25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

UPASUAJI WA HISTORIA MOI

Na VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM


NI historia mpya. Ndivyo unavyoweza kusema, baada  ya Taasisi  ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI),  kwa mara ya kwanza, kumfanyia upasuaji mkubwa wa ubongo mgonjwa aliyepooza mwili kutokana na ajali ya barabarani.

Wiki mbili baada ya upasuaji huo  mgonjwa alisimama na kuanza kutembea na kula mwenyewe bila msaada wa mtu yeyote.

Upasuaji huo wa aina yake ulifanyika mwezi uliopita na madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ambao ni Watanzania.

Madaktari hao ni Nicephorus Rutabasibwa ambaye alijifunza   kufanya upasuaji huo Afrika Kusini na mwenzake,Laurent Lemery aliyepata utaalamu huo  Morocco.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu mwishoni mwa wiki, Dk. Rutabasibwa alisema upasuaji huo utaalamu unaitwa Craniocervical Stabilization & Fussion.

“Ni upasuaji mkubwa unaohusisha kuunganisha mishipa ya fahamu iliyovunjika…mgonjwa alikuwa amevunjika mno katika pingili za mifupa ya kichwa hasa eneo la kichogo inapoungana na uti wa mgongo,” alisema.

Alisema   kuvunjika kwa uti wa mgongo ndiko kulisababisha mgonjwa  kupooza mikono na miguu yake.

“Tulipompokea alikuwa hawezi kushika kitu chochote hata kutembea, alikuwa analala tu kitandani muda wote,” alibainisha.

Alisema alifanyiwa kipimo cha kwanza cha CT-Scan  na kuchunguzwa uti wake wa mgongo, kuangalia ulikuwa umevunjika kwa ukubwa kiasi gani.

“Pia tulimfanyia kipimo cha MRI ambacho kilituonyesha uti wake wa mgongo ambao unashika ile mishipa ya fahamu ulikuwa umebana mno kuliko kawaida yake,” alisema.

Dk. Rutabasibwa alisema kubana kwa mishipa hiyo ya fahamu nako kulichangia kwa namna moja au nyingine mgonjwa huyo kupooza.

“Baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo tulimpeleka chumba cha upasuaji na kuanza kuirudisha ile mifupa iliyokuwa imeachana   kuirejesha katika hali yake ya kawaida,” alisema.

Aliongeza: “Ule mfupa wa fuvu la kichwa na uti wa mgongo nao tukaurejesha katika hali yake ya kawaida pamoja na ile mifupa iliyokuwa imebana nayo tuliirudisha katika hali yake ya kawaida.

“Sasa ingawa tulikuwa tumeirejesha katika nafasi yake ya awali, bado ilikuwa si imara kwa sababu ilikuwa haishikiliwi na kitu chochote kuiwezesha kuimarika tena.

“Hivyo, ikatubidi tumuwekee ‘implant’… hivi ni vipandikizi maalumu vya ndani kwa ndani ambavyo tuliweka eneo la kichogo katika kichwa chake na tukaunganisha na uti wake wa mgongo katika eneo la shingo.

“Tulimfanyia pia ‘fussion’ hii ni hatua ambayo tunaunganisha eneo hilo kwa kutumia gundi maalumu”.

Alisema kwa kumpandikiza kifaa hicho, mishipa hiyo sasa ipo imara na mgonjwa anaweza kugeuka upande mmoja hadi mwingine.

“Alikuwa hawezi hata kugeuka sasa anaweza.  Baada ya upasuaji alikaa wodini wiki mbili akaanza kufanya mazoezi mepesi (rehabitation) akaimarika tukamruhusu kurejea nyumbani,” alisema.

Alisema mgonjwa huyo ataendelea kufanya mazoezi hayo mepesi kwa miezi mitatu na   baada ya muda huo kuisha atakuwa amepona kabisa.

“Ni upasuaji ghali mno, tulimuwekea ‘implant nane’, kushoto nne na kulia nne, kila kimoja kinauzwa Dola za Marekani 1,000 ambazo ni   Sh milioni mbili. Imegharimu takriban   zaidi ya Sh milioni 10 kumtibu,” alibainisha.

Alisema iwapo mgonjwa huyo angepelekwa nje ya nchi kufanyiwa upasuaji, ingegharimu zaidi ya Sh milioni 25, ikiwa ni gharama za tiba, usafiri na gharama za daktari msindikizaji.

Alisema mbali na kupooza mwili, madhara mengine ambayo mtu anayepatwa na tatizo kama hilo hukabiliana nayo ni kushindwa kupumua ipasavyo.

“Hiyo ni kwa sababu misuli ya kifua chake inakuwa inashindwa kutanuka inavyotakiwa, huwa pia anashindwa kumeza kitu chochote anachokula au anachoweka mdomoni.

“Msukumo wao wa damu mwilini huwa upo chini mno kwa sababu mishipa inayopokea na kutoa damu kwenye moyo huwa inapooza na kushindwa kufanya kazi yake sawa sawa,” alisema.

Aliwashauri madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani  kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

“Zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa tunaowahudumia hapa MOI ni wa ajali hasa za bodaboda, ni muhimu wakafuata sheria za usalama barabarani kuepuka ajali.

“Hadi sasa wodini kuna wagonjwa sita ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji wa aina hii ambao tutawafanyia wakati wowote kuanzia sasa.

“Hii yote ni kutokana na ajali, ni muhimu madereva wakafuata sheria za usalama barabarani kwa sababu ajali zinamaliza nguvu kazi ya familia na taifa kwa ujumla.

“Lakini nitoe rai kwa mtu yeyote aliyepooza mwili ni muhimu ndugu zake wakamleta hospitalini tumfanyie uchunguzi tujue kinachomsumbua aweze kupata matibabu sahihi.

“Kwa sababu ikiwa ataendelea kukaa nyumbani na kugundulika baadaye tatizo linakuwa limekomaa na inakuwa vigumu kurejea katika hali yake ya kawaida kama binadamu wengine,” alibainisha.

Meneja Uhusiano na Ustawi wa MOI, Almasi Jumaa alisema upasuaji huo ni wa aina yake ambao sasa unafanyika nchini kwa mara ya kwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles