NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
WATAALAMU wa mitandao wametoa wito kwa jamii juu ya matumizi salama ya mitandao ili kupunguza uhalifu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa mawasiliano, mtaalamu wa usalama katika mitandao na uchunguzi wa makosa ya digitali, Yusuph Kileo, alisema matumizi mabaya ya mitandao yasipodhibitiwa yanaweza kuchangia kuyumba kwa mataifa mbalimbali duniani.
“Wakati huu tukiwa tunaelekea Uchaguzi Mkuu lazima tujue mitandao ya kijamii inaweza kabisa kuyumbisha taifa letu, hivyo hakuna budi kuwa na umakini madhubuti katika hili,” alisema Kileo.
Alisema baadhi ya nchi ziliyumba na kuanguka huku sababu kuu ikiwa ni mitandao ya kijamii kuchochea fujo katika nchi hizo.
Kileo alizitolea mfano nchi zilizoathirika na mitandao ya kijamii kuwa ni Misri, Libya na nyinginezo.
“Ni wakati mwafaka kwa wadau mbalimbali kutambua athari kubwa katika nyanja zote kuanzia kiuchumi hadi kisiasa zinazoweza kuonekana kama usalama mtandao hautaangaziwa macho ipasavyo,” alisema Kileo.
Pia, Mkurugenzi wa kitengo cha Mawasiliano (Tehama) kutoka TTCL, Injinia Peter Philip, alisema kuunganishwa kwa mkongo wa taifa kumesaidia kuwaleta wadau kutoka nchi mbalimbali.
Alisema kabla ya mwaka 2010, bei za kupiga simu na intaneti zilikuwa juu lakini kadiri siku zinavyokwenda zimezidi kupungua hadi kufikia asilimia 90 hivyo jitihada zinatakiwa kufanyika kwa kasi ili kuweka sheria madhubuti za usalama wa mitandao.
Philip alisema ni vyema nchi mbalimbali zikaunganishwa katika mkongo huo huku akisisitiza kufanyika pia ushirikishwaji wa mitandao.
Naye, Waziri wa Tehama wa Lesotho, Khotso Letsatsi, alisema wimbi kubwa na matumizi mabaya ya mitandao nchini kwao ndilo limeendelea kuwa kikwazo cha maendeleo yao.
Alisema ana mikakati ya kuandaa sera pamoja na sheria ya mitandao ili kuhakikisha anahimili vishindo vya ukuaji wa matumizi mabaya ya mitandao.
Kwa upande wake, Waziri wa Tehama wa Burundi, Tharcisse Nkezabahizi, alisema ni vyema jamii kila nchi ikahakikisha usalama wa mitandao ili kujilinda na wahalifu wanaotumia mitandao vibaya.
Alisema anaamini kabisa tatizo kubwa ni upungufu wa ukuzaji wa uelewa juu ya mambo ya usalama wa mitandao pamoja na Serikali nchi za Afrika kutokuona usalama mitandao ni kipaumbele huku wakisahau uhalifu wa mtandao una uwezo mkubwa wa kuangusha taifa lolote.
“Uhalifu wa mitandao una uwezo zaidi wa kuangusha taifa lolote hivyo ni vyema Serikali katika nchi husika ikajipanga kupambana na uhalifu wa mitandao,” alisema.