30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

RAIS TRUMP NI MWOGA ANAYEHOFIA JINSIA NA RANGI?

WENGI huchanganya baina ya jinsi na jinsia na kuibua mkanganyiko wa lipi wanalofikiria kama Rais Donald Trump wa Marekani anavyojikanganya, hususani anapokumbana na upinzani wa ‘jinsi’ ingawa ameshawahi kujigubika katika mtanziko tata kuhusiana na mustakabali huo.

 

Licha ya kufahamika kuwa mhafidhina wa imani yake lakini katika kuonekana anatetea haki amewahi kuonesha kuunga mkono Jumuiya ya LGBT inayojumuisha wanawake wenye mapenzi ya jinsia moja, mashoga, wenye ‘jinsi’ zaidi ya moja na waliobadili jinsia. Mkanganyiko wa kijinsia umemgubika tena hivi karibuni Rais Trump kutokana na hotuba ya kupokea tuzo iliyotolewa na mwanamama Oprah Winfrey, anayeshabikiwa  dunia nzima kutokana na vipindi vyake kiasi kwamba Rais Trump ameshindwa kujizuia na kujibu kilichohisiwa kuwa ni dhamira ya Oprah kugombea urais. Ingawa mwenyewe hakulisema hilo lakini kwa Trump ni kama jinamizi jipya kupambana na mwanamke  mwingine kama alivyopambana na Hillary Clinton aliyekuwa chini ya kivuli cha ‘Mweusi’ Obama kwa hiyo kwake ilikuwa jinamizi lenye sura mbili moja ya kijinsia nyingine ya rangi!

 

Katika tuzo hizo za Golden Globes 2018 baada  ya alichokizungumza Oprah wakati akipokea tuzo yake  wafuasi na mashabiki wake  wakaanza kumpigia upatu kugombea urais, kutokana na Oprah kuzungumzia unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji wa haki hususani kwa wanawake pia ubaguzi wa rangi ambapo aliwataja washindi weusi waliopita wa tuzo mbalimbali, wakiwamo Sidney Poitier naye akifuata nyayo zao akishukuru wote waliomuunga mkono katika changamoto mbalimbali alizopitia, kikiwamo chama cha wanahabari wa kimataifa cha Hollywood  ingawa  kwa sasa tasnia ya habari inashutumiwa kimakosa kwa mujibu  wa Oprah akimuelekezea kombora Trump ambaye alianza utawala wake kwa kusigana  na vyombo vya habari.

 

Akaenda  mbali zaidi kwa kusema kwamba vyombo vya habari vinashutumiwa kwa kuanika  ukweli pia aligusia tuhuma zinazowakabili vigogo wa Hollywood  juu ya unyanyasaji wa kijinsia na kukiuka maadili ya dunia, kijamii, imani, siasa na hata sehemu za ajira. Inawezekana ni kwa hulka yake ya kupigania haki za binadamu kwamba Oprah hutumia jukwaa lolote la fursa kupaza sauti, lakini hotuba yake ikageuzwa kisiasa hususani alipotoa mifano hai ya waathirika wa kadhia za kunyanyaswa  kijinsia walizovumilia kwa miaka mingi. Aligusa hisia za wengi alipomtaja Recy Taylor mwanamke aliyetekwa na kubakwa na wanaume sita katika Jimbo la Alabama mwaka 1944 na kwa miaka yote iliyofuatia mfumo wa utawala wa sheria wa Taifa hilo umeshindwa kuwakamata wahusika, hadi wakati umauti  unamkuta  Recy akiwa na umri wa miaka 98 siku chache zilizopita.

 

Kinachochagiza hisia za kugombea urais kwenye mrengo wa kisiasa kutokana na hotuba ya Oprah  ni jinsi alivyomalizia hotuba yake akisema: “Kwa hiyo mabinti wote mnaonitazama nataka kuwaambia kwamba mwanzo mpya umekaribia na mara utakapowadia, utatimia kutokana na juhudi za wanawake wengi waliojitolea wengine wakiwa hapa na wanaume waelewa ambao kwa pamoja tumepambana kuhakikisha  tunapata viongozi watakaotupeleka kwenye mustakabali unaotakiwa,” Trump alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na Oprah endapo atagombea urais, alijigamba kwamba anamfahamu vyema mwanamama huyo na atamshinda kirahisi ingawa kwa  uhakika Oprah hajaamua kujitosa kwenye ulingo huo licha ya kujihusisha kwa karibu na chama cha Democrat hususani  kwenye harambee nyingi za chama hicho,  akifanikisha upatikanaji wa fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia ustawi wa watu dhalili ingawa sifa hizo zinapondwa  na wapambe wa Trump kwenye chama chake kwamba hazimpi uzoefu wowote, licha ya kwamba Bosi wao mwenyewe wakati anajitosa kugombea hakuwa na uzoefu wowote hata wa kuongoza mtaa sembuse kuwa Rais wa Taifa kubwa la Marekani. Ingawaje pia wapambe hao wanakiri ushawishi wa Oprah miongoni mwa Wamarekani pengine hicho ndicho kinachowatikisa wakifikiria uwezekano wa mwanamama huyo kuamua kugombea.

 

Trump anaweweseka kwa dhana kwamba ikiwa Oprah ataamua kugombea na kufanikiwa katika dhamira hiyo, kwa kuwa mchakato wa kusimikwa  ugombea kwa taratibu za Marekani ni mrefu basi mafuta yake mwenyewe yatamkaanga, kwa kuwa amekuwa na hulka ya kutoa kauli zinazombinya mwenyewe kama alivyofanya hivi karibuni kwa kutamka kuwa nchi yake imelundikana watu wachafu wasiostahili, wengi wao wakitoka Afrika ambao hawahitajiki nchini humo. Kwa maana hiyo ikiwa atakumbana na Oprah atakuwa anapambana na jinamizi lenye sura tatu moja ikiwa ya jinsia, ikifuatiwa na rangi ya Oprah na ya tatu  umaarufu wake ambao unaweza kuifanya nafasi yake kuwa katika mtihani.

 

Haikutarajiwa tuzo zilizoasisiwa na chama cha waandishi wa kimataifa wa Hollywood zinazowatuza waliofanya vyema kwenye filamu na luninga ambazo zimeasisiwa mwaka 1944 zizue hamkani ya uchaguzi ujao wa Marekani. Mengi yako nyuma ya pazia kwenye siasa za Taifa hilo kubwa hususani kutokana na hulka ya Rais wa awamu ya sasa ambaye alipojinadi kwamba akiingia madarakani atakachozingatia ni kipaumbele cha Taifa lake, lakini anawakwaza wengi kwa mwenendo wake kisiasa pengine ndiyo maana Wamarekani wameanza kutamani kumpata mbadala anayetofautiana naye hata ikibidi kuwa Oprah Winfrey.

 

Mwisho….

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles