31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AWAAMBIA MAPADRE ARUSHA MAOMBI YAO NI MAGUMU

Eliya Mbonea na Janeth Mushi, Arusha

Rais John Magufuli amewahakikishia viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali nchini kwamba Serikali yake haitawangusha kwani inatambua mchango wao huku akiwasisitiza kuhubiri amani.

Aidha, amewaambia mapadre mkoani Arusha kuwa maombi yao matatu yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Mapadri Jimbo Kuu la Arusha, Padri Aloyce Kitomari ambaye alimuomba kuihamisha Shule ya Msingi Naura iliyopo jirani na Kanisa na Kituo cha Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani, kumilikishwa bustani iliyopo mbele ya Kanisa na kufutiwa kodi ya mapato kwa Shule ya St. Jude, kuwa ni magumu, hayawezekani..

Akizungumza mjini hapa leo Jumapili Aprili 8, mjini hapa akiwa mgeni rasmi kwenye ibada ya kusimikwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isack Aman iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu ambayo pia imehudhuriwa viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na mkewe, Rais Magufuli amelitaka kila dhehebu kwa imani yake kutambua kwamba Serikali yake iko pamoja nao.

“Natambua Serikali haina dini, viongozi wake waliomo ndani ndiyo wana dini zao, niwahakikishie, natambua mchango mkubwa mnaoutoa kama kiongozi wenu sitawaangusha, nipo pamoja na ninyi,” amesema Rais Magufuli.

Akijibu maombi hayo, Rais Magufuli amesema maombi hayo ni magumu hivyo hawezi kutoa au kuwa na majibu ya moja kwa moja.

Amesema Shule ya Msingi Naura iliyopo Kata ya Sekei kwa taarifa alizonazo ilianzishwa mwaka 1950 ikiitwa St. Theresia Primary School. Lakini mwaka 1967 wakati wa Azimio la Arusha shule hii ilitaifishwa na kuitwa Shule ya Msingi Naura.

“Mwaka 1996 Kanisa lilitafuta hati namba 8848 Juni 16, mwaka 1996 ambapo hati hiyo ilijumuisha eneo la shule hiyo iliyotaifishwa ndani. Hapo ndipo kwenye changamoto, ni kweli kabisa shule ipo kwenye mazingira ya kanisa, lakini ilitaifishwa.

“Lakini mali zilizotaifishwa nchi hii ni nyingi na aliyetaifisha hayupo, sasa unaweza kusimama kusema unarudisha hiki matokeo yake nitakuwa nimefungua boksi la kila mmoja kurudisha vitu vilivyotaifishwa na serikali.

“Hii ndiyo changamoto kubwa ninayoiona na ndiyo maana sitaki kutoa jibu hapa, naweza kurudisha shule hii baadaye pakawa mgogoro mkubwa nchi nzima,” amesema Rais Magufuli.

Amesema yapo majengo mengi yaliyomilikiwa na kanisa na kwamba Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Muhadhama Kadinali Polycarp Pengo, amekuwa akimuandikia kuomba baadhi ya majengo yaliyoko Bagamoyo.

“Nayo nataka nimueleze jibu hapa kwamba hapana. Ila anisamehe, kama nayo ni dhambi basi anisamehe moja kwa moja hapa. Nitakwenda kumueleza sababu za msingi nikifika Dar es Saalam kwa sababu waliokuwapo waliuza na fedha wakapewa,” amesema.

Akifafanua kuhusu maombi ya bustani, Rais Magufuli amesema bustani hiyo inayopita pembeni mwa Barabara ya Uhuru na Mto Naura kwa mujibu wa nyaraka zinaonyesha kuwa ni eneo la wazi.

“Kwa mujibu ya Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 unapokuwa kwenye Mto, Ziwa au Bahari huwa ni Mita 60 kutoka hapo na sheria ni msumeno.

“Hili nalo naliona bado ni gumu, najaribu kuzungumza haya nakujitahidi kuzungumza kwa uwazi ili ndugu Wakristo muwe upande wangu nanyi muone kama mngekuwa Rais mngefanyaje?” Amehoji Rais Magufuli.

Kuhusu kuondolewa kodi kwa Shule ya St Jude, amesema “Padri Kitomari amezungumza shule inayodaiwa Sh bilioni mbili, sasa zimeongezeka kufikia Sh bilioni sita nalo kwangu bado ni gumu, ugumu wake nimeambiwa kuna kesi mahakamani”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles