Na PETER FABIAN
MADIWANI wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Wilaya ya Nyamagana wametakiwa kuacha usanii wa kuendekeza mgogoro baina yao na Meya wa Jiji hilo, James Bwire pamoja na Mkurugenzi, Kiomoni Kibamba.
Wametakiwa kuacha kutumia fedha za walipakodi kujilipa posho bila kufanya vikao vyenye tija kuwaletea maendeleo wananchi.
Ushauri huo ulitolewa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jumuiya zake za kata na Tawi la Mahina.
Wamewataka madiwani kuacha kuzua migogoro inayokwamisha maendeleo ya wananchi waliowachagua kuwatumikia.
Walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari jana wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Kata hiyo, Felician Burakari.
Nurakari alisema mgogoro unaoendelea kwenye halmashauri Jiji kati ya Meya, Mkurugenzi na madiwani unaidhoofisha CCM na kudumaza maendeleo ya wananchi .
“Tukerwa na minyukano ya siasa kati ya Diwani wetu, James Bwire ambaye ni Meya wa Jiji na Mkurugenzi Kiomoni Kibamba na baadhi ya madiwani.
“Migogoro yao wasiilete katika kata yetu, wao wanyukanie kwenye ofisi za halmashauri lakini pia wakumbuke kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo,” alisema Burakari.
Alisema madiwani na maofisa wa halmashauri ya jiji walikwenda kwenye kata hiyo kutembelea eneo inakojengwa hospitali na Kampuni ya Nyamwaga Ltd inayomiliki Kituo cha Alliance Sports Academy bila kutoa taarifa kwa uongozi wa serikali ya mtaa, kata na wamiliki wa eneo hilo.
Burakari alisema hatua hiyo ilisababisha watimuliwe kwa mawe na wananchi.
“ Madiwani na maofisa wa jiji (wataalamu) walifuata nini bila taarifa kukagua mradi ambao hauhusiani na jiji ? huku wakijua kuwa eneo hilo ni mali ya Kampuni ya Nyamwaga na Alliance Sports Academy ambayo ina uongozi wake.
“Eneo hilo lilinuliwa kutoka kwa wamiliki wa asili na halikuwahi kulipwa fidia, na jiji wakijua kuwa mgogoro wa eneo hilo uko mahakamani?” alihoji Burakari.
Katibu wa CCM Tawi la Mahina, Prudence Gabriel, aliyekamatwa pamoja na Burakari, alisema madiwani hawana budi waache usanii kwa sababu muda huo umeisha umebaki wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Viongozi wa CCM Burakari na Gabriel walikamatwa na polisi Novemba 9, mwaka huu wakiwa kwenye kampeni za udiwani katika Kata ya Mhandu.
Walidaiwa kuwashambulia madiwani na maofisa Jiji la Mwanza waliokwenda kwenye eneo lenye mgogogro uliopo baina ya halmashauri na Kampuni ya Nyamwaga ambayo meya ni mmoja wa wakurugenzi.