NA MARKUS MPANGALA |
JANUARI 31, mwaka huu, Taifa la Kenya liliweka rekodi ya kipekee ambayo inakuwa ya pili katika duru ya kisiasa na kisheria nchini humo, kama si duniani.
Rekodi ya kwanza iliwekwa Septemba 14, mwaka jana, baada ya Mahakama ya Rufaa chini ya Jaji Mkuu, David Maraga, kufuta matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake, William Ruto, kutoka Chama cha Jubilee. Lilikuwa tukio la kipekee barani Afrika, ambapo kesi hiyo inatarajiwa kutumiwa na majaji mbalimbali barani humu.
Rekodi ya pili ni hii ya mwanasiasa mkongwe nchini humo na kiongozi wa Muungano wa Upinzani -Nasa, Raila Oginga Odinga, kujiapisha kuwa rais wa wananchi katika Jamhuri ya Kenya.
Tunasema ni rekodi kwakuwa hazikuwahi kufanyika popote pale barani Afrika, hivyo Kenya inakuwa Taifa la kwanza kushuhudia mwanasiasa akijiapisha kuwa rais wa nchi bila kutambuliwa na vyombo vinavyohusika.
Ikumbukwe Raila alikataa kushiriki uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26, mwaka jana, baada ya kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi kushinda, hivyo kuilazimu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC, kutangaza tarehe mpya ya uchaguzi.
Awali IEBC ilitangaza kuwa, uchaguzi huo ungefanywa Oktoba 17, lakini upinzani walikataa kushiriki, hivyo Tume ikasogeza mbele ili kutoa nafasi ya maandalizi. Hata hivyo, kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, alijitoa kushiriki uchaguzi huo na kumwacha Uhuru Kenyatta akipambana na wagombea dhaifu.
Rekodi hiyo mpya ya kushuhudia mwanasiasa akijiapisha kuwa ‘rais’ wa nchi imezua tafrani na kusababisha malumbano makali ya kisiasa, haki za binadamu na masuala ya kisheria.
Wakati Raila Odinga akijiapisha, amesababisha serikali kuchukua hatua kali dhidi ya baadhi ya vituo vya habari vilivyokuwa vinarusha matangazo ya moja kwa moja ya tukio hilo.
Serikali ilizima masafa ya luninga za Citizen TV, NTV na KTN News pamoja na kuathiri vituo kadha vya redio chini ya mwavuli wa Kampuni ya Royal Media Services. Kuzimwa kwa masafa hayo kulifanyika baada ya madai ya jopo la wahariri nchini Kenya kusema kuwa, Serikali ya Jubilee ilikuwa ikivihangaisha na kutishia vyombo vya habari, ili kuvizuia kupeperusha moja kwa moja matukio ya kuapishwa kwa kinara mkuu wa Nasa, Raila Odinga.
Kupitia kwa mwenyekiti wa jopo hilo, Linus Kaikai, vyombo vya habari vilifichua Januari 29 kuwa, Rais Uhuru Kenyatta aliwaita Ikulu na kuwatishia kuhusu hafla ya Nasa. Kulingana na Kaikai, wakuu wa vyombo vya habari waliokuwa Ikulu, walitakiwa kuhakikisha kuwa, sherehe ya Nasa hairushwi kwenye televisheni wala redio yoyote nchini humo.
Licha ya tishio hilo kutoka kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi, Japhet Koome, Nasa walishikilia msimamo wao kuwa sherehe ingefanyika kama ilivyopangwa.
Kamanda Koome alionya dhidi ya yeyote kuingia Uwanja wa Uhuru Park, lakini wafuasi wa Nasa waliingia katika uwanja huo. Serikali pia ilimuonya Raila dhidi ya kula kiapo na ilisema ikiwa atafanya hivyo, litakuwa kosa la uhaini, ambalo adhabu yake ni kifo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Januari 30, mwaka huu ya mtandao wa gazeti la The Standard, ilimkariri Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani, Fred Matiang’I, akikiita kikundi cha vuguvugu pingamizi dhidi ya serikali, NRM kinachoongozwa na Raila Odinga kuwa ‘kikundi cha wahalifu’. Waziri huyo alitumia kipengele cha 22 cha sheria ya uhalifu uliopangwa ya mwaka 2010.
