Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Ramadhani Nsanzurwimo, amesema baada ya kuisoma Simba wakati ikicheza na watani zao, Yanga wiki iliyopita, tayari amepata dawa ya kuwaangamiza wekundu hao wa Msimbazi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nsanzurwimo alifanya kazi ya kuisoma Simba katika pambano la watani wa jadi lililochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Uhuru, ikiwa ni siku moja baada ya kupoteza mchezo wao dhidi ya Azam FC, uliochezwa Ijumaa iliyopita katika Uwanja Azam Complex.
Mbeya City, inayoshika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, ikivuna pointi 11, inatarajia kuwaalika vinara Simba, wenye pointi 16, kwenye mchezo wa raundi ya tisa utakaopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, Jumapili.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Nsanzurwimo alisema aliwasoma Simba ili kupata mbinu za kuwazuia washambuliaji Laudit Mavugo na Emmanuel Okwi wasiweze kuleta madhara kwenye mchezo huo.
“Nimepata bahati ya kuwaona wakicheza dhidi ya Yanga, shida yangu kubwa ilikuwa kuwachunguza Mavugo na Okwi, Mavugo ni mrundi mwenzangu, lakini sijawahi kumuona akicheza, hivyo kupitia mchezo ule nilipata pa kuanzia.
“Tumepanga kuhakikisha tunarekebisha haraka mapungufu yaliyotukwamisha kupata ushindi kwenye mchezo uliopita, tumepania kupata pointi muhimu nyumbani,” alisema.