Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka matatu yakiwamo kufanya uchochezi wa chuki kwa wananchi dhidi ya serikali.
Heche amefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi aprili 5, baada ya kujisalimisha polisi alikokua akishikiliwa tangu juzi.
Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, Heche anadaiwa kutenda kosa hilo akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Buibui Kinondoni, jijini Dar es Salaam Februari 16, mwaka huu.
Katika mashtaka mengine, anadaiwa kufanya mkusanyiko pamoja usio halali pamoja na wenzake saba akiwamo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na kuendelea kukusanyika na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Aquilina Akwilini na askari kujeruhiwa.
Heche ameunganishwa katika kesi inayowakabili viongozi wengine saba wa chama hicho waliopata dhaman juzi baada ya kukaa mahabusu ya Segera kwa siku tano.