtu mwenye ushawishi, nguvu na sauti ya mwisho pale uamuzi mgumu unapohitajika. Familia yenye watu wasioelewa nani ni kiongozi, familia yenye watu wanaogombania nafasi ya kuwa na sauti ya mwisho haiwezi kuwa na utulivu.

Pia, heshima ina maana ya kutokuwapo mtu anayepuuzwa kwa sababu yoyote ile. Tunafahamu wakati mwingine hutokea kuwapo kwa mtoto asiyefanya vizuri kama anavyotarajiwa awe. Uwezekano ni mkubwa mtoto kama huyu akajikuta akiwa daraja la chini katika familia. Hali kama hii inaweza kuwa chanzo cha misuguano.

 

Mawasiliano

Mawasiliano ni zaidi ya kusema kile unachofikiri. Mawasiliano ni uwezo wa kuelewa mwenzako ana mtazamo upi katika jambo hilo hilo. Familia yenye mawasiliano inampa kila mwanafamilia nafasi ya kutoa mchango wake wa mawazo. Kila mmoja anajisikia ana haki ya kusikika lakini pia anatambua wajibu wake wa kumsikiliza na mwenzake pia.

 

Moja ya sababu zinazoondoa utulivu katika familia, tafiti zinasema; ni tabia ya baadhi ya wazazi kudhibiti mno mawazo ya wanafamilia. Wanafamilia waliodhibitiwa kupita kiasi wanakuwa mithili ya kiumbe aliyenyimwa pumzi. Hali hii inaweza kuchangia migogoro ya chini chini inayoweza kuleta matatizo.

 

Kusudi la pamoja

Hakuna taasisi inayoweza kufika mbali bila kuwa na mwelekeo unaofuatwa na kila mwanataasisi. Hapa zinajitokeza dhana kama ‘maono/dira’ na ‘dhima’ ya taasisi zinazoongoza utendaji wa kila mwanataasisi.

 

Hata katika ngazi ya familia ni vyema kuwa na misingi inayoongoza utendaji wa kila mwanafamilia. Panahitajika utamaduni na tunu za familia zinazosaidia kujua kipi kuna umuhimu na hivyo kifanyike na kipi hakina umuhimu na hivyo kiachwe.

 

Familia yenye utulivu lazima iwe na dira inayoeleweka na kila mwanafamilia. Lazima kuwe na tabia zinazoitambulisha familia. Kama ilivyo kwenye taasisi nyingine, familia ya namna hii inakuwa na dhima ya pamoja inayoongoza mwelekeo wa kila mwanafamilia.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles