Na Omary Mlekwa, Hai
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, kimetoa msaada wa vifaa vya ujenzi kwa Shule ya Msingi Kibohehe ili kukarabati shule hiyo kutokana na mvua kubwa iliyosababisha kuanguka kwa ukuta na kuua mwanafunzi mmoja wa darasa la sita.
Kwa sasa shule hiyo imefungwa na serikali kupisha ukarabati wa miundombinu yake huku wanafunzi wakiwa wamehamishwa katika shule za jirani.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa CCM wilayani hapa, Wang’uba Magai amesema lengo la msaada huo ni kuunga jitihada za kuboresha miundombinu ya shule hiyo na kuwarejesha wanafunzi shuleni hapo.
“Katika ilani ya chama chetu inaelezea umuhimu wa elimu kwa jamii, kitendo cha kuharibika kwa miundombinu ya shule hii zisipochukuliwa hatua za haraka inaweza kuwa kero kwa wanafunzi waliokuwa wanasoma hapa,” amesema
Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Yohana Sintoo alisema kutokana na uharibifu uliotokea katika shughuli wameamua kujenga vyumba vya sita vya madarasa ambavyo vitakumika katika shule hiyo
“Tathimini iliyofanywa na Wahandisi wa Wilaya ni kuwa madarasa yote ya upande mmoja yatavunjwa na kujengwa upya kwa gharama ya Sh milioni 207 ,” amesema.