33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KUJIJENGEA USHAWISHI, KUKOMOANA KWALIVURUGA ENEO LA BAHARI NYEKUNDU

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA YA HABARI


HARAKATI za kila taifa hasa miongoni mwa yale yenye nguvu kutaka kupanua ushawishi wake, kutunishiana misuli au kutaka kukomoana kumesababisha hali tete katika Ukanda wa Bahari Nyekundu.

Ni hali ambayo imekuwapo kwa muda mrefu ikianzia kuhusisha mataifa machache jirani kutokana na sababu za kihistoria, lakini sasa idadi ya imeongezeka hadi mataifa ya mbali na eneo hilo.

Mwelekeo huo ulijionesha wazi wakati wa ziara ya Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan nchini Sudan mwezi uliopita.

Ziara hiyo iliyotajwa na vyombo vya habari vya mataifa hayo kuwa ya kihistoria kwa vile ilikuwa mara ya kwanza kwa mkuu wa nchi wa Uturuki kuitembelea tangu mwaka 1956 wakati Sudan ilipopata uhuru wake.

Maofisa wa Sudan wamesema mataifa hayo yamekubaliana kuanzisha jopo la mikakati la kujadili masuala ya kimataifa na kwamba wamelenga kuhusisha mkataba wa kijeshi.

Miongoni mwa zaidi ya dazeni ya makubaliano yaliyosainiwa baina ya Erdogan na Rais wa Sudan, Omar al-Bashir mjini Khartoum yalihusu kukikabidhi kwa muda kisiwa kilichopo Bahari Nyekundu cha Suakin kwa Uturuki.

Mataifa hayo yalisema Uturuki itajenga upya kilichokuwa Kisiwa maarufu chenye wingi wa watu enzi zile za dola la Ottoman ili kuongeza utalii na kutengeneza njia ya mahujaji kuvuka Bahari Nyekundu kwenda kuhiji katika jiji takatifu la Kiislamu la Mecca.

Lakini vyombo vya habari vya Misri na Saudia, ambazo hazifurahishwi na misimamo ya karibuni ya Uturuki hasa kuhusu migogoro ya Mashariki ya Kati huku pia Misri ikiwa na uhusiano mbaya na Sudan viliyakosoa vikali makubaliano hayo.

Mataifa hayo washirika wakubwa katika ulimwengu wa Kiarabu yaliituhumu Uturuki kuwa imepanga kujenga kambi ya kijeshi katika kisiwa hicho.

Awali mataifa yote hayo matatu yalikuwa marafiki wakubwa, kabla ya kudhoofu hasa wakati Ankara ilipolaani vikali mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013 nchini Misri.

Mapinduzi hayo yalimwondoa Rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohamed Morsi wa vuguvugu la Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood).

Aidha Saudia haipendezwi na Uturuki kujenga uhusiano na hasimu wake mkubwa katika kusaka ushawishi Mashariki ya Kati, Iran, imetofautiana nalo katika suala la kuitenga Qatar mwaka jana.

Mataifa kadhaa ya Kiarabu yakiongozwa na Saudia na Misri yalivunja uhusiano na Qatar kwa madai ya kusaidia magaidi, kushirikiana na Iran pamoja na kuingilia mambo ya ndani ya mataifa hayo, hatua ambayo Uturuki iliilaani.

Tukirudi katika suala la kisiwa cha kisiwa hicho, Gazeti la Saudia, al-Okaz lilikuja na stori yenye kichwa cha habari kisomekacho: “Khartoum yakabidhi Suakin kwa Ankara … Sudan mikononi mwa Uturuki.”

“Ulafi wa Uturuki katika Bara Afrika umeonekana kuvuka mipaka,” ripoti ya gazeti hilo ilisomeka ikirejea hatua ya hivi karibuni ya Uturuki kuanzisha kambi kubwa kabisa ya kijeshi ng’ambo nchini Somalia.

Ubalozi wa Sudan nchini Saudi Arabia ulijibu hayo kwa kusema “Suakin inamilikiwa na Sudan, si taifa linguine lolote’ na kuahidi kuwa makubaliano na Ankara hayatahatarisha usalama wa mataifa ya Kiarabu.

Hata hivyo, mzozo huo mara moja ukashika kasi na kuvuma kote barani Afrka.

Akitetea mradi huo, Serdar Cam, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uratibu na Ushirikiaano la Uturuki (TIKA), alisema Uturuki imekuwa ikianzisha miradi ili kusaidia miundo mbinu ya msingi katika mataifa ya Afrika yanayoihitaji katika kila sekta.

“Lengo la juhudi hizi zetu ni kuthibitisha kuwa mataifa ya Afrika yanaweza kujitosa katika michakato ya miradi endelevu na ya kimaendeleo bila kujali ukubwa wa fedha tunazotumia kusaidia,” Cam alisema

“Hivyo, Uturuki pia imelenga kuionesha dunia nzima kuwa hakuna taifa ambalo limeumbwa kwa ajili ya kuwa masikini milele na tunalenga kuisaidia Afrika kufuta dhana ya kuwa bara la giza

Katika kile kinachoweza kuwa mwitikio unaotokana na wasiwasi kuwa Uturuki inapanua ushawishi wake eneo hilo, Misri ilituma mamia ya askari wake katika kambi ya Muungano wa Mataifa ya Kiarabu (UAE) nchini Eritrea, mpakani na Sudan.

Khartoum iliitikia hatua hiyo kwa kumuita balozi wake mjini Cairo, saa chache baada ya Mkuu wa Kamati ya Kiufundi ya Mipaka ya Sudan, Abdullah al-Sadiq, kuituhumu Misri kujaribu kuiingiza Sudan katika makabiliano ya kijeshi.

Siku chache baadaye Sudan ikafunga mpaka wake na Eritrea na kupeleka maelfu ya askari eneo hilo.

Ikumbukwe mataifa haya yana mgogoro wa miaka kadhaa baada ya Cairo kudai kwamba Khartoum imekuwa ikiwaunga mkono wanachama wa Udugu wa Kiislamu na Khartoum nayo kuituhumu Cairo kuwasaidia waasi wa Sudan.

Mbali ya hilo Mradi wa Bwawa Kubwa la la Umeme la Ethiopia (GERD) ambao ni kubwa kuliko wote wa kuzalisha umneme barani Afrkika uko katikai ya mgogoro eneo hilo.

Ikiwa haifurahishwi na Khartoum, Misri mwanzoni mwa mwezi huu iliripotiwa kuishawishi Ethiopia iiondoe Sudan kutoka majadiliano kuhusu hali ya baadaye ya bwawa hilo.

Misri yenyewe imekuwa katika mgogoro na jirani yake Ethiopia kwa muda mrefu ikipinga mradi huo mkubwa wenye thamani ya dola bilioni 4.8, ikihofia utaathiri yataathiri upatikanaji wa maji katika taifa hilo lisilo na chanzo kingine kikuu cha maji zaidi ya hayo ya Mto Nile.

Misri iliwasilisha ombi kutoka Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi kwenda kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, ikitaka ifanye mazungumzo na Ethiopia pekee, kwa mujibu wa gazeti la Addis Fortune. Hata hivyo, Misri ilikana madai hayo.

Jumatatu wiki iliyopita, Hailemariam akampokea Mkuu wa Jeshi wa Sudan, Emad al-Din M Adawi na kujadili namna ya kuboresha uhusiano wa kimkakati.

Adawi alisema majirani hao wawili wataendelea na juhudi zao za kutatua matatizo yanayokabili eneo hilo.

Aidha kuna mzozo mwingine baina ya Eritrea na Ethiopia, ambayo awali yalikuwa taifa moja kabla ya Eritrea kushinda vita ya kujitenga mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Kumiminwa kwa askari wa Misri nchini Eritrea kumeikasirsha vikali Ethiopia. Ikifahamu fika uwapo wa uhusiano duni baina ya Misri na Ethiopia kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile, Serikali ya Eritrea ikapokea kwa mikono miwili ujio wa askari wa Misri.

Ethiopia, ambayo ina jeshi la tatu kwa ukubwa barani Afrika ikaitikia kwa kutuma askari zaidi katika mpaka wake na hasimu wake huyo Eritrea.

Asmara na Addis Ababa zilikuwa na vita kali ya umwagaji damu kuhusu mgogoro wa mpaka baada ya mataifa hayo kutengana.

Ethiopia pia haipendezwi na UAE ambayo ina ushirika mwema na Cairo, kwa kupanua ushawishi wake katika eneo hilo.

Hivi karibuni UAE ilizindua kambi za kijeshi na majini katika nchi zinazopakana na Ethiopia, Somalia kwa upande wa mashariki na Eritrea kwa upande wa kaskazini pamoja na Yemen. Ikumbukwe pia Somalia ni hasimu mkubwa wa jadi wa Ethiopia.

Hilo liliifanya Ethiopia kumalizia hasira zake kwa kupuuza majadiliano na kelele zote kuhusu ujenzi wake wa bwawa la umeme ikisema asilimia 60 ya mradi huo umekamilika.

“Ujenzi hautasimama na kamwe hautosimama hadi ukamilike. Hatujali kile Misri inachofikiria. Ethiopia imedhamiria kunufaika na maliasili yake ya maji bila kusababisha hatari kwa yeyote,” Waziri wa Umwagiliaji, Maji na Umeme wa Ethiopia Seleshi Bekele alisema Novemba mwaka jana.

Wakati Misri, Uturuki na UAE zikifanya juhudi za kupanua ushawishi wao na kujipatia washirika eneo hili, ni wazi bila uangalifu wa kidiplomasia na iwapo malengo yamejikita katika kukomoana na kuoneshana ubaba, baina ya mataifa ya Afrika yataendelea kuwa chungu.

 

Hilo huenda likamulikwa wakati wa mkutano wa wakuu wa mataifa ya Afrika mjini Addis Ababa baadaye mwezi huu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles