33.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU SHOO ATUMA TENA UJUMBE MZITO

Na Upendo Mosha-Moshi


MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Fredrick Shoo, amesema anatamani kuona Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla wanakuwa na sauti za ujasiri kwa kuonya watu wamuogope Mungu kwa yale maovu yanayofanyika.

Dk. Shoo ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, aliyasema hayo jana wakati akiongoza ibada ya Jumapili katika Usharika wa Msaranga mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika dunia hii iliyojaa watu wenye midomo michafu, watu  waliojaa viburi na unafiki mkubwa ambao hawaoni madhaifu yao, ni vema Watanzania na Wakristo wakaungana katika kuonya watu hao, lengo likiwa ni kuwafanya waishi kwa amani na hofu ya Mungu.

“Katika dunia hii iliyojaa watu wenye midomo michafu, watu wenye viburi, wenye unafiki mkubwa, wenye kukata tamaa na wanaokataa kuonywa na wasioona madhaifu yao na wanaokataa kutubu, Yesu anasema nimtume nani awapelekee ujumbe. Kwa mantiki hiyo natamani kuona Wakristo wakaotekeleza haya bila hofu,” alisema.

Alisema kanisa linatamani kuona Watanzania wanaishi katika hali ya amani, upendo, mshikamano na maelewano pasipo kujali vyeo vyao wala  itikadi zao za  kisiasa na ubaguzi wa kikabila na ukanda.

“Natamani sana watoke Wakristo na Watanzania ambao watakuwa tayari kusema nitume mimi bwana katika kutoa maonyo dhidi ya watu wa aina hiyo, kwani hili litafanya Watanzania wote waishi kwa amani, upendo na mshikamano pasipo kujali itikadi za kisasa wala kabila,” alisema.

Alisema kumekuwa na watu ambao wamekuwa wakijinadi kwa maneno mazuri katika kuhubiri amani  na mshikamano, jambo ambalo halina uhalisia na kwamba Wakristo na Watanzania wana wajibu wa kusimama na kuhubiria amani na mshikamano wa kweli kwa vitendo.

“Katika nchi yetu kumekuwa na watu wanaojua kuyapamba maneno kwelikweli  na wanahubiri amani ya Yesu mfufuka, lakini maisha yao na mienendo yao ipo kinyume kabisa na hilo, hivyo wakati umefika Wakristo tuhubiri  haki ya kweli, upendo na mshikamano,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles