Wananchi wa Vijiji na Kata za Tarafa za Loliondo na Sale, wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na operesheni ya kikatili ya kuondoa mifugo na watu akiwamo Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye anadaiwa kutoa amri ya kuchoma maboma ya wananchi ndani ya ardhi ya kijiji.
Aidha, wananchi hao wameishukuru Serikali kwa kumaliza mgogoro wa maslahi katika eneo la Loliondo uliodumu kwa miaka 26 kwa tamko la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Dodoma, baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.
Akisoma tamko la viongozi kutoka maeneo hayo leo Ijumaa Desemba 8, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mathew Siloma amesema operesheni hiyo imesababisha madhara makubwa ikiwamo uchomaji wa makazi, ukamataji na kuwafungulia kesi wananchi, ukamataji wa mifugo na watu kupigwa na kujeruhiwa.
“Tumefurahishwa na hatua zote tulizopitia kutoka kuanzishwa kwa kamati ya pamoja, mikutano, mrejesho na kuwezeshwa kupatikana mkutano wa pamoja na kupata uamuzi wa serikali, sisi viongozi tuliohudhuria mkutano ulewa Waziri Mkuu tumefurahishwa kusikia serikali inakiri baadhi ya mambo,” amesema.
Kuhusu operesheni iliyofanyika Agosti mwaka huu, Siloma amesema kuwa operesheni hiyo imesababisha umasikini mkubwa kwa jamii na kuchangia hofu hivyo kuiomba Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, viongozi hao wa vijiji na Kata watashiriki katika mchakato huo iwapo mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji, upimaji na upatikanaji wa vyeti vya ardhi utafanyika kama hatua ya awali kabla ya mchakato wowote kufanyika.