Waziri huyo alikwenda mbali zaidi na kusema kufungiwa kwa vituo vya NTV, KTN, Citizen TV pamoja na redio ni hatua ya awali, kwani uchunguzi dhidi ya vyombo hivyo unaendelea na vitafunguliwa baada ya kukamilika.
Serikali ya Uhuru Kenyatta pia imechukua hatua kali dhidi ya Mbunge wa Ruaraka kwa tiketi ya chama cha ODM, Tom Kajwang’, ambaye alihusika katika kumlisha kiapo Odinga. Kajwang’ amekamatwa na maofisa wa kitengo cha Flying Squad na kufunguliwa mashtaka.
Hekaheka za kumwapisha Raila pia kuligusa utendaji mwingine wa vyombo vya habari, baada ya baadhi ya waandishi kutoka vyombo binafsi kuzuiliwa kupiga picha na kuandika habari kuhusu kurejea Rais Uhuru Kenyatta kutoka Ethiopia, alikokuwa kwenye kikao cha Umoja wa Afrika.
Miongoni mwa wanahabari hao ni wa kutoka televisheni ambazo serikali ilifunga masafa yake.
Badala yake, Televisheni ya K24 inayomilikiwa na Uhuru Kenyatta na KBC ambayo ni mali ya serikali, viliruhusiwa kupata habari na kupiga picha, ndani ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na habari wamekiri kuwa, hiyo ni dosari ambayo imetengeneza uhusiano mbaya kati ya serikali na vyombo vya habari binafsi, ambavyo vitaona kuwa vinatengwa katika shughuli za kiserikali ambazo umma unapaswa kufahamu.
Sakata la kujiapisha Raila lilitua mikononi mwa sheria katika mahakama kuu, safari hii likivihusisha vyombo vya habari dhidi ya zuio la serikali la kuzima masafa yake.
Jaji wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita, aliiagiza serikali kurejesha hewani vituo vya luninga vya Citizen, NTV na KTN, baada ya kuvifunga.
Jaji huyo alitoa amri ya kuizuia serikali kuhitilafiana na vituo hivyo hadi pale kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtata itakaposikilizwa na kuamuliwa Februari 14, mwaka huu. Omtata aliwasilisha kesi mahakamani kupinga hatua ya kuvifunga vituo hivyo, akidai serikali ilikiuka sheria za uhuru wa vyombo vya habari kwenye vipengele vya 33 na 34 vya Katiba.
Uamuzi huo ulilenga kufuta agizo la Waziri wa Usalama wa Ndani, Dk. Fred Matiang’i, aliyeamuru vituo hivyo vizimwe kwa madai ya kukiuka hali ya usalama wa taifa.
“Wamiliki wa vyombo vya habari na wengine wanaohusika walipewa maelezo kamili kabla ya shughuli za Nasa. Licha ya hayo, baadhi ya vyombo vya habari viliamua kupuuza ushauri huo. Serikali ilizima vituo vilivyohusika kwa muda usiojulikana, ikianzisha uchunguzi wa kukiukwa kwa hali ya usalama,” anasema Matiang’i kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Kwa upande wa Raila, upo mjadala mwingine kuhusiana na kiapo hicho. Katika viwanja vya Uhuru Park, jijini Nairobi, maelfu ya wafuasi wa Nasa waliduwazwa kukosekana kwa mgombea mwenza, Kalonzo Musyoka kutoka chama cha Wiper na viongozi wengine waandamizi wa muungano huo, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula.
Si hao pekee waliosusia, wapo pia wanasiasa wengine, wakiwamo marafiki wakuu wa Raila, ambao awali walijitutumua kushiriki katika hafla hiyo.
Magavana 15, wabunge 77 na mamia ya wawakilishi wa kata katika muungano wa Nasa hawakuwapo.
Ni magavana wawili tu waliohudhuria, Cornel Rasanga na Hassan Joho wa Siaya na Mombasa mtawalia. Gavana wa Kisumu, Anyang Nyong’o, ambaye ni mgonjwa aliwakilishwa na Naibu wake, Ochieng Owili.
Vigogo wengine walioingia mitini ni pamoja na mkewe Raila, Ida Odinga, Amason Kingi (Kilifi), Wycliffe Oparanya (Kakamega), Josephat Nanok (Turkana), James Ongwae (Kisii), Johnson Muthama, Boni Khalwale, Okoth Obado (Migori), na Sospeter Ojaamong (Busia).
Wengine ni Cyprian Awiti (Homa Bay), Kivutha Kibwana (Makueni), Granton Samboja (Taita Taveta), Wilber Ottichilo (Vihiga), Charity Ngilu (Kitui), John Nyagarama (Nyamira), Patrick Khaemba (Trans Nzoia) na Wycliffe Wangamati (Bungoma). Wabunge waliohudhuria walikuwa 57, licha ya wote 127 wakiwa wametia saini.
Mhadhiri wa takwimu na mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mkoani Morogoro, Richard Ngaya, anasema: “Kwanza tunaweza kuona kama kichekesho. Ni dhahiri Raila anasaka nguvu kutoka kwa wananchi ili waendelee kushinikiza masuala yanayopiganiwa na Nasa au upinzani kwa ujumla. Hata baadhi ya wandani wake kisiasa kutotokea kwenye hafla ya kuapishwa kwake naamini wamekubaliana kama sehemu ya mbinu nyingine za ziada ili kutoharibu taswira zao kisiasa, kwasababu ukizingatia wenzake bado umri unawaruhusu kugombea tena, mfano Kalonzo Musyoka anaweza kurudi kugombea mwaka 2022. Kalonzo Musyoka ana miaka 65 sasa na Musalia Mudavadi ana miaka 58. Nawaona bado wanayo nguvu ya kisiasa, hawatastaafu. Hivyo wamekwepa kuungana na Raila kwa makubaliano kama haitapokelewa vyema wasiharibu mipango yao ya baadaye.
“Jambo la pili, Odinga ameitega serikali, watamshtakije kwa uhaini wakati kwanza ameapiswa na mtu ambaye hana mamlaka ya kumwapisha mtu wa hadhi yake? Hiyo pekee inafanya kiapo chake kuwa feki. Na hivyo akipelekwa mahakamani anashinda kesi alfajiri. Faida ya hilo atakuwa amepata jukwaa la kuielezea dunia yaliyotokea na ndicho wanachotafuta hadi sasa.
“Siasa za Afrika ni kituko, ukimsifia kiongozi mwezi huu, mwezi ujao anakuumbua kuwa ulikosea kumsifia. Tuna safari ndefu mno, tuko tayari kulinda uongozi na makundi yetu kwa gharama yoyote ile, ikiwamo kuchagua nchi kuendelea kuwa masikini.
“Jambo la tatu ni kwamba, nashindwa kuelewa malengo ya Rais Uhuru Kenyatta kuruhusu kufanyika zoezi la kuapishwa Raila. Kwa hali ilivyo, nadhani alikuwa anaionyesha dunia kuwa watu wa Kenya wanatekeleza demokrasia kwa vitendo kwa mujibu wa mitazamo na njia zao bila kusumbuliwa na dola la kigeni. Na zaidi huenda alichukulia mpango huo kama maandamano ya kawaida tu. Na hivyo kuacha watu wafanye maandamano ambayo ni haki kwa mujibu wa Katiba ya Kenya.”
Naye mhariri na mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (Deutche Welle), Mohammed Ghassani, anasema: “Alichokifanya Raila ndicho kinachopaswa kufanywa popote kura zinapoibiwa barani Afrika. Kote ambako wapigakura hawaheshimiwi na wanapuuzwa na wahesabuo kura. Demokrasia duniani haikupatikana kwa kuwaridhia watawala. Bali kwa kuwashurutisha”.