JANA tulianza mfululuzo wa makala maalumu ya afya, ambapo mwandishi wetu Veronoca Romwald amezungumza na wakunga na wazazi kuhusu hali ya uzazi Tanzania.
Wakunga na wazazi wameelezea changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika harakati za kuzalisha na kutafuta watoto.
Tunaendelea na makala hii, ambapo Muuguzi Mkunga Mwandamizi, Agnes Mtawa ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Msajili wa Baraza la Wakunga Tanzania anaelezea hali ilivyo.
Mtawa ambaye amehudumu miaka zaidi ya 20 katika fani hiyo, amepitia mambo mengi.
“Katika hospitali niliyokuwa nasimamia, kuna siku aliletwa mjamzito ambaye alifikishwa akiwa amechoka mno na bahati mbaya mtoto alifariki tukiwa zamu ya usiku tutachukua kitenge chake tukamstiri mtoto.
“Ndugu walipokuja asubuhi wakabaini kitenge hakikuwapo wakadai kwamba kilikuwa kimeibwa na wakunga tuliokuwa usiku ule, kwa haraka haraka tulikubaliana tulipe.
“Lakini tulifanya jitihada kuangalia kilienda wapi, tukakagua na kubaini kwamba tulimfungia mtoto baada ya kufariki dunia, ndugu walikuwa tayari wamekasirika hawakuwa na uchungu tena na kifo cha mtoto wao, bali walikuwa na uchungu na kile kitenge.
“Tulikubaliana kwamba mama akiletwa pale hospitalini (Muhimbili) kila kitu chake alichokuja nacho lazima kiandikwe pindi anapoingia na anapotoka, hatua hiyo ndiyo ilitusaidia kujua ukweli kwamba kitenge hakikupotea bali alifungiwa mtoto kumsitiri,” anasema.
Huwashusha morali
Mtawa anasema changamoto kama hizo zinapojitokeza na wakunga kutupiwa lawama, huwashusha morali ya kufanya kazi.
“Kwa sisi wazoefu, huwa tunajipa moyo tu kwamba ni changamoto za kazi, lakini kuna wakati inabidi mkunga aliyekumbana na changamoto ya kutukanwa au ndugu wa mgonjwa kumkejeli huwa tunalazimika kumpatia ushauri nasaha ili arudi katika ule moyo wa kufanya kazi,” anabainisha.
Ukweli ni kwamba, mkunga ni mtu muhimu mno katika kumsaidia mama tangu anapogundulika kuwa mjamzito, kipindi cha kulea ujauzito na hadi kujifungua.
Mkunga mtaalamu anatajwa kuwa mtu muhimu mno kwani msaada wake anaompatia mama katika vipindi vyote hivyo, unachangia kwa kiasi kikubwa kukabili vifo vitokanavyo na uzazi ambavyo kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) vinaonekana kuongezeka nchini.
Hali halisi
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), mwaka 2015/16 idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi imefikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000.
Takwimu hizo zinaonesha idadi hiyo imeongezeka kwani mwaka 2011/12 utafiti wa NBS unaonesha kulikuwapo na vifo 454 kwa kila vizazi 100,000.
Idadi hiyo ilikuwa pungufu ikilinganishwa na ripoti ya utafiti wa mwaka 2004/5 ambayo inaonesha vifo hivyo vilikuwa 578 kwa kila vizazi hai 100,000.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema kulingana na wastani wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000, inaamaanisha kwa siku wanawake wapatao 30 hufariki dunia wakati wa kujifungua na wastani wa wanawake 11,000 kwa mwaka.
Pia takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha wajawazito kuhudhuria kliniki katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kimeongezeka kufikia asilimia 98.
Aidha, kiwango cha wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya nacho kimeongezeka kutoka asilimia 47 hadi kufikia asilimia 63.
Idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano nayo imepungua kutoka asilimia 81 hadi kufikia asilimia 67 katika kila vizazi hai 1,000.
Hali ya vifo duniani
Kulingana na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA-Tanzania), inakadiriwa kila mwaka ulimwenguni wanawake wapatao 303,000 hufariki dunia wakati wa kipindi cha ujauzito na wakati wa kipindi cha kujifungua.
Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA – Tanzania), Jacqueline Mahon anasema takwimu za mwaka 2016 nazo zimeonesha watoto wapatao milioni 2.6 hufariki dunia wiki chache baada ya kujifungua.
“Hii inamaanisha watoto wachanga wapatao 7,000 hufariki dunia kila siku na asilimia 99 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania.
“Wakunga wataalamu ni kundi muhimu katika kukabili vifo vitokanavyo na uzazi, wana uwezo wa kutoa huduma bora ya afya ya uzazi inayojumuisha utunzaji wa mama na mtoto katika kipindi chote cha ujauzito na kujifungua.
“Hivyo basi, ni muhimu kuwa na mfumo na sera ya uuguzi inayoweka mazingira ya kazi yenye kuridhisha ili kuhakikisha wakunga waliopata mafunzo wanapangiwa na kubakia sehemu za kazi iliyo sahihi,” anasema.
Anasema pamoja na changamoto zilizopo, vifo vya kina mama vimeripotiwa kupungua kwa asilimia 44 ulimwenguni tangu mikakati ya kupunguza vifo ilipoanza miaka 25 iliyopita (1990 – 2015).
“Kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano, lakini bado kuna changamoto nyigi zinazohitaji kupewa kipembele ili tufikie malengo endelevu,” anasema.
Dk. Hashina Begum wa UNFPA – Tanzania, anasema takwimu zinaonesha wazi kwamba hali ya uzazi nchini bado si nzuri na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kupunguza vifo hivyo.
“UNFPA tumeendelea kuhakikisha tunashirikiana kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kusaidia kutatua changamoto zilizopo,” anasema.
JK na malengo ya 2030
Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, alisema anasikitishwa na ongezeko la idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi nchini na kwamba juhudi zaidi zinahitajika kuvikabili.
“Wakati naingia madarakani, ripoti ya utafiti iliyotolewa mwaka 2004/5 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilieleza kulikuwa na vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2004/5.
“Mwaka 2011/12 NBS walitoa ripoti nyingine ambayo ilionesha tulifanikiwa kupunguza idadi hiyo kufikia vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2011/12,” anasema.
Anasema mwaka 2015/16 NBS walitoa tena ripoti nyingine ambayo inaonesha idadi imeongezeka kufikia vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000.
“Kwa hiyo, maisha ya mama na mtoto yanapotea kila siku, hatuwezi kuzikataa au kuzikwepa takwimu hizi lazima tutafakari wapi tulikosea na tuchukue hatua, ili tuweze kufikia lengo la kidunia la kupunguza idadi kufikia vifo 70 ifikapo 2030,” anashauri na kuongeza:
“Napongeza juhudi na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli hasa kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.
“Ni hatua muhimu, kwani vinapokuwa karibu zaidi na wananchi maana yake watapata huduma kwa wakati,” anasema Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JMK Foundation) iliyozinduliwa hivi karibuni.
Anasema takwimu zinaonesha asilimia 51 ya wanawake hujifungulia kwa wakunga wa jadi na kwamba asilimia 49 pekee ndiyo ambao hujifungulia hospitalini ambako kuna wakunga wataalamu.
“Katika nchi za wenzetu hawa wanawatambua, kwa sababu ndiyo ambao wapo karibu zaidi na jamii, tuna changamoto ya watumishi, ni muhimu kuwekeza katika eneo hilo.
“Lakini si kila muuguzi anaweza kuwa mjuzi katika upande wa afya ya uzazi, naweza kusema ‘A nurse is good, but a Mid-wives is better,” anasema.