30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

TUJIULIZE MASWALI MAGUMU NA TUYAJIBU WENYEWE

WIKI iliyopita hoja kubwa ilihusu masuala ya uchaguzi Kenya na uamuzi wa kihistoria wa Mahakama yao ya Juu. Kabla ya hapo tulikuwa na mshangao wa mabomu ofisi za mawakili hapa Dar es Salaam.

Wakati nikijipanga kuzungumzia jinsi suala hili lilivyoshugulikiwa na mawakili hasa katika maamuzi ya baraza la uongozi la Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), tukapokea mshtuko mwingine mkubwa zaidi pale tulipoarifiwa kuwa Rais wa TLS na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameshambuliwa kwa risasi nje ya nyumbani kwake huko Dodoma.

Huu ulikuwa mshtuko mkubwa si kwa vile hatujawahi kusikia mtu kushambuliwa na risasi bali ni kutokana na ukweli kuwa si kawaida katika nchi hii mtu wa wadhifa huo kushambuliwa mchana kweupe wakati anafika nyumbani tena kwenye eneo ambalo tungedhani lina ulinzi wa kutosha.

Pia ni kwa vile mbunge huyu amekuwa mstari wa mbele kusema kwa uwazi yale anayoona yanahitaji kurekebishwa katika utawala uliopo madarakani. Mimi katika ubinafsi wangu nilishangaa zaidi hasa nikikumbuka kuwa kwenye suala la mabomu katika ofisi za mawakili tulishirikiana na Rais huyu pale tulipoamua kuunga mkono kauli ya chama hicho ya kulaani na kuwa na mgomo wa siku mbili kwa kutokuhudhuria mahakamani kwa nia ya kupinga kitendo hicho kilichokuwa kinaashiria kuwatisha na kuwaogofya mawakili na watetezi wa haki kwa ujumla wao.

Katika maongezi yake Lissu alisisitiza kuwepo na umoja katika kukemea mambo ambayo hayako sawa kama hilo lililokuwa limetokea na alisema hatuwezi kujua ni nani atafuata baada ya hili. Bahati mbaya sana yeye ndio amefuata. Tunamshukuru Mungu kwa kumnusuru na tunazidi kuomba apone na aweze kurejea katika maisha yake ya kila siku.

Haya matukio ya sampuli hii ambayo yameharibu kabisa sifa ya nchi yetu kiasi ambacho hatutakosea tukisema amani yetu ‘imebikiriwa’ kwani hatuna tena ujasiri kama tulivyozoea kuwa nchi hii ni kisiwa cha amani. Ni kitu gani au watu gani au hali gani zimetufikisha hapa?

Kumekuwepo na viashiria  mbalimbali vya kuharibika kwa amani nchini ambavyo kwa kweli havikutiliwa maanani na sisi wote. Shida ni pale kila mtu anavyodhani havimhusu na havimhusu kwa vile hakuguswa yeye. Kuna mtu alituma picha moja katika mtandao wa whatts app ikimuonyesha mamba aliyemkamata nyumbu.

Yule nyumbu alikamatwa mbele ya nyumbu wenzake kundi kubwa sana na pia walikuwepo na pundamilia. Wakati nyumbu yule akijitahidi kuokoa maisha yake kujinasua katika mdomo wa mamba wale wenziwe hawakuonekana kuhangaika au hata kujali waliendelea na maisha yao.

Huyu nyumbu aliyekamatwa nusura azidiwe nguvu na yule mamba bahati wakatokea viboko wawili majini wakamsukuma mamba huyo nyumbu akaachiwa na kukimbia huku akichechemea kwa maumivu.

Hata baada ya nyumbu huyu kunusurika wale wenziwe hawakuonyesha kumjali hata kumsogelea kama ishara ya kumpa pole. Nilipoangalia hiyo picha nilipata maswali kadhaa kwa nchi yetu katika muktadha wa mambo yaliyokuwa yanaendelea kwa baadhi ya watu wengine wakiwa wanaangalia tu na kuendelea na maisha yao au hata kukejeli.

Nchi hii ni nzuri mno. Imejaa sifa sana kwa jinsi ilivyo na watu wema, wastaarabu, wanaobadilishana madaraka kila inapotakiwa na katiba kiasi kuwa hivi sasa tunao marais wastaafu watatu.

Mungu amlaze pema Mwalimu Julius Nyerere kwani naye angekuwa mmoja wao. Katiba iliyokuwa haina hati za haki za binadamu iliwekewa hati hizo mwaka 1984. Mfumo wa vyama vingi uliositishwa baada ya uhuru ulirejeshwa mwaka 1992. Chaguzi ziliendelea kufanyika na vyama vikaendelea kujijenga.

Hii hali ya chuki kiasi hiki hadi kuchoma ofisi kwa mabomu na hata kufikia kutaka kumuua Mbunge na Rais wa chama cha wanasheria imetoka wapi? Je wapo wageni wametuingilia bila wenyewe kujua? Je tulilala hadi mioyo yetu ikageuzwa kuwa na kutu bila sisi kujua? Bahati mbaya sana vitendo ambavyo vimetendeka katika kipindi hiki cha karibuni na matamko ambayo yameendelea kutamkwa na viongozi wa ngazi mbalimbali yamejenga chuki kiasi ambacho nimeona watu wengine wakiona pengine hatuhitaji uwepo wa vyama vingi vya siasa. Na kama kuna uhusiano wa matamko na vitendo hivyo na matukio kama haya basi tungepata majibu.

Kila mara matukio mabaya na ya kihalifu yakitokea umekuwepo msemo wa kuwa yamefanywa na watu wasiojulikana. Hawa watu wamefanya kazi ya upelelezi hapa nchini iwe kama haiwezekani. Matukio kama yale ya watu waliouawa kule Tanga, watu nane wa familia moja sina kumbukumbu kuwa walishakamatwa na ni nani na hatua gani zilichukuliwa.

Yapo matukio ya msikitini Mwanza nayo pia sina uhakika walishajulikana na hatua zikachukuliwa. Huko Kibiti nako na hivi karibuni ofisa ya IMMMA Advocate na sasa Lissu.

Ukisikia wapo waliopatikana baadaye utapata taarifa kuwa walijaribu kukimbia au walirushiana risasi na polisi, kwa hiyo wamefariki wakiwa wanapelekwa hospitali baada ya kujeruhiwa na risasi za polisi waliokuwa wakiwadhibiti. Hivi kweli polisi wetu hawako makini kiasi hicho kwamba kila mara wawe wanakimbiwa na watuhumiwa na kuviziwa kwa risasi?

Tunaendelea kuangalia pale ambapo watu wameonekana ama kwa picha katika tukio kama vile yule mtu aliyemnyooshea bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni, Nape Nnauye mbona hatuna taarifa ya nini kilimtokea? Tunahitaji kujiangaliza sana.

Watanzania tusiangalie haya masuala kama vile ni sinema ambayo itaisha na kiranja wake hauawi, tusiangalie kama vile ni ndoto kwamba tutaamka tukute imeondoka na si kweli. Kila mmoja wetu anapaswa kuhoji ili tupate majibu hasa ya mambo ambayo sasa yametuharibia kabisa muonekano wa nchi yetu.

Tusiendelee na maisha kama kawaida wakati hayapo kawaida. Kama unadhani ni yule ipo siku inaweza kuwa ni wewe au jamaa yako. Mamlaka zetu hebu zijiangalize katika yale ziyatendayo na yale viongozi wayasemayo.

Jinsi nilivyoona tukio la kushtusha lililomtokea Lissu hasa kutoka nje ya nchi  kuna sababu ya kujiuliza sana kulikoni, hii kweli ni Tanzania yetu. Maana tumeshuhudia  Kenya, Uganda, Afrika Kusini, India ,Uingereza, Umoja wa nchi za Ulaya, Marekani  na hata Umoja wa Afrika wa Wanasheria wote hao wakituma salamu za pole zilizoanza kwa kueleza kiasi walivyoshtushwa na tendo hilo la  kinyama kwenye nchi hii ya kiutu.

Turudi tulipojikwaa tukiangalie hicho kisiki kilichosababisha. Iwapo kinafaa kung’olewa king’olewe iwapo ni cha kupunguza kipunguzwe. Tusipojiangaliza sasa tutakuwa tunajiandaa kwa dhiki zaidi. Nazidi kuwasihi watanzania kwa ujumla wetu tusimame na haki tukatae vitendo vya kidhalimu.

Kama tunavyojibidiisha kupambana na wezi wa rasilimali zetu tupambane kulinda amani yetu. Amani ikitoweka rasilimali zitaibiwa zaidi. Pamoja na kuwa tumeitia doa amani yetu bado tuna nafasi ya kuitetea na kuirejesha mahali pake hili ni jukumu letu sote vijana kwa wazee wanawake kwa wanaume.

Tanzania ni yetu sote tukumbuke hatuna pa kukimbilia tumekuwa kisiwa na gome kwa miaka mingi. Ngome ikibomoka si salama kwa waliomo na wanaotaraji kuwemo.

MUNGU IBARIKI TANZANIA NA WATU WAKE

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles