Na MALIMA LUBASHA
CHAMA cha Wafugaji Wilaya ya Serengeti, kinatarajia kuchangia ng’ombe 300 katika ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya hiyo ambayo inaendelea kujengwa huku michango ikiendelea kukusanywa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji (CCWT) Kanda ya Ziwa, Mrida Mshota alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa uchaguzi wa viongozi wapya wa chama hicho.
Alisema wafugaji ni kundi kubwa linalomiliki uchumi mkubwa lakini mchango wao katika shughuli za maendeleo siyo wa kuridhisha.
Mshota alisema kutokana na wingi wa mifugo waliyonayo kila wilaya inatakiwa kuchangia ng’ombe 300 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya iweze kukamilika na kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Alisema Wilaya ya Serengeti inakadiriwa kuwa kinara katika Mkoa wa Mara kwa kuwa na ng’ombe zaidi ya 400,000, hivyo utajiri huo unatakiwa usaidie kuleta mabadiliko kwa wafugaji na wilaya kwa kuchangia shughuli za maendeleo zinazobuniwa na viongozi wao.
“Haiwezekani viongozi wetu waende kuomba msaada kwa watu wa nje ya wilaya kuwajengea hospitali wakati sisi tupo na rasilimali hii, kwani watakaonufaika ni wananchi wote,” alisema.
Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Chandi Marwa alichangia ng’ombe wanane, mbuzi saba na Sh milioni moja, huku akiwaomba wafugaji wenzake kutojiona wanyonge wakati wanamiliki uchumi mkubwa kupitia mifugo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji (CCWT) Wilaya ya Serengeti, Mtiro Marinya, alisema watapita vijiji vyote 78 na kata 30 za wilaya hiyo kuunda uongozi wa wafugaji kuhamasisha kampeni ya kujenga hospitali kwa ng’ombe mmoja.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, aliwataka viongozi wa chama hicho kuwaelemisha wafugaji waheshimu sheria na taratibu za mifugo na kuepuka migogoro.