32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

NYUMA YA PAZIA MBUNGE WA CUF KUJIUZULU

*Asubiri ruksa ya CCM kuwania tena ubunge Kinondoni

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


SIKU moja baada ya aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) kutangaza kujiuzulu ubunge na nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho, sababu za uamuzi wake zimebainika.

Taarifa kutoka ndani ya CUF kupitia watu wake wa karibu zilidai  mbunge huyo amekuwa akikabiliwa na madeni mengi kiasi cha kuwa kwenye hatari ya kufilisiwa baadhi ya mali zake.

Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA kuwa licha ya hali hiyo, kwa mwezi mmoja, hakumshirikisha   kiongozi yeyote kwenye matatizo yake.

Gazeti hili lilimtafuta Mtulia na kuzungumza naye lakini akasema  wote wanaomzushia mitaani kwa uamuzi wake, wanasumbuliwa na povu.

Alisema ameamua mwenyewe kwa hiari yake na si suala linalohusu madeni yake ila amevutiwa  na uchapakazi wa Rais Dk. John Magufuli.

Alipoulizwa kama atawania tena jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, alisema   anasubiri kupangiwa na wakubwa wake lakini kwa sasa hawezi kujipangia.

Na hata alipoulizwa ni kwa nini kila kiongozi au mwanachama akitoka upinzani anasema ni kwa sababu anamuunga mkono Rais Dk. Magufuli, alisema ni lazima iwe hivyo.

Alisema  kwa sababu  ndiye kiongozi wa nchi na chama tawala ambaye pia ni mtekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa Watanzania.

“Hivi unafikiri inakua kwa ajili ya nani?  Ni Magufuli kutokana na utendaji wake na ndiyo msimamizi mtekelezaji wa shughuli zote ndani ya chama changu nilichokiona kinafaa.

“Hakuna mwingine ni yeye na huwezi kukwepa kumpa sifa hizo,” alisema Mtulia.

CUF MAALIM WAMBARIKI

Chama cha Wananchi (CUF), upande unaounga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kimesema kimeridhia kujiuzulu kwa Mtulia huku kikimtakia safari njema katika siasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa  jana na kusainiwa na Naibu Mkurugenzi wa CUF, Mbarala Maharagande, chama hicho kilitarajia hayo mapema na wala hakikushtushwa kutokana na taarifa za intelijensia kilizopata.

“Tuliyatarajia hayo mapema na wala hatukustushwa na uamuzi wake kutokana na taarifa za intelijensia za ukaribu wake na viongozi wa CCM akishirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba.

“Tuna uhakika kuwa wafuasi wengi wa Lipumba watafuata mkondo huo na yeye amefungua njia,”alisema.

Maharagande alisema   uamuzi aliochukua Mtulia ni haki yake kwa mujibu wa katiba ya CUF ibara ya 117(1) na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sura ya 11 Ibara ya 149(1), (d).

Hata hivyo, alisema CUF hakikubaliani na sababu za kujiuzulu kwake kwa sababu upo mwenendo usiofaa wa kuua mfumo wa demokrasia nchini, ukandamizaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Kila mtanzania mwenye akili na fahamu timamu kwa kiwango kidogo tu bila ya kujali itikadi ya vyama, anashuhudia ukweli huu wa ugumu wa hali ya maisha.

“Tunatoa pole kwa wanachama na wananchi wa Kinondoni ambao walipambana kwa hali na mali kuhakikisha   mabadiliko ya  siasa nchini yanapatikana kwa kusimamia ushindi wa CUF na Mtulia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa CUF kitaendelea kusimamia imara kupinga vitendo vya ovyo na kinaamini   ukombozi haujawahi kupiganiwa na watu wenye fikra dhaifu na maono duni.

“Mwisho tunamtakia Mtulia safari njema ya siasa huko alikokwenda.

“Ni haki na uhuru wake ambao unapaswa kuheshimiwa na kila mmoja wetu.

“Tunapingana naye kwa nguvu zote kwa sababu alizozieleza katika kufikia uamuzi alioufanya,”alisema Maharagande.

CUF LIPUMBA KUZUNGUMZA LEO

Kwa upande wa CUF inayoongozwa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, umesema utatoa tamko lake leo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Abdul Kambaya allisema wamepanga kutoa tamko leo.

“Sisi tumepanga kutoa tamko leo kwa waandishi wote na si mmoja mmoja hivyo ngoja hadi hapo kesho (leo) nitakapozungumza na waandishi wa habari,’’ alisema Kambaya.

BUNGE HALIJAPATA TAARIFA

Akizungumza na MTANZANIA kwa   simu, Katibu wa Bunge, Dk. Steven Kagaigai alisema  ofisi ya Bunge haijapokea taarifa rasmi.

“Bado hatujapata taarifa rasmi, tunazisikia hizo za kwenye mitandao tu,” alisema Dk. Kagaigai.

CHADEMA YANENA

Chadema ambacho kiliungana na CUF katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwa sehemu ya ushindi wa Mtulia, kimesema mbunge huyo alikuwa timu ya Profesa Lipumba hivyo hana madhara yoyote kwa Ukawa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, aliliambia MTANZANIA kuwa Mtulia baada ya kushinda ubunge aliusaliti Ukawa ambao ulimwezesha kushinda.

“Kuhusu hatima ya Ukawa, ni kuwa huyu alikuwa timu Lipumba na hivyo hana madhara yoyote kwa Ukawa  kwa sababu baada ya kushinda uchaguzi aliamua kuusaliti Ukawa ambao ulimwezesha kushinda.

“Hivyo hajapunguza lolote kwa vile  hakuwa muumini wa Ukawa. Tunajua kuna jitihada kubwa za kuwarubuni baadhi ya wabunge, madiwani na viongozi wa Ukawa  waweze kujiengua au kujiuzulu kwa hoja kuwa wanaunga mkono serikali.

“Kama wanataka kufanya hivyo wanatakiwa kuchapa kazi na si kuacha kazi waliyoomba kwa wananchi … huwezi kuacha kazi ukasema unaenda kuunga mkono dhana ya hapa kazi tu wakati huna kazi,” alisema Mrema.

WASOMI WATOFAUTIANA

Akizungumzia hatua hiyo ya Mtulia, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema kujitoa kwake  na wengine wanaofanya hivyo, ni wazi  siasa ya Tanzania ina matatizo makubwa.

Alisema haiwezekani mbunge akajitoa kabla ya kumaliza muda wake huku akisahau maelfu ya wananchi waliomchagua.

Mpangala alisema katika nyakati hizi ambazo demokrasia imeminywa huku katiba mpya ikikataliwa, alitegemea upinzani ungejiimarisha kwa kupigania hayo lakini si kukimbilia kulekule.

“Huu ni ubinafsi. Wakati huu nilitegemea upinzani wangejiimarisha kwa sababu ni wazi kwamba demokrasia imeminywa, Katiba mpya imekataliwa. “Ilikuwa ni wakati wao kusimama pamoja kupigania hayo badala ya kufanya hivyo ndiyo unakimbilia kulekule… ndiyo maana nimesema kuna utata mkubwa. Binafsi nachanganyikiwa kabisa kwa haya yanayoendelea.

“Ninavyoona siasa ya Tanzania ina matatizo. Haiwezekani mtu unajitoa katikati, bora ungesubiri muda wako uishe vinginevyo hiyo haieleweki.

“Wananchi walikuchagua na imani yako kwa chama chako sasa wewe unaamua kama mtu binafsi unasahau wale maelfu waliokuchagua katika misingi ya chama chako, unavyojiuzulu binafsi wala hushauriani na wananchi waliokuchagua, hili ni tatizo kubwa.

“Wanasiasa wa sasa wengi ni wasomi, sielewi elimu wanayopata, nahisi ina utata haina misingi ya demokrasia na wanaofanya hivyo wanaangalia masilahi yao ukizingatia serikali ya sasa inabana upinzani hivyo wanaona ukiwa kule utanufaika.

“Yule wa Singida Kaskazini (Lazaro Nyalandu) sababu alizotoa zilikuwa nzito na alikuwa na hoja, lakini wengine hawana hoja eti yale waliyokuwa wakiyapigania sasa yanatekelezwa kwani ukiwa upinzani huwezi kufanya hivyo?”aliuliza Profesa Mpangala.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema sababu zilizotolewa na Mtulia zisipuuzwe.

“Mbunge alipigania ubunge wake hivyo anaona upinzani umeshanyang’anywa donge mdomoni. Kitendo cha kujiondoa na CUF unaijua iko vipande vipande, hivyo wanawanyima wananchi haki hivyo ameona bora ajiondoe.

“Kuacha ubunge si jambo la kawaida ni nyeti unapoteza mamilioni yako ni uamuzi mgumu na mkubwa lakini lazima tuuheshimu,”alisema Dk. Bana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles