Na Ahmed Makongo
WAFUGAJI katika Halmashauri ya Mji wa Bunda wametakiwa kutumia rasilimali yao ya mifugo kusomesha watoto wao waweze kupata elimu inayostahili itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alisema wazazi nao watafaidika na elimu hiyo kwa kutunzwa vizuri na watoto hao wanapokuwa wazee.
Alikuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa uwekaji chapa kwenye ng’ombe katika Halmashauri ya Mji wa Bunda uliofanyika katika Mtaa wa Butakare Kata ya Bunda stoo.
Bupilipili alisema elimu ndiyo msingi wa maisha hivyo ni vema na haki kwa wafugaji katumia rasilimali ya mifugo yao na kuivuna kwa kuiuza kwa ajili ya kusomesha watoto wao waweze kupata elimu bora itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.
“Ninawahimiza ndugu zangu wafugaji musomesheni watoto wenu kwa kutumia hii mifugo yenu.
“Maana ukisomesha mtoto wako utakuwa umefanