Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimefuta matokeo ya kura za maoni ya Singida Kaskazini kutokana na waliokuwa wagombea wawili Haider Gulamali na Elia Mrangi, kujihusisha na rushwa katika mchakato huo.
Kutokana na hatua hiyo, zoezi la kura ya maoni litarudiwa ambapo kuanzia kesho Jumatano, Desemba 13 wanachama wa chama hicho wanaotaka kugombea jimbo hilo wametangaziwa kuchukua fomu za kugombea na kuzirejesha siku hiyo hiyo ambapo wagombea hao hawataruhusiwa kugombea tena.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, imesema kura za maoni zitapigwa na Halmashauri Kuu ya Jimbo badala ya Mkutano Mkuu wa Jimbo ili kuwahi mchakato huo.
“Wagombea hao wawili suala lao liko mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (Takukuru) na Wana-CCM waliojiuhusisha kwa namna moja au nyingine na vitendo vya rushwa wanaendelea kuchunguzwa na vyombo vya chama vyenye dhamana ya udhibiti wa nidhamu, usalama na maadili pamoja na vyombo vingine vya dola vya kiuchunguzi.
“Pamoja na mambo mengine, wanachama wengine ambao waligombea wanaruhusiwa kugombea tena kwa kufuata utaratibu wa kuomba ridhaa kwa namna barua inavyoelekeza isipokuwa hao wawili,” imesema taarifa hiyo.