MOSCOW, URUSI
RAIS Vladimir Putin wa Urusi, hufuatilia kile anachoandika mwenzake wa Marekani, Donald Trump katika mitandao ya jamii.
Hayo yamebainishwa jana na msemaji wa Ikulu ya Urusi, Dmitry Peskov alipozungumza na wanahabari mjini hapa.
Msemaji huyo alisema kwa hivi karibuni, Rais Putin alipokea taarifa hizo juzi na kwamba Serikali imekuwa ikizihesabu kupitia akaunti ya Twitter ya Rais Trump kuwa rasmi.
“Serikali ya Moscow imekuwa ikizihesabu taarifa zote zilizotolewa kwenye akaunti rasmi ya Twitter ya Trump kuwa rasmi, hivyo kinachoandikwa huwasilishwa kama ripoti kwa Rais Putin, ikiwamo zile za wanasiasa wa nchi nyingine,” alisema msemaji huyo.
Peskov alikataa kueleza kuhusu vitendo vya Trump, ambaye anafahamika kwa kuropoka kadiri apendavyo katika akaunti ya Twitter.
“Sidhani ni vyema kutoa maoni kuhusu vitendo vya Rais Trump, itakuwa makosa kufanya hivyo,” alisema msemaji huyo wa Putin.
Aidha msemaji huyo alisema kwamba Putin hana akaunti ya Twitter na hana mpango wa kufungua.