33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

PIERRE GEORGES LE CHANTRE ATAONGEZA FURAHA AU HUZUNI MSIMBAZI ?

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM


HAKUNA asiyejua tabia zilizopo katika klabu za  Sunderland  na Everton, ambazo suala la kubadilisha makocha katikati ya msimu wa ligi ni jambo la kawaida.

Sunderland iliyoshuka daraja kwenye Ligi Kuu England (EPL) katika msimu wa 2015-16 kwa hivi sasa  inanolewa na kocha Chris Coleman, imeonekana kuendelea kufanya vibaya, huku sababu kubwa ikiwa ni tabia ya kutimua timua makocha.

Katika miaka mitano iliyopita imewafuta kazi  makocha wanne na kati yao  ni Gus Poyet pekee, ndiye aliyefanikiwa kufanya kazi kwa miaka miwili mfululizo.

Kwa upande wa Evarton, wao hivi karibuni  wamejikuta kwenye wakati mgumu EPL kutokana na utamaduni huo wa kulifumua mara kwa mara benchi lao la ufundi.

Kwa kipindi cha miaka miwili pekee, tayari timu hiyo imebadilisha makocha mara tatu, wakianza na David Unsworth aliyefanya kazi mara vipindi viwili tofauti kisha akaja, Ronald Koeman na huyu wa sasa Sam Allardyce ‘Big Sam’.

Tabia ya timu hizo imeonekana kuzikumba pia klabu kongwe za Tanzania hususani za Simba na Yanga, lakini kwa kipindi cha misimu minne mfululizo Simba imeshafundishwa na makocha nane tofauti.

Ukianzia msimu wa 2011/12 Simba ilipochukua ubingwa ikiwa chini ya kocha Milovan Cirkovic raia wa Serbia, kunamakocha tofauti waliopata nafasi ya kuinoa timu hiyo, licha ya kushindwa kutimiza lengo la Wekundu wa Msimbazi kuchukua taji la Ligi Kuu pamoja na kushiriki mashindano ya kimataifa.

Mara baada ya kuondoka kwa Cirkovic, uongozi wa Simba ukaikabidhi timu kwa Mfaransa Patrick Liewig, aliyeanza kazi Desemba 2012-Mei 2013 Simba ilikuwa chini yake, kabla ya kuja Abdallah ‘King’ Kibadeni aliyeanza kazi June 2013 hadi Novemba mwaka huu, kisha kikosi kuja kukabidhiwa kwa Zdravko Logarusic raia wa Croatia aliyeanza kazi Desemba 2013 hadi June 2014.

Kipute cha kubadili makocha kiliendelea baada ya Simba kumleta Patrick Phiri  aliyeanza kazi Agosti 2014 hadi Novemba 2014, alipotimuliwa kisha kumleta Mserbia, Goran Kopunovic aliyefanya kazi kuanzia Disemba 2014 na June 2015.

Wakati Dylan Kerr akija kuchukua mikoba ya Goran kuanzia Julai 2015 hadi 2016 Januari, kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Jackson Mayanga, aliyedumu kwenye ukuu wa benchi la ufundi kwa miezi mitano tu na Julai Mosi, Joseph Omog akavaa gwanda hilo rasmi kabla ya Disemba mwaka jana kuvunjwa kwa mkataba wake.

Licha ya kubadilisha huko makocha mara kwa mara, Simba wamejikuta wakitoka patupu kwani Azam FC imeweza kuchukua taji mara moja, huku watani zao Yanga wakilinyakua taji hilo kwa mara tatu mfululizo na hivyo kuonekana kinachofanywa na Simba hakuna faida kwao.

Ijumaa iliyopita Wekundu hao wa Msimbazi walimtambulisha tena kocha wao mpya Pierre Georges Le Chantre kuwa ndiye mkuu wa benchi lao la ufundi, akichukua nafasi ya Omog huku Masoud Djuma akiendelea na majukumu yake ya usaidizi.

Kocha  Le Chantre anayetimiza miaka 68 Februari 2 mwaka huu,alitua nchini juzi kumalizana na uongozi wa juu wa Simba, huku akitarajiwa kuanza majukumu yake rasmi kesho, mara baada ya timu kurejea jijini Dar es Salaam ikitokea mkoni Kagera kukipiga na Kagera Sugar.

Kuletwa kwa kocha huyo huku ikimrejesha Djuma katika nafasi yake ya ukocha msaidizi, kumeonekana kuwastua wadau wengi wa soka huku wakiingia mashaka iwapo kama kweli ujio wa kocha mpya huyo kunaweza kuipa klabu mafanikio wanayotaka.

Mchambuzi wa masuala ya soka na kocha wa zamani, Joseph Kanakamfumo anasema kuwa kitendo kinachofanywa na Simba hivi sasa ni sawa na kucheza kamari, waliyokuwa wakiifanya kila msimu lakini mafanikio hakuna.

“Ndani ya msimu mmoja Simba imebadili makocha mara tatu, sasa hili si jambo zuri kwa timu inayohitaji mafanikio tena ikikabiliwa na mashindano mkubwa ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho, lazima waelewe wanawachanganya wachezaji kwani kila kocha anakuja na mfumo wake.

“Tayari tumeona hivi sasa kikosi cha Simba kikiwa  bora tena kikiwa na morari kubwa uwanjani, tangu alipokabidhiwa Djuma sasa ujio wa huyo kocha Mfaransa sio mbaya, lakini itachukua muda mrefu wachezaji kumuelewa na kufanya kile anachotaka, hivyo kwa ratiba hii ya kubadili makocha kila wakati wasitegemee mafanikio kwa mwaka huu hivyo wasubiri tu mwakani ndio watapata kile wanachokitaka,”anasema Kanakamfumo.

Upande wake mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Ally Mayay, anasema kwa hivi sasa Simba hawakuwa na sababu ya kubadili kocha kwani tayari Djuma ameshaonekana anaweza kuifikisha timu hiyo sehemu wanayotaka.

“Simba walitakiwa kuwa na uvumilivu katika suala la kumleta kocha mpya, kwani Djuma ameonyesha anaweza kubadili timu na hili limejionyesha kwa muda mfupi aliyokabidhiwa, kikosi kimeweza kubadilika sana uwanjani kwa kucheza soka safi lenye mvuto machoni mwa watazamaji ambalo pia linawapa matokeo chanya.

“Lakini kwa kuwa wameamua kumleta mwingine huku Masoud akirejea kwenye nafasi ya ukocha msaidizi, basi wacha tuone ila wategemee mabadiliko makubwa kimfumo na uenda hata wakayumba kidogo kabla ya kukaa sawa.

Mayay anasema kulingana na mfumo wa soka la Tanzania ujio wa kocha Mfaransa, hauwezi kuleta matokeo makubwa ya haraka Simba  .

“Timu zetu hizi kubwa zimekuja na kasumba ya kuleta makocha au wachezaji pasipo kuangalia mahitaji halisi ya timu, kwani kwa hivi sasa Simba haikuhitaji kocha mpya kwani aliyekuwapo alitosha kuvaa viatu hivyo, lakini alitaka msaidizi pekee”,anasema Mayay.

Wakati huo huo, aliyewai kuwa mwenyekiti wa Simba, Aden Range anasema maamuzi ya kuvunja mkataba na Omog yalikuwa ni haraka mno, hakustaili kuondolewa bali alipaswa amalize ligi.

“Nilishitushwa niliposikia Omog amefukuzwa kisa timu imeondolewa katika michuano ya  Azam Federation Cup, wakati yeye ndiye aliyeisaidia pia kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho mwaka huu, alipaswa amalize ligi kwanza.

” Lakini pia timu alipokabidhiwa Djuma imeonekana kufanya vizuri kwani kuna mambo mengi ya kiufundi yamebadilika na kukifanya kikosi kuonekana cha ushindi, ili ni jambo la kupogezwa lakini hata msimu haujaisha nasikia ameletwa Mfaransa haya wacha tuone anajambo gani jipya ila ila ukweli tusitarajie mafanikio ya haraka kutoka kwake,”anasema Rage.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles