26 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI WA RELI YA KISASA UTAKAVYONUFAISHA WANANCHI

NORA DAMIAN, DAR Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


RAIS Dk. John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (Standard gauge), kutoka Dodoma hadi Morogoro, huku akisema anataka Tanzania iwe kama Ulaya, kwamba mtu anaweza kufanya kazi Dodoma na kuishi Dar es Salaam.

Akizindua reli hiyo, alisema miundombinu imara ya usafiri ni kichocheo muhimu cha ukuaji uchumi katika nchi na kwamba bila miundombinu hiyo ni ndoto kupata maendeleo.

“Kukosekana kwa miundombinu imara na ya uhakika, imesababisha gharama za usafiri kuwa juu kulinganisha na maeneo mengine duniani,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wastani wa bei ya kusafirisha kontena moja la futi 20 kwenye nchi za Afrika Mashariki umbali usiozidi kilomita 1,500 ni Dola za Marekani 5,000 na kwamba bei hiyo ni sawa na gharama ya kusafirisha kontena lenye ukubwa kama huo kutoka China hadi Tanzania umbali wa kilomita 9,000.

“Tafiti zinaonyesha pia kukosekana kwa miundombinu imara ya usafiri kunashusha pato la nchi za Afrika kwa asilimia kati ya moja na mbili na kuongeza gharama za usafirishaji kwa asilimia 40.

“Hali hii inasababisha nchi zetu zishindwe kushindana na nchi zingine katika masuala ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya viwanda,” alisema.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, ripoti ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ya 2015 kuhusu usafiri wa reli, inaonyesha usafiri wa reli ni muhimu kwani ni mhimili mkubwa kwa maendeleo ya kiuchumi na usipoboreshwa, Afrika haitaweza kutumia rasilimali na utajiri ilionao.

Alisema utendaji kazi wa reli zilizopo sasa si wa kuridhisha kutokana na uwekezaji mdogo na ubovu wa miundombinu na matatizo ya uongozi yaliyokuwapo.

“Siku za nyuma reli hii ilibinafsishwa kwa kampuni moja na ilikaa kwa miaka zaidi ya mitano, lakini hakuna ilichofanya,” alisema.

 

FAIDA RELI YA KISASA

Magufuli alisema nchi yoyote ili iweze kujitegemea, ina wajibu wa kumiliki vitu muhimu kama reli, bandari, nishati, barabara, mawasiliano na vingine.

Alisema ujenzi wa reli ya kisasa utaongeza tija na ufanisi katika usafiri wa reli nchini kwani utarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria.

“Mtu atasafiri kwa kutumia saa tisa hadi Mwanza kutoka saa 36 kwa kutumia usafiri wa reli uliopo sasa, itaongeza biashara hapa nchini na nchi jirani,” alisema.

Alisema kati ya nchi nane ambazo Tanzania inapakana nazo, sita hazina bahari na zinategemea kusafirisha mizigo kupitia hapa nchini.

“Itaimarisha biashara kati ya nchi yetu na nchi za Burundi, DRC, Rwanda na Uganda. Itasaidia kutunza barabara na kupunguza gharama za kuzikarabati mara kwa mara.

“Itakuza sekta zingine za kiuchumi kwani nyingi zinategemea miundombinu ya usafiri wa uhakika.

“Nchi nyingi zimeshindwa duniani, zinakopa halafu zinapewa masharti makubwa, wapo wengine wamejaribu lakini wamejenga ya ovyo tu,” alisema.

Alitoa wito kwa Wizara ya Ujenzi, mshauri msimamizi na mkandarasi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

 

VYUMA KUKAZA

Alisema ujenzi wa kilomita 726 za reli ya kisasa utatoa ajira 30,000 za moja kwa moja na 600,000 zisizo za moja kwa moja zitatolewa, hivyo kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira nchini.

“Suala la ajira tumelijibu kwa vitendo kwa kuwa na miradi mikubwa kama hii, hivyo nawaomba Watanzania msichague kazi.

“Serikali inahamia Dodoma na mimi mwaka huu nahamia, fursa nyingi zimekuja hasa za ujenzi.

“Mkandarasi akishaanza hapa, nitashangaa sana kama wananchi wa Ihumwa watakuwa hawaji kufanya kazi, vya bure hakuna na asiyefanya kazi asile na asipokula afe, hii ndiyo lugha ya ukweli na siku zote tutawaambia ukweli.

“Kama kuna miradi yote hii halafu awepo mtu analalamika njaa, vyuma vimebana, amejibanisha yeye mwenyewe vyuma, avifungue kwa kufanya kazi,” alisema.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles