Na SUZAN UHINGA
-TANGA
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amewataka wanachi wilayani humo kulima kwa wingi mihogo kutokana na zao hilo kustahimili ukame lakini pia lina soko la uhakika.
Amesema ofisi yake imefanya mazungumzo na mtaalamu ambaye watamtumia kwa ushauri lakini pia tayari Balozi wa China ameridhia mihogo ya Tanzania kuuzwa nchini China.
Gondwe ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea wilayani humo kujionea namna wakulima walivyohamasika kulima mihogo.
Amesema amewahamasisha wananchi na walimu wakuu katika shule zote wilayani humo kulima zao hilo linalostahimili ukame, kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo wakulima wengi hutegemea mvua.
“Nahamasisha kulima muhogo pamoja na viazi lishe ili tuweze kujiepusha na baa la njaa hasa kwa nyakati ukame kwani Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa wilaya zilizokumbwa na ukame mwaka juzi jambo ambalo lililotulazimu kubuni mazao mbadala yanayostahimili ukame kwa kuwahamasisha wananchi kupanda mihogo kama zao mbadala kwa mahindi na kwamba pale inapotokea mvua zimekosekana waweze kuwa na chakula,” amesema Gondwe.
Pia Mkuu wa Wilaya amewatoa hofu wananchi kwamba tari utaratibu wa inapatikana mbegu nzuri zitakazowafanya walime mihogo watakayouza kwenye soko la kimataifa.