24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

HONGERA PAPA FRANCIS, KUTETEA ULINZI WA MAZINGIRA

RAIS wa Awamu ya 32 wa Marekani, Franklin D. Roosevelt aliwahi kusema:‘‘Taifa linaloharibu ardhi yake, hujiharibu lenyewe. Misitu ni mapafu ya ardhi yetu na usafi wa mazingira huleta afya katika miili ya watu wetu,’’

Akiwa katika ziara yake katika mataifa ya Bara la Amerika ya Kusini, Mkuu wa Kanisa  Katoliki Duniani Baba Mtakatifu Papa Francis ameonesha kuhuzunishwa  na vitendo vinavyoashiria kuutokomeza msitu maarufu wa Amazon, ambao kimsingi ni kitovu cha ulinzi wa mazingira, si tu katika ukanda wa Amerika bali dunia nzima kwa ujumla.

Kuhuzunika  kwa kiongozi huyu kumetokea Ijumaa ya Januarim 19, mwaka huu baada ya kuwasili nchini Peru ambako aliwahimiza wananchi kuachana na vitendo vitakavyoangamiza msitu huo mfano uvunaji ovyo wa mbao, kuchimba gesi asilia na madini ya dhahabu.

Aidha Papa Francis ameendelea kushangazwa sana  na  wakazi wanaozunguka maeneo ya msitu wa Amazon kudumisha utamaduni wa ujenzi wa barabara mpya ndani ya msitu, ujenzi wa mabwawa, shughuli za kilimo,  kutupia takataka, vitendo ambavyo vimesababisha kutoweka kwa rangi asili ya kijani katika msitu huo mkubwa.

Kiongozi huyu kuumizwa na tishio la kutoweka  msitu wa Amazon,inatokana na ufahamu wake mkubwa katika masuala yahusuyo mazingira kwani anatambua kuwa misitu ni kichocheo cha kupunguza majanga ya asili kama vile ukame, mafuriko na vimbunga.

Si tu kuzuia majanga bali pia Papa anaelewa fika ya kwamba misitu husaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa hewa chafu ambazo husababisha kuleta magonjwa  mfano kansa  inayopoteza maisha ya maelfu ya watu duniani.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), Septemba 27, 2016 ilieleza kuwa watu tisa kati ya kumi huvuta hewa chafu duniani kote kila siku.  Hivyo shirika hilo lilizitaka Serikali zote duniani kuchukua hatua kwa kuweka  mikakati ya kupambana na uchafuzi wa hewa kwani  pamekuwapo  na ongezeko la magonjwa mbalimbali yanayosababisha zaidi ya watu milioni 6 kupoteza maisha kila mwaka duniani kote.

Pia kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa (UN) katika mwaka uliopita  inasemekana watoto wawili kwa kila watoto 10,000 wenye  umri chini ya  miaka mitano hufariki dunia kila siku duniani kote  kutokana na njaa inayosababishwa na ukame wa muda mrefu.

Kama  Baba Mtakatifu, Papa Francis ameliona hili la uharibifu wa msitu na kuamua kutolifumbia macho kwa kutoa kauli nzito, Je, viongozi wetu wa dini katika Taifa letu wana mchango gani kuhusiana na ulinzi wa mazingira?

Je, kazi ya  mashehe, wachungaji na mapadri ni kutumia mahekalu kutoa mahubiri/mawaidha kwa waumini wao kuacha dhambi ili waionje mbingu/pepo, au wanayo nafasi nyingine ya kuwajenga wafuasi wao kupenda kutunza mazingira?

Je, viongozi wa  dini ufahamu wao umejengeka kuwa waumini  wakitoa sadaka ndio njia mbadala ya kuleta baraka na kusahau kuwa umaskini mwingine ni matokeo  ya uharibifu wa mazingira?

Je, ni viongozi wangapi wa dini hutumia Sikukuu za  Eid na Krismasi kuwaonya waumini wao wasiharibu   mazingira kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakifanya kwa kutoa matamko mbalimbali dhidi ya utendaji wa viongozi wa  Serikali?

Naamini kabisa kutokana na ushawishi walionao viongozi wetu wa  dini, wakiamua kuhamasisha waumini wao kuogopa kuharibu mazingira, hatutashuhudia tena uvuvi haramu, ukataji miti ovyo, wala utupaji takataka katika maeneo yetu yanayotuzunguka

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles