Maregesi Paul, Dodoma
Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (Chadema), amesema wafugaji wataendelea kutorosha mifugo na kuiuza nje ya nchi kwa kuwa mazingira ya ndani hayajaboreshwa kwa wafugaji.
Aidha, mbunge huyo ameitaka serikali kufuta tozo na kodi zilizoko katika sekta ya ufugaji kama ambavyo imekuwa ikifuta kodi na tozo hizo katika sekta ya kilimo.
Kalanga ameyasema hayo bungeni leo Mei 17, alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/19 iliyowasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo Luhaga Mpina.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Masele (Chadema), amelalamikia operesheni inayofanywa kwa ajili ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.
“Operesheni hiyo imejaa kasoro nyingi kwa kuwa wavuvi wananyanyaswa ikiwa ni pamoja na kupigwa na kutozwa faini kubwa zisizoendana na sheria za nchi,” amesema.
Hoja ya mbunge huyo iliungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Agnes Marwa (CCM), aliyelalamikia operesheni hiyo.