Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema uchunguzi wa wa tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu utafanywa na vyombo vya dola vya hapa nchini.
Kutokana na hatua hiyo, amewataka Watanzania kuamini vyombo vya ulinzi na usalama katika kuchunguza tukio hilo na mwngine yanayofanywa na watu wasiojulikana.
“Juzi tu baada ya tukio hili nilisikia ndugu zetu wanaomba vyombo vya nje vifanye upelelezi, mimi nasema kazi hii itafanywa na vyombo vyetu na watafikishwa kwenye vyombo vya sheria vya hapa hapa kwa sababu hata ukimtoa mtu mbali atauliza watu wa hapa hapa.
“Sisi kama serikali niwahakikishie hawa watu tutashughulika nao kweli kweli na wale wanaojiandaa kuwatia hofu watu wetu kwa mambo ya kiusalama wanatafuta vita ambayo wameshindwa kabla hawajaanza tutashughulika nao mmoja mmoja.
“Na hii kasumba ya watu kushambulia watu na kubebeba jina la watu wasiojulikana wamemshambulia Lissu, wamemshambulia mwanajeshi mstaafu, hakimu pale Lindi, sasa wanaofanya uhalifu wa aina hiyo dakika zao za kufika kwenye mkono wa sheria zinahesabika,” amesema Mwigulu.