29.7 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

WIKI YA MAJONZI

NA WAANDISHI WETU –MOROGORO/DAR ES SALAAM/KILIMANJARO

WAKATI wiki hii ikielekea ukingoni na kuacha taswira ya matukio ya simanzi na majonzi, tukio jingine la mauaji ya kutisha limemkumba Diwani wa Kata ya Namawala (Chadema), Godfrey Lwena.

Tukio la diwani huyo limetokea wakati jana mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini (22), akizikwa kijijini kwao Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, baada ya kuuawa Februari 16, mwaka huu kwa kupigwa kichwani na kitu kinachodhaniwa ni risasi inayodaiwa kufyatuliwa na askari aliyekuwa akitawanya maandamano ya wafuasi wa Chadema.

Tukio hilo la mwanafunzi limetanguliwa na jingine la kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Daniel John, aliyetoweka nyumbani kwake na mwili wake kukutwa katika Ufukwe wa Bahari ya Hindi katika eneo la Coco Beach, Dar es Salaam.

John aliuawa Februari 11, mwaka huu na mwili wake ulikutwa na majeraha ikiwamo shingo yake kunyongwa na watu ambao hadi sasa hawajajulikana.

TUKIO LA DIWANI

Tukio jipya kabisa la kuuawa kwa diwani huyo Lwena na ambalo kimsingi limethibitishwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, limeacha sintofahamu na kuzua maswali mengi.

Lwena aliyeuawa kikatili kwa kukatwa mapanga sehemu za kichwani, mikononi na mgongoni na watu wasiojulikana, wakati polisi wakilihusisha tukio hilo na kisasi cha mgogoro wa shamba kati ya wananchi na Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Chadema wao wamewanyooshea kidole baadhi ya viongozi wa Serikali na CCM mkoani Morogoro.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei, alisema mgogoro wa shamba la SBT na wananchi ambao kwa sasa kesi yake ipo Mahakama Kuu unahusishwa na tukio hilo kutokana na mazingira ya kifo cha aliyekuwa shahidi wa kesi hiyo upande wa SBT, Kenani Haule, aliyefariki dunia mwaka juzi kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana.

Matei alisema kuwa Lwena alikuwa akisikika akisema kama Kenani akifa wananchi watapata haki yao ya mashamba hayo yanayodaiwa kumilikiwa na SBT.

“Tunajaribu kuunganisha visa na kuhisi pengine kifo cha Lwena kikahusika na visasi vya mgogoro huo na kauli zake za awali,” alisema.

Akizungumzia jinsi alivyouawa, Matei, alisema tukio la kifo cha Lwena lilitokea juzi saa moja na nusu usiku akiwa nyumbani kwake wilayani Kilombero.

Matei alisema inadaiwa kuwa Lwena akiwa nyumbani kwake ghafla umeme ulikatika na alipotoka nje ya nyumba kujua sababu za umeme kukatika ndipo alipokutana na watu hao wasiojulikana na kumvamia na kumkatakata mapanga kichwani, mikononi na mgongoni na kusababisha kifo chake.

Matei alisema baada ya watu hao kutekeleza uhalifu huo walitokomea katika msitu uliokaribu na nyumba ya Lwena na polisi wanaendelea kuwasaka na aliwataka wananchi kushirikiana nao kutoa taarifa zitakazofanikisha wahalifu hao kukamatwa.

CHADEMA WATOA TAMKO

Katika hatua nyingine, Chadema kilisema tukio la mauaji ya diwani huyo si ya kulaani tu bali polisi inatakiwa kuchukuwa hatua ikiwamo kuchunguza watu waliokuwa na mgogoro na Lwena.

Pia kilitoa wito kwa polisi ijieleze kwanini ilitumia takribani saa tatu kufika eneo la tukio.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika, anayekaimu nafasi ya Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji, alisema mauaji hayo yalitokea saa moja na nusu usiku lakini polisi walifika takribani saa 4:45 usiku.

“Polisi walifika saa tano kasoro ambazo ni saa tatu baadaye, waeleze kwa Watanzania kama kuchelewa kwao hakukuwa kwa makusudi ili kutoa mwanya kwa washambuliaji kutoweka. Si mapema kuwatupia lawama lakini waeleze hatua gani walichukua katika kuchunguza,” alisema.

Mnyika alisema diwani huyo alikuwa na mgogoro na baadhi ya viongozi wa Serikali na CCM mkoani Morogoro.

“Uchunguzi ufanywe haraka kuchunguza watu waliokuwa na mgogoro naye ambao ni baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro na CCM kutokana na migogoro ya ardhi katika kutekeleza majukumu yake,” alisema.

Mnyika alisema mauaji hayo ni ya kisiasa hivyo watetezi wote wa haki za binadamu na demokrasia wanapaswa kujua kuna mauaji.

Pia alisema mauaji hayo yalikuwa tofauti na yale yaliyotokea Hananasif kwa sababu kwa Lwena walikata umeme na alipotoka nje kutaka kujua tatizo alishambuliwa.

Alisema sasa ni wakati wa wanachama, viongozi na wafuasi wa chama hicho na wengine walio katika tishio kuchukua tahadhari ya kujilinda ikiwamo waandishi wa habari.

Alisema Taifa linahitaji kukubaliana kuwa matukio hayo na mengineyo yanahitaji uchunguzi huru.

“Viongozi, wabunge na watu wanaojua wako mbele kutetea masilahi wakigongewa usiku hata wakijitambulisha ni polisi wasikubali kufungua,” alisema.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali, alizungumzia kifo cha Lwena na alisema ameuawa kikatili pia ni vigumu hata kusimulia.

Alisema walipokea mwili wa Lwena saa 10 alfajiri ya kuamkia jana na kushuhudia ukiwa na majeraha makubwa kichwani huku mikono yake ikiwa imekatwa katwa sehemu ya mabegani.

“Kimsingi watu hao ni wakatili kwa jinsi nilivyoona majeraha ya marehemu sehemu ya kichwani,” alisema Lijualikali.

Pia alisema kifo cha Lwena kimeibua simanzi na gumzo kubwa Kilombero huku wananchi wakiwa katika hali ya simanzi katika Hospitali ya St Francis ambako mwili wake umehifadhiwa.

AKWILINA AZIKWA

Mamia ya wakazi wa Kilimanjaro walijitokeza katika Kijiji cha Marangu Kitowo, Kata ya Holele wilayani Rombo kushiriki mazishi ya Akwilina.

Mazishi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwihira, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Kippi Warioba na viongozi wa dini na siasa.

Akizungumza katika ibada ya mazishi iliyofanyika Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Kata ya Olele, Padri Emanuel Ndekusare, alisema wananchi hawapaswi kulalamika kwanini kifo hicho kimetokea bali ni mapenzi ya Mungu.

“Kifo hiki kinauma na hakiwezi kuelezeka, ila tukumbuke maisha ya Akwilina hayajapotea bali muda wake wa kuishi hapa duniani umeisha na sasa anaenda kuungana na Kristo, hivyo ndugu zangu tusilalamike na kurushiana lawama,” alisema.

Alisema kupitia kifo hicho ni vema sasa wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wakajijengea utamaduni wa kudumisha upendo na kuondokana na vitendo vya chuki na ubinafsi ambavyo kwa namna moja au nyingine vimeonekana kutawala na kukosesha amani baadhi ya watu.

“Pamoja na kwamba kifo hiki ni cha kuhuzunisha, lakini kimetupa mafundisho mengi hasa katika kipindi hiki cha mfungo mtakatifu, tujifunze kupendana na kuondoa chuki na ubinafsi kwa sababu ni mambo ambayo kwa sasa yameonekana kutawala maisha yetu, tutimize matendo ya upendo na huruma kwa watu tunaoishi nao,” alisema.

FAMILIA YALAANI MAUAJI

Akisoma historia ya Akwilina, Moi Kiyeyeu, ambaye ni kaka yake alilaani mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.

Alisema familia hiyo inalaani mauaji ya Akwilina na sasa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kutosha ili kuwabaini haraka waliohusika na hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.

“Tukiungana na jamaa na marafiki wa familia hii, tunalaani vikali mauaji ya kikatili ya binti yetu, hivyo wito wetu kwa Serikali tunaomba iharakishe uchunguzi wa mauaji haya na hilo liende sambamba na kuwachukulia hatua wote waliohusika na kitendo hiki cha ukatili,” alisema.

Alisema ni wajibu wa Serikali yoyote duniani kulinda raia wake ikiwamo vijana na wanafunzi wanaosoma katika vyuo mbalimbali lakini kitendo cha mauaji ya Akwilina kinadhihirisha ulinzi dhidi ya raia haupo wa kutosha.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), Freeman Mbowe, wakati akitoa salamu za rambirambi, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema kifo cha Akwilina ni cha kikatili na hakipaswi kufumbiwa macho na matukio ya aina hiyo yanapaswa kukemewa.

“Msiba huu unatisha na unasikitisha kwa sababu kifo cha Akwilina ni cha kikatili, kumbukeni Akwilina alikuwa hataki mazishi ya kifahari bali alikuwa anahitaji elimu na kuja kuisaidia familia yake, hivyo ndugu zangu mauaji ya aina hii hayapaswi kufumbiwa macho na tunayapinga,” alisema.

NDALICHAKO KUMSOMESHA MDOGO WAKE AKWILINA

Akitoa salamu za Serikali katika mazishi hayo, Profesa Ndalichako, alisema atamsomesha Angela ambaye ni mdogo wake Akwilina na sasa ni wakati wa kudumisha umoja na mshikamano kama Taifa na kifo hicho kisiwagawe Watanzania.

“Serikali imepokea msiba huu kwa uzito sana lakini naomba kifo hiki kisitugawe bali tushikamane na kudumisha ushirikiano wetu.

“Akwilina alikuwa ni mpiganaji wa elimu, nasikitika kwamba alikuwa akitumia fedha zake za kujikimu kumsomesha mdogo wake Angela, hivyo mimi naahidi kwamba nitamsomesha mtoto huyu hadi hapo atakapoona inafaa,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa NIT, Zacharia Mganilwa, alisema Akwilina ni miongoni mwa wanafunzi waliokuwa wakifanya vizuri katika masomo yao na kifo hicho kimezima ndoto zake.

“Tumepata pigo kubwa kwa sababu nakumbuka Akwilina alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wangu na leo (jana) ilikuwa ni siku yake ya kumaliza mitihani ya muhula wake wa kwanza hivyo ndoto zake zimezimika ghafla,” alisema.

SHUGHULI ZA KIJAMII ZASIMAMA

Hali ya simanzi katika viunga vya Rombo vilitawala hali iliyosababisha baadhi ya shughuli mbalimbali za kijamii kusimama ikiwamo shule mbili za msingi kufungwa kwa muda ili kupisha shughuli za kuaga mwili wa Akwilina.

Shule za msingi zilizofungwa kwa muda ni za Olele na Mengeni. Pia simanzi na majonzi zilitawala wakati historia ya Akwilina ikisomwa katika ibada hiyo ya mazishi na kuzua vilio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles