24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI WA CUBA ATIMULIWA ZAMBIA

LUSAKA, ZAMBIA


SERIKALI ya Zambia inamulikwa na jumuiya ya kimataifa baada ya kumtimua balozi wa Cuba kwa kuhudhuria uzinduzi wa chama kipya cha siasa cha upinzani cha Socialist Party (SP).

Balozi huyo, Nelson Pages, alijikuta katika hasira ya Serikali ya Zambia kwa kudaiwa kuunga mkono ‘mapinduzi’ ya Serikali ya taifa hilo.

Hata hivyo, Balozi Pages akamenusha madai hayo kwa kueleza kuwa yeye ni mshiriki tu wa mfumo wa demokrasia.

Ingawa Zambia imekuwa na uhusiano wa karibu na Cuba kwa zaidi ya miaka 60, uamuzi wa Balozi Pages kuhudhuria mkutano wa kisiasa wa siku moja wa chama upinzani umekuwa sumu kwa historia hiyo ndefu ya ushirikiano.

Pages aliwasili Zambia Alhamis iliyopita kuliwakilisha taifa lake kidiplomasia nchini Zambia na siku mbili baadaye alishiriki mkutano huo wa kisiasa.

Ni baada ya tu kushiriki mkutano huo ndipo alipotimuliwa akiwa ameingia katika ofisi yake kwa siku moja tu.

Rais wa Zambia, Edgar Lungu kupitia kwa msemaji wake, Amos Chanda alisema kuwa tabia ya Balozi Pages akiwa Zambia kwa siku moja tu imeonyesha hajui kazi yake na yuko tayari kuvunja kila mustakabali wa ubalozi mwema.

Lakini vyombo vya habari vya kimataifa vimemshangaa Rais Lungu baada ya kuibuka na msimamo kuwa kitendo cha balozi wa kigeni kushiriki mkutano wa upinzani si kitu kipya nchini humo.

Katika ripoti zake kuhusu tukio hilo, vimekikumbusha chama chake ambacho sasa kiko madarakani cha Patriotic Front (PF) wakati kikiwa chama cha  upinzani mwaka 2011, kilimwalika Balozi wa Marekani wakati huo, Mark Storella, katika hafla yake ya kisiasa na akahudhuria.

“Leo hii Rais Lungu akiwa madarakani anaona hilo ni kosa, lakini ilikuwa sawa kwa chama chake wakati huo kikiwa upinzani kufanya hivyo.

“Rais wa wakati huo, mwaka 2011, Rupiah Banda hakuchukua hatua au kukasirishwa na hatua ya Balozi Storella kushiriki hafla ya upinzani kama ambavyo Lungu anafanya leo,” kimeripoti moja ya vyombo hivyo.

Rais Lungu anajitetea kuwa Balozi Pages katika hotuba yake ya kisiasa alikiahidi chama hicho uungwaji mkono na Cuba.

“Huyu balozi anapaswa aelewe kuwa hakutumwa hapa na Cuba kuwakilisha maslahi ya chama cha siasa bali kuwakilisha maslahi ya taifa lake na letu.

“Hatutaki aegemee chama tawala kwa kuwa hiyo si kazi yake, na pia hatutaki aegemee mrengo wa upinzani kwa kuwa pia hicho si kilichomleta.”

“Tunachotaka ni balozi ambaye anajielewa na anayeelewa kazi yake,” alisema Rais Lungu katika taarifa yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles