33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

MNYIKA: MSAJILI ANATAKA KUIFUTA CHADEMA, HATAWEZA

Na MWANDISHI WETU

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John Mnyika, amedai wamebaini kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ana njama za kufuta usajili wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini, na kudai malengo hayo hayatafikiwa.

Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari, Mnyika alisema wamebaini hayo kutokana na barua waliyoandikiwa na Msajili, akiwataka waeleze kwanini wasichukuliwe hatua kutokana na maandamano waliyofanya Februari 16, kabla ya kutawanywa na polisi.

“Kama wanafikiri wana uwezo wa kukifuta Chadema wajaribu, ipo sheria ya vyama vya siasa. Wakizuia mlango wa demokrasia ipo njia nyingine ya kufanya siasa nje ya demokrasia na vyama vya siasa,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema Msajili anapaswa kusema hatua alizochukua baada ya mikutano ya hadhara na maandamano kuzuiwa na kutoa kauli ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, jijini Dar es Salaam, Daniel John.

Alisema siku hiyo ya maandamano hakuna kiongozi, mfuasi au mwanachama wa chama hicho aliyefanya vurugu siku ya kufunga kampeni za uchaguzi wa Kinondoni na kwamba kinachopaswa kulaaniwa ni kufyatuliwa kwa risasi za moto dhidi ya watu waliokuwa hawana silaha na kusababisha majeruhi na kifo.

Alidai mashambulizi hayo yaliwalenga viongozi wa chama hicho.

Pia alikosoa uandishi wa barua ya Msajili akisema:  “Alitaka tujieleze juu ya Jimbo la Ubungo na Mwananyamala kwa Kopa na wala haipo Ubungo, inaonekana amekurupuka. Kwamba tumevunja kifungu cha sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 cha 9 (2), hiki kinatoa masharti kwa chama kinachoomba usajili wa muda na chama chetu hakiombi usajili wa muda kwa wakati huu. Amekosa kifungu na kutupa cha vyama vya siasa vyenye usajili wa muda,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema katika barua hiyo ya Msajili yenye Kumb: HA. 322/362/16/34 ya Februari 21, mwaka huu, ilitumia pia kanuni ya maadili ya vyama vya siasa ya 6 [1, (b)] ambacho kinamtaka kupokea malalamiko na kusikiliza pande zote, lakini barua hiyo haikueleza iwapo alipokea malalamiko kutoka upande upi.

“Hii inampa Msajili kutumia pande mbili na kusikiliza malalamiko, lakini hakueleza mlalamikaji ni nani, kajigeuza yeye mlalamikaji, hakuwa na hoja, tunaelewa tuko katika shambulizi pande zote za serikalim, Msajili anasukumwa,” alisema Mnyika.

Alisema dhamira inayoonekana ni kutaka kukifuta Chadema, jambo ambalo haliwezekani.

Mtanzania iliona barua ya Chadema kwenda kwa Msajili yenye kumbukumbu namba C/HQ/ ADM/ 17/MSJ/04/115 ya Februari 22, ambayo ilidai barua ya Msajili haina sehemu iliyomnukuu Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ikionyesha kukiukwa kwa masharti ya Sheria na Maadili ya Vyama vya Sisa.

“Ni ngumu kutoa maelezo kwa madai na tuhuma ambazo ni jumuishi, ni vyema ofisi yako ikaeleza na kunukuu maneno hayo na ieleze pia kama yalizua taharuki kwa nani au yamemchochea nani, ili iwe rahisi kutoa maelezo,” ilisema barua hiyo.

Katika hatua nyingine, Mnyika alisema wapo watu watatu ambao aliwataja kama Aida Ulomi, Isack Ngada na John, ambao wako mikononi mwa Jeshi la Polisi, huku wakiwa na majeraha ya risasi, lakini hawajafikishwa mahakamani na hawapati matibabu sahihi.

“Hawa majeruhi wa sasa wa risasi hali zao si nzuri, lakini mawakili wanashughulikia hilo, kwani hawajapata matibabu yanayostahili, haki za binadamu na walione hili na wafuatilie. Isack alikamatiwa Kibaha alikokuwa akiendelea na matibabu, John kakamatwa leo (jana). Waliopigwa risasi wanakamatwa ili kuficha kuwa si risasi moja iliyofyatuliwa,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema taratibu zilikuwa zikifanyika jana ili kufungua kesi dhidi ya serikali na kujua hatima ya walio mahakamani ambao hawajapata dhamana.

Akizungumzia jitihada za kujilinda, Mnyika alisema Chadema kinashambuliwa na serikali, vyombo vya ulinzi na usalama na watu wasiojulikana.

Alisema viongozi wa chama wanakutana ili kujadili na kujua jitihada zinazofanyika kuhusu hali hiyo.

Akijibu swali la waandishi kuwa ni wapi alipo Mbowe, ambaye hajaonekana tangu wakati wa vurugu, Mnyika alijibu kuwa yuko nje ya Dar es Salaam.

“Mwenyekiti yuko nje ya Dar es Salaam, kuna majukumu mengine anashughulikia, hata Katibu Mkuu naye yuko nje ya Dar es Salaam,” alisema Mnyika.

Alipotafutwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alijibu kifupi kuwa, iwapo barua hiyo imeletwa kwake basi ataipata.

Februari 16, mwaka huu, Chadema kupitia viongozi wake waandamizi waliandamana kuelekea Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao ambao wangesimamia uchaguzi mdogo uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Maandamano hayo ndiyo yaliyosababisha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, kuuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati polisi wakiwatawanya wafuasi hao wa Chadema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles