Na Joyce Kasiki, Dodoma
Jumla ya Sh trilioni 10.004 zimetengwa katika mwaka ujao wa fedha 2018/19, kwa ajili ya kulipia deni hilo deni la taifa.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Philip Mpango amesema hadi kufikia Desemba mwaka jana deni la taifa lilifikia Dola za Marekani milioni 21,308.7 sawa na Sh bilioni 47,756.3 (trilioni 47.7) ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 20,766.3 sawa na Sh bilioni 46,081.42 (trilioni 46.081) Juni mwaka jana.
Dk. Mpango amesema hay oleo Jumanne Machi 13, wakati akiwasilisha kwa wabunge mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19.
Amesema kati ya kiasi hicho deni la nje lilikuwa Dola za Marekani milioni 15,237.0 sawa na Sh bilioni 34,148.6 (Sh trilioni 34 .148) ikiwa ni asilimia 71 .5 ya deni lote ambapo deni la ndani lilikuwa Dola za Marekani milioni 6,071.7 sawa na Sh bilioni 13,607.7 (Sh trilioni 13.3) sawa na asilimia 28.5 ya deni lote.
“Ongezeko la deni hilo, lilitokana na kupokelewa kwa mikopo ambayo mikataba yake ilikwishaingiwa pamoja na mikopo ya ndani mipya kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo,” amesema Dk. Mpango.
Hata hivyo, Waziri huyo amesema,deni hilo bado ni himilivu kwa kipindi cha muda wa kati na muda mrefu ,kutokana na tathimini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba 2017 kwa kipindi kilichoishia Juni 2017.