FRANCIS GODWIN NA RAYMOND MINJA, Iringa
USHAHIDI wa kesi inayomkabili mwanafunzi, Abdul Nondo umeendelea kutolewa kwa upande wa Jamhuri kupeleka mashahidi wengine wawili kati ya wa nne.
Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi jana, ni pamoja na aliyekuwa mpenzi wa zamani wa Nondo ,Veronica Fredy (22) mkazi wa Igunga mkoani Tabora.
Shahidi huyo ambaye alifikishwa mahakamani hapo akiwa amefichwa sura yake kwa kufunikwa na polisi aliingizwa moja kwa moja mahakamani.
Baada ya kutoa ushahidi wake, alitolewa nje ya mahakama hiyo, chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo alipandishwa kwenye gari pa polisi lenye vioo vyeusi. Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, John Mpitanjia, shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa aliwahi kusoma na Nondo Shule ya Sekondari Igunga.
Alidai wakiwa shuleni, walikuwa kipindi chote cha masomo yao, huku Nondo akiwa kiongozi wake,baadaye waliingia kwenye mahusiano ya kimapenzi kabla ya kuachana muda mrefu.
Katika mahojiano yake na wakili wa Jamhuri,Alex Mwita na shahidi alisema elimu yake ni kidato cha sita na sasa anajishughulisha na kazi ya ususi wa nywele kijijini kwao Igunga.
Vero, alidai alimfahamu Nondo tangu Agosti,2014 na kuwa mazingira ya kufahamiana yalikuwa ya shuleni kama kiongozi wake na kuwa uhusiano wao wa mapenzi ulianza mwaka 2015 hadi mwaka 2017 mwanzoni,baada ya hapo wakaendelea na uhusiano wa kawaida.
Alisema njia ambazo walikuwa wakitumia kuwasiliana ni simu na mitandao ya kijamii, hasa Whatsapp na kusisitiza kuwa anachokumbuka ni Machi 7, mwaka huu saa 9 usiku, Nondo alimpigia simu.
“Ulikuwa usiku wa pekee nikiwa nasumbuliwa na mafua, nilipigiwa simu na Nondo akaniuliza uko wapi, nikamjibu nipo nyumbani Igunga,akaniuliza unaishi na nani, nikamweleza naishi pekee yangu, akaniomba aje kwangu ana matatizo nikamkatalia na kumkatia simu.
“Baada ya kukata simu, niliendelea kulala, ilipofika saa 10 usiku, simu yangu iliita nilipoitazama nikaona ni namba ya Nondo, safari hii akiomba nimpe namba ya rafiki yake Masumbuko, nikamwambia sina…baada ya hapo alikata simu,”alisema .
Akijibu swali la wakili upande wa utetezi, shahidi huyo alisema anatambua wapo watu wanaoigiza sauti mbalimbali, lakini alimtambua Nondo kupitia sauti yake namba yake.
Alisema wakati wakizungumza, Nondo alikuwa ni mtu anayeongea haraka haraka, huku akitumia namba ya mtandao wa Tigo inayoishia 25.
Alisema alitumia muda wa dakika tatu mara ya kwanza kuongea na Nondo usiku huo na mara ya pili, alitumia dakika kama nne hivi .
Hata hivyo,wakili wa upande wa utetezi, Kambone Jebra alihoji mtu anayesafiri kutoka Dar es salaam kwenda Igunga mkoani Tabora,lazima afike mkoani Iringa, kama ni hivyo aliwezaje kuitambua sauti ya Nondo kwa njia ya simu wakati inaweza kuigizwa kwa mfano, msanii Steve Nyerere amekuwa akiingiza sauti nyingi analitambua hilo.
Alisema naalitambua, lakini alipohojiwa kuwa hakuumia alipoachana na Nondo kama mpenzi wake, alisema hakuumia.
Akijibu maswali ya wakili huyo, shahidi huyo alikiri mtu anayekwenda Tabora, si lazima apite Iringa na kuwa anakubaliana kuwa wapo wanaoweza kuigiza sauti za watu kama anavyofanya msanii Nyerere.
Alipoulizwa kama bado anampenda Nondo, alikataa kuendelea kumpenda, lakini alibanwa zaidi kuwa imekuwaje kama hampendi amekwenda mahakamani kumtolea ushahidi.
Shahidi huyo alijibu kuwa anampenda kama binadamu mwingine na si mpenzi.
Veronica ambaye ni shahidi wa tatu katika kesi hiyo, alisema amepata kuishi Mtaa wa Semtema eneo la Kihesa katika nyumba ya mzee Chusi na wakati huo alikuwa akisoma chuo cha Kikuu cha Tumaini, japo alisema katika kuishi kwake Iringa hafahamu hata uwanja wa Somora.
Naye shahidi wa nne,PC Abdul karim kutoka Kitengo cha Makosa ya Mtandao makao makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, alieleza mahakama kuwa alipokea vielelezo kutoka kwa Koplo John, vikiwamo kompyuta mpakato na simu ya mkononi.
Alisema baada ya kupokea vifaa hivyo, alivihifadhi ndani ya kabati lake,baadae alifanyia uchunguzi na kubaini vitu kadhaa ndiyo amevikisha mbele ya mahakama ili vitumike kama vielelezo vya ushahidi .
Hata hivyo, upande wa utetezi kupitia wakili Kambone aliomba mahakama kutokupokea kilelezo hicho kwa kuwa kina upungufu mwingi.
Hakimu Mpitanjia, aliitaka Jamuhuri iwe na muda mzuri wa kupitia vielelezo ili kujiridhisha na kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho.