24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ZIMBABWE SAWA NA MWEZI UNAOIZUNGUKA DUNIA

KUNA sifa tatu zinazotofautisha Jua, Sayari na Mwezi katika anga ambayo dunia ni Sayari mojawapo inayoelea ndani yake kwamba jua ndiyo kiini cha nishati inayogubika Sayari zote likisababisha uhai duniani lakini ambayo inaushikilia mwezi ulipo.

Dunia inalizunguka Jua na Mwezi unaizunguka dunia kwa siku 30 zinazogawanyika katika mafungu mawili ya miezi sita kwa sita na kusababisha miezi 12. Sizungumzii Sayansi ya anga lakini mkanganyiko uliopo Zimbabwe hususani malalamiko ya baadhi ya waliokuwa viongozi waandamizi wa Serikali iliyoondoshwa madarakani ya aliyekuwa Rais, Robert Mugabe, yanajimithilisha na mwezi unaoizunguka dunia angani kwa kuwa ukweli halisi ni kwamba siku zote duniani tunauona mwezi kwenye upande mmoja tu kwani ukiwa unajizungusha kwenye upande wa pili kwa siku 30 nyingine unakuwa gizani. Ndicho kinachotokea Zimbabwe kwamba dunia nzima inaiona nchi hiyo kwa upande mmoja tu, kuondoshwa kwa Mugabe, lakini sio upande wa pili wa uhalali wa Serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa.

Si chini ya mara moja aliyekuwa Waziri wa Habari wa Taifa hilo aliyekimbia bila kukimbizwa bali kwa kuhofia usalama wake, Jonathan Moyo, ambaye wakati wa utawala wa Mugabe alikuwa moja ya ‘midomo’ ya kutetea sera za chama cha ZANU-PF zilizoendeshwa na Serikali ya bosi wake amesikika akiloloma kwamba nchi hiyo imegeuka ‘Banana Republic’ akimaanisha imetepeta mbele ya jeshi lililopoka madaraka na kuvunja Katiba ya nchi. Kwamba kwa Jeshi kuingilia kati kwa sababu ya hisia za watu wachache dhidi ya mtu mmoja, Grace Mugabe, ni kukiuka demokrasia na kumuaibisha Robert Mugabe ambaye alijitolea kupigania Uhuru wa Taifa hilo kwa kisingizio cha mkewe ambaye hata hivyo alikuwa Kiongozi Mwandamizi wa Umoja wa Wanawake wa ZANU-PF, ambaye kwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake alistahili kupewa nafasi ya kujieleza na kujitetea.

Kwamba kinachoshabikiwa na dunia nzima kwa sasa ni Serikali haramu iliyogubikwa na Jeshi lililopanga njama za Mapinduzi, kwa kumsimika madarakani Mnangagwa aliyekuwa swahiba wa Mugabe kinyume cha utaratibu unaopaswa wa kupiga kura na kuchagua viongozi kupitia demokrasia ya matakwa ya wananchi. Kwa msingi wa kelele zinazopigwa na waliokuwa viongozi waandamizi wa Serikali iliyoondoshwa madarakani, ni sawa na tunavyoridhika kuuona upande mmoja wa mwezi angani ndivyo dunia inavyotathmini yanayoendelea katika nchi hiyo. Ni hulka katika medani ya siasa za kimataifa habari ya moto zaidi kuzipiku nyingine na kuziondosha katika kuzingatiwa ingawa bado fukuto huwa endelevu kwa mkanganyiko unaojitokeza.

Anachokilalamikia Jonathan Moyo kinaakisi hisia za kundi lingine ndani ya Zimbabwe ambalo pengine kwa sasa halina mvuto wa kusikilizwa, kutokana na yaliyojiri kwa muda mrefu katika Taifa hilo ambalo limegubikwa Mapinduzi baridi ya kijeshi yasiyokuwa na umwagaji damu. Lakini kinachoifanya dunia kuitazama Zimbabwe kama mwezi angani ni jinsi ilivyojijengea uhasama na wanaoshika mpini wa mzania wa ustawi duniani, Rais Mugabe alipopoka mashamba ya wakulima wa Kizungu wapatao 4000 na kusababisha kudorora kwa uzalishaji wa chakula na kusababisha janga la njaa. Benki Kuu nchini humo ikachochea mfumuko wa bei katikati ya uhaba wa bidhaa kwa kuchapisha noti na kuziingiza kwenye mzunguko na kusababisha mfumuko huo kupanda, ukosefu wa ajira ukaongezeka na uchumi kuporomoka vibaya na katika kutapatapa Taifa hilo likaitosa sarafu yake na kuamua kutumia Dola ya Marekani na Randi ya Afrika Kusini sanjari na fedha nyingine za eneo linaloizunguka nchi hiyo.

Katika kutapatapa zaidi baada ya mbinyo wa vikwazo, Mugabe alitishia kutaifisha rasilimali zote zilizowekezwa na kampuni za kigeni ya Magharibi nchini humo hiyo ilisababisha wawekezaji wapya kuikwepa nchi hiyo na kuyumbisha sekta ya madini. Hivyo ndivyo Mugabe alivyoiacha Zimbabwe ambayo Mnangagwa anayeiongoza ana kibarua kigumu cha kubadilisha hali hiyo na kuzuia mdororo wa uchumi, lakini waliopokwa ‘kitumbua’ bado wanashutumu kwamba jeshi limejisimika na kupoka madaraka kwa chuki dhidi ya baadhi ya waandamizi wa Serikali.

Kwamba hata kama Mnangagwa na Serikali yake ikiwasamehe na kuwakubalia waliokimbia warudi nyumbani, hawawezi kupokea msamaha unaotoka kwa ‘shetani’ kwa mujibu wa Jonathan Moyo. Lakini turufu ya walioondoshwa madarakani inadhoofishwa na jinsi dunia inavyoitathimini Zimbabwe kwamba hata kama Jeshi limepoka madaraka na kujisimika hususani baada ya Mkuu wake (Chiwenga) kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, lakini ni bora kuuona upande mmoja wa Taifa hilo kama mwezi unavyoonekana duniani kuliko kurudi kwenye hali iliyokuwapo kabla katika nchi hiyo, ingawa pia kuna makundi yaliyokuwa yanamuunga mkono Mugabe yanaofurukutwa na matakwa ya kurejeshwa utawala wa kisheria wa Katiba wanaohoji uvunjwaji wa Katiba kutokana na jeshi kufanya Mapinduzi baridi.

Inavyoelekea Mnangagwa na kundi lake walijipanga kabla ya kunyakua madaraka kwani tayari wameanza kuwanyooshea tawi la Mzeituni wapinzani walioteswa kwa muda mrefu na Mugabe akiwamo Morgan Tsvangirai wa chama cha MDC, ambapo kwa turufu hiyo matumaini ya kurudi kwenye Jamhuri ya Mugabe kutoka Jamhuri ya ‘Banana’ kama inavyodaiwa na walioondoshwa madarakani yanazidi kufifia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles