Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR
MBIO la kuwania urais wa Zanzibar zimeanza kupamba moto huku baadhi ya makada wa CCM wakiwamo mawaziri wa Serikali za Zanzibar na Jamhuri ya Muungano, wakitajwa kuanza kutafuta kuungwa mkono.
Makada hao wakiwamo mawaziri wanadaiwa kuanza kampeni kabla ya muda kwa lengo la kutaka kumrithi Dk. Shein mwaka 2020.
Hali hiyo inayoonekana kutaka kuleta vurugu ndani ya Serikali ya Zanzibar, imemfanya Rais wa Visiwa hivyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kuwaonya makada hao walioanza kampeni kabla ya muda.
Amewataka kutambua kuwa yeye bado ni Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa sheria.
Onyo hilo alilitoa jana kwenye mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Tunguu, Wilaya ya Kati Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema makada hao wameanza kupanga timu za urais badala ya kushughulika na mambo ya msingi ya ujenzi wa chama.
Alisema makada hao badala ya kufanya shughuli za ujenzi wa chama zitakazofanikisha kuibakiza CCM madarakan,i badala yake wanapanga safu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.
Dk. Shein alisema nafasi ya urais haipatikani kwa kampeni wala makundi yasiyokuwa halali ila hupatikana kwa utaratibu maalumu na kwa mujibu kanuni na Katiba ya CCM.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, aliwatahadharisha viongozi hao kwa kuwataka kuacha tabia hizo kwa sababu inaweza kuleta migogoro na mgawanyiko usiokuwa wa lazima ndani ya CCM kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema watu hao wanaosaka urais kwa sasa wasipoacha tabia hiyo na kuvumilia mpaka 2020, watachukuliwa hatua kali za nidhamu ikiwamo majina yao kufikishwa katika vikao vya Usalama na Maadili vya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) ili wahojiwe na kuchunguzwa kutokana na mienendo yao isyokuwa na manufaa.
Kamati hiyo ya Maadili na Usalama huongozwa na Mwenyekiti wa CCM ingawa kwa ngazi ya uchunguzi Makamu Mwenyekiti husimamia shughuli zote ikiwamo kufungua majalada ya wanaotajwa kila mkoa na wilaya ili kupata taarifa za wahusika.
Alisema viongozi, watendaji na wanachama wa CCM wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kukisaidia Chama kushinda na siyo kuhangaika kumrithi yeye kwenye urais.
“Naheshimu Katiba ya nchi, muda wangu ukifika naondoka madarakani kwa vile huo ndiyo utaratibu wa chama chetu na kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Lakini sifurahishwi hata kidogo kuona baadhi yenu mnaanza kuhangaika na urais badala ya kufanya kazi za kuitafutia ushindi CCM mwaka 2020,” alisema na kuonya Dk. Shein.
Aliwataka mabalozi na viongozi wengine wa ngazi za mashina kukataa kuingizwa katika mitandao hiyo ya kampeni.
Akizungumzia umuhimu wa viongozi hao, Dk. Shein alisema CCM inathamini mchango mkubwa wa kuimarisha chama unaofanywa na viongozi wa mashina ambao ndiyo jeshi la siasa la Chama Cha Mapinduzi.
Dk. Shein alisema chama kitaendelea kuisimamia vizuri serikali itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kama ilivyowaahidi wananchi katika kampeni za uchaguzi zilizopita.
Aliwataka viongozi hao kujenga utamaduni wa kusoma Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017 wajue majukumu yao kwa mujibu wa Katiba na kuyatekeleza ipasavyo.
Alisema katika hatua za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi, serikali inaendelea na mikakati ya matengenezo ya barabara ya Mwanakwerekwe na kutengeneza daraja la kisasa katika eneo la Kibonde Mzungu kuwaondolea usumbufu wananchi wa Mkoa wa Kusini Unguja.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.