Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amenusurika kifo baada ya kupuliziwa kwa inayodaiwa kuwa gesi ya kuwasha katika Uchaguzi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), jijini Mwanza.
Uchaguzi huo uliolazimika kufanyika katika Uwanja wa CCM Kirumba baada ya mmoja wa vijana kudaiwa kupulizia gesi hiyo ya kuwasha iliyozua taharuki ndani ya ukumbi wa Rock City Mall jijini humo, hali iliyosababisha Naibu Waziri huyo kusaidiwa kutolewa nje haraka na alipatiwa huduma ya kwanza huku wajumbe wengine wa mkutano huo waliofanikiwa kutolewa ndani ya ukumbi huo wakiwa hoi ambapo walipatiwa maziwa na maji kwa ajili ya kuondoa gesi hiyo iliyokuwa ikiwasha.
Tukio hilo limetokea leo Jumatano Novemba 29, baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa UVCCM kuwasili na kuelekezwa kuingia ndani ya ukumbi tayari kwa kumpokea mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.
Wakiwa ndani ya ukumbi huo huku wakiimba nyimbo za chama, ghafla hali ya hewa ilibadilika baada ya watu kuanza kukohoa na kupiga chafya kutokana na hewa nzito na kusababisha wajumbe kukikimbilia nje kujiokoa.
Hofu ya usalama ilitanda ndani ya ukumbi huo hivyo Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Raymond Mwangwala alilazimika kukutana na Mkuu wa Mkoa John Mongela na kukubaliana mkutano huo kuhamishiwa uwanja wa CCM Kirumba na kuendelea na uchaguzi.
Hata hivyo, tukio hilo liliwalazimu kuita polisi ambao baada ya kufika walianza kufanya upekuzi kwa baadhi ya wajumbe waliokuwa na mabegi na mikoba na kufanikiwa kumkamata mjumbe mmoja ambaye walimtilia shaka na kuondoka naye hali iliyozua vurugu zaidi kwa vijana kupinga kukamatwa kwake.
Lakini inadaiwa kijana aliyekamatwa alikuwa na pafyumu ya kawaida wakati polisi wakiifananisha na gesi ya kuwasha ambapo walianzisha vurugu wakishinikiza aachiwe ndipo Mkuu wa Mkoa alipoingia kati kuwatuliza kwa kuamuru polisi kumwachia kijana huyo ambaye alirejea mkutanoni.