24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

MWAKA MMOJA WA RAIS TRUMP MADARAKANI

JANUARI hii, Rais Donald J. Trump, anatimiza mwaka mmoja wa uongozi wake.  Rais huyo wa 45 wa Marekani aliapishwa Januari na hivyo anakaribia kumaliza mwaka mmoja kwenye ofisi yake hiyo mpya.

 

Hata hivyo, hatuna budi kukiri kwamba wengi huenda wasiamini kwamba Trump bado hajamaliza hata mwaka akiwa Rais. Hiyo ni kutokana na dunia kushuhudia kiongozi huyo akiwa katika migogoro na watu tofauti tofauti katika kipindi hiki kifupi tangu alipoapishwa kuwa Rais.  Kutokana na hilo, vyombo vya habari duniani kote vimekuwa na habari mpya kuhusu Trump kila siku.

 

Kwa wanaofuatilia habari za kimataifa, watakumbuka kwamba habari kuhusu Trump zilianza tangu enzi za kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Marekani, kuanzia pale alipokuwa akigombea ndani ya chama chake cha Republican ili apitishwe kuwa mgombea wa kiti cha urais.  Wengi hatukuamini kwamba angeweza kuvuka, lakini alishinda.

 

Aliendelea kuandikwa zaidi baada ya kupitishwa na chama chake kuwa mgombea wa urais, mpinzani wake mkuu akiwa Hilary Clinton wa chama cha Democrats.  Nadhani ule ulikuwa ni wakati ambao watu wengi walitamani uchaguzi ufike na kuondoka, kwani walichoshwa na habari zilizokuwa zikiandikwa kila siku kuhusu wagombea wa urais, hasa kuhusu Trump alichowahi na kauli zake nyingi zenye utata.

 

Uchaguzi ulifika na kwa mshangao wa wengi, Trump alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani.  Hata hivyo, bado habari za kumuhusu yeye hazikuisha na badala yake zimekuwa zikiendelea kila siku, huku kukiwa na kutokuelewana kwa dhahiri kati ya Rais huyo na baadhi ya vyombo vya habari, kama vile CNN, ambavyo yeye huviita “fake news”.

 

Yote hayo yalitokana na mambo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiendelea tangu Trump alipoingia madarakani, kama vile tuhuma kwamba Urusi ndio waliomsaidia kushinda kiti cha Urais, tuhuma ambazo Warusi wenyewe wamezikanusha.  Tuhuma hizo ndizo zilizosababisha hata aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), James Comey, kufukuzwa kazi na Rais Trump.

 

Kwa sasa huenda jambo kubwa zaidi linaloendelea kwa upande wa Marekani ni wasiwasi wa kutokea kwa vita kati ya Marekani na Korea Kaskazini.  Wasiwasi huo umetokana na pande zote mbili kutishiana na kuonyeshana ubabe, huku dunia ikiwa inaangalia na kuwaza endapo kutakuwa na Vita Baridi nyingine, au kama kutakuwa na Vita Kuu ya Tatu ya Dunia.

 

Lakini huenda lililofunga mwaka kuliko yote, ni mapenzi makubwa ya Rais Trump kwa aina mmoja wa mtandao wa jamii – Twitter.

 

Ni kweli kwamba kabla hajawa Rais, Trump alikuwa akitumia Twitter kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa aina yoyote, lakini hasa kuwasema wale aliodhani wamemkoa kwa namna fulani.  Ni matumizi hayo ya mtandao wa jamii ambao ulifanya wengi waamini kwamba Trump hastahili kuwa Rais.  Alipochaguliwa, tulidhani ataacha.  Hakuacha.

 

Huenda Rais Donald Trump ndiye mtumiaji maarufu zaidi wa mtandao wa kijamii wa Twitter.  Licha ya kuwa Rais wa nchi yenye nguvu kuliko nchi zote duniani, kamwe hajawahi kuachana na mtandao wa Twitter.  Imefikia hatua, anatoa hata matamshi mazito kupitia mtandao huo, hasa kuwasema wale asioelewana nao kikazi na kisiasa.

 

Matumizi ya Trump ya mtandao wa Twitter yamezungumzwa kila kona, kwani yameonekana kwamba yanaweza kusababisha kufarakana kwa Marekani na nchi nyingine washirika, kutokana na yeye kutokujali anayatumiaje.

 

Mfano mzuri ni wa takribani mwezi mmoja uliopita ambapo Rais Trump aliamua kusambaza video ikipingana na imani ya Kiislamu.  Hata aliposhutumiwa kuhusu hatua yake hiyo, aliwashangaa waliokuwa wakimshangaa.  Hata Waziri Mkuu wa Uingereza, Teresa May alipopingana na kitendo hicho cha Trump, Trump alimjibu kupitia Twitter kwamba ayatazame yale yanayoendelea nchini mwake (Uingereza), kwani Marekani hawana mashambulizi ya kigaidi.

 

Bado Trump anaendelea kuandama watu kupitia Twitter na bado vyombo vya habari visivyokubaliana naye vinaendelea kumshambulia pia.  Hilo limesababisha wengi wadhani kwamba Trump amekwishakukaa madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu, lakini ukweli ni kwamba, ndio kwanza anatimiza mwaka mmoja Januari 20.

 

Hatapunguza wala kuacha matumizi ya Twitter, hivyo ni dhahiri kwamba dunia inatakiwa kujiandaa kwa mashambulizi zaidi ya maneno kutoka kwa Rais huyo.  Ambacho dunia bado haijajua ni endapo 2018 itakuwa ni mwaka wa vita kwa Trump, ama kama yeye na Korea Kaskazini wataendelea kuwaweka watu roho mkononi bila ya chochote kutokea.

 

Mwisho….

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles