23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: VIONGOZI WA DINI SITAWAANGUSHA

ELIYA MBONEA Na JANETH MUSHI-ARUSHA


RAIS Dk. John Magufuli, amewahakikishia viongozi wa dini nchini, kwamba Serikali yake haitawaangusha kwani inatambua mchango wao.

Rais Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana mjini hapa akiwa mgeni rasmi kwenye ibada ya kusimikwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isack Aman, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu.

Akizungumza kwenye ibada hiyo, Rais Dk. Magufuli alilitaka kila dhehebu kwa imani yake kutambua kwamba Serikali yake ipo pamoja nao.

“Natambua Serikali haina dini, viongozi wake waliomo ndani ndio wana dini. Kwa hiyo, nawahakikishia kwamba natambua mchango mnaoutoa na kama kiongozi wenu, sitawaangusha, nipo pamoja na ninyi,” alisema Rais. Dk. Magufuli.

MAOMBI MATATU YA KANISA

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadri, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Aloyce Kitomari, alimuomba Rais Dk. Magufuli ihamishwe Shule ya Msingi Naura, iliyopo jirani na kanisa pamoja na Kituo cha Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani.

Pia, alitaka kanisa hilo limilikishwe bustani iliyopo mbele ya kanisa lao na pia awasaidie kufutiwa kodi ya mapato kwa Shule ya St. Jude.

Akijibu maombi hayo kwenye hotuba yake, Rais Dk. Magufuli alisema maombi hayo ni magumu, hivyo hawezi kuwa na majibu ya moja kwa moja.

“Shule ya Msingi Naura iliyopo Kata ya Sekei kwa taarifa nilizonazo, ilianzishwa mwaka 1950 ikiitwa St. Theresia Primary School. Lakini, mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha, shule hiyo ilitaifishwa na kuitwa Shule ya Msingi Naura.

“Juni 16, mwaka 1996, kanisa lilitafuta hati namba 8848, ambapo hati hiyo ilijumuisha eneo la shule hiyo iliyotaifishwa.

“Hapo ndipo kwenye changamoto ingawa ni kweli kabisa shule ipo kwenye mazingira ya kanisani.

“Lakini, mali zilizotaifishwa nchi hii ni nyingi na aliyetaifisha hayupo, sasa unaweza kusimama kusema unarudisha hiki matokeo yake nitakuwa nimefungua boksi la kila mmoja kurudisha vitu vilivyotaifishwa na Serikali.

“Hii ndiyo changamoto kubwa ninayoiona na ndio maana sitaki kutoa jibu hapa, naweza kurudisha shule hii baadaye pakawa mgogoro mkubwa nchi nzima.

“Kuna majengo mengi yaliyomilikiwa na kanisa na Kardinari Polycarp Pengo amekuwa akiniandikia kuomba baadhi ya majengo yaliyoko Bagamoyo.

“Nayo nataka nimueleze jibu hapa kwamba hapana. Ili anisamehe kama nayo ni dhambi, basi anisamehe moja kwa moja. Nitakwenda kumweleza sababu za msingi nikifika Dar es Saalam kwa sababu waliokuwapo waliuza na fedha wakapewa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli alilipongeza Jimbo Kuu la Arusha kwa kuwa na miradi mingi ya maendeleo ambayo wamekuwa wakishirikiana na Serikali zikiwamo shule za awali 16, shule za msingi 19 na shule za sekondari 11.

“Nawapongeza kwa kuwa na hospitali tatu, vituo vya afya sita, zahanati 15, kituo cha walemavu kimoja na kituo cha yatima kimoja. Haya mnayoyafanya, mnayafanya kwa kuwatumikia Watanzania na Mungu pia,” alisema.

PADRI KITOMARI

Awali, akisoma risala ya wanafamilia ya wana wa Mungu Arusha, Padri Kitomari alisema wanaendelea kumuombea Rais Dk. Magufuli na Taifa la Tanzania liendelee kuongozwa na ukweli wa Kimungu usio na unafiki ndani yake kama asemavyo Kristo.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles