LONDON, ENGLAND
MSHAMBULIAJI wa klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea, Alvaro Morata, amekanusha kwamba hapendi kuishi nchini England, hivyo amedai yupo tayari kuongeza mkataba hata wa miaka 10 ndani ya mabingwa hao.
Awali mchezaji huyo aliliambia gazeti moja la nchini Italia kwamba hana maisha marefu katika Jiji la London na ataondoka kwa kuwa hapapendi.
Alipoulizwa kuhusiana na kauli hiyo wakati wa kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya jana dhidi ya AS Roma, alisema alimaanisha hatakaa London baada ya kustaafu soka.
“Nina furaha kubwa sana kuwa hapa, ninafurahia kila kitu cha London pamoja na mke wangu, lakini nadhani wapo watu ambao wameninukuu vibaya.
“Nimejiunga na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano, ninaamini endapo nitaendelea kufanya vizuri kwa ajili ya timu nitapata nafasi ya kukaa hapa kwa zaidi ya miaka hiyo mitano niliyosaini baada ya kujiunga.
“Chelsea wakiwa tayari kunipa mkataba mwingine wa miaka 10 nipo tayari kusaini, lakini natakiwa kuongeza kasi yangu ya kupachika mabao na vinginevyo wataamua kuachana na mimi na kumsajili mchezaji mwingine.
“Nadhani London kuna utamaduni tofauti na ule niliouzoea nchini Italia katika klabu ya Juventus na nchini Hispania, hivyo naweza kusema ninahitaji mazoea ili kukaa kwa muda mrefu na bila hivyo naweza kurudi Italia au Hispania.
“Hata hivyo, familia yangu bado inaonesha kuwa na furaha kuwa hapa, hivyo chochote kinaweza kutokea lakini sijasema kama sina furaha kubwa hapa,” alisema Morata.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25, hadi sasa amefanikiwa kupachika mabao saba baada ya kucheza michezo 13 tangu alipojiunga na kikosi hicho kwa uhamisho wa pauni milioni 60 Julai mwaka huu akitokea Real Madrid.
Hata hivyo, mchezaji huyo amedai anatamani siku moja kurudi katika klabu yake ya zamani ya Juventus kwa kuwa uongozi wa klabu hiyo ulimfanya kama mtoto wao na hadi anaondoka alionekana kuwa mchezaji aliyekomaa.
“Juventus ni sehemu ambayo naweza kusema wamenifanya niwe hapa nilipo sasa, walinichukua nikiwa mdogo na kuniacha kwa amani nikiwa mchezaji bora, hivyo bado ninaamini ipo siku nitarudi katika klabu hiyo, ninaikumbuka sana Juventus, ninawakumbuka sana mashabiki wake, nawapenda sana, lakini kwa sasa ninaipigania Chelsea na lengo langu kubwa ni kuacha historia jijini London,” aliongeza.
Wakati anakipiga katika klabu ya Juventus, alifanikiwa kutwaa mataji mawili ya ligi kuu pamoja na mataji mawili ya Coppa Italia, huku akicheza michezo 93 ya ligi kuu na kupachika mabao 29. Wakati huo katika klabu ya Real Madrid akishinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa, mawili ya ligi kuu, mawili Copa del Rey, moja Spanish Super Cup na Uefa Super Cup, huku akicheza jumla ya michezo 88 ya ligi kuu na kupachika mabao 34.