Na Adam Mkwepu, Dar es Salaam
TANZANIA imeendelea kupata hasara kutokana na upotevu wa mafuta kwenye mabomba ya kupakulia yaliyopo bandari hali iliyosababisha mamlaka husika kuingia kati.
Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya kutolewa ripoti maalumu ambayo inaonyesha upotevu wa mafuta takribani lita milioni mbili, ambazo zilipotea hivi karibuni wakati wa upakuaji wa mafuta katika meli mbili kwenye boya la Single Point Mooring (SPM).
Barua iliyoandikwa na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uratibu wa Uagizaji wa Mafuta (PIC), Michael Mjinja ya Machi 2, mwaka huu kwenda kwa wamiliki wenye matanki makubwa ya mafuta, ilieleza kuwa limekuwapo ongezeko kubwa la upotevu wa mafuta wakati wa upakuaji.
Mjinja alisema upotevu wa mafuta wakati wa upakuaji kwenye mabomba kutoka melini kwa kutumia boya la SPM, umekithiri kwa ukubwa.
“Utafiti wetu wa pamoja umebaini kuwa upotevu wa mafuta wakati wa kupakua meli za MT Maersk Prosper na MT Front Lion, umefanyika kutokana na kuwapo hujuma wakati wa kupakua mafuta hayo kwenye mabomba,” alisema Mjinja.
Katika barua hiyo ambayo nakala yake imepelekwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), iliezwa wasiwasi wa kuendelea kutumia njia hiyo katika upakuaji wa mafuta bila kupata ufumbuzi wa namna ya kukabiliana na hali hiyo.
Ripoti iliyobainisha madudu hayo ilitolewa na Kamati Maalumu ya Kampuni za Mafuta na wadau wake chini ya Mpango wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS) ambayo ilitaja maeneo matatu yanayotakiwa kuangaliwa kwa makini mojawapo ikiwa ni wakati wa upakuaji wa mafuta kutoka melini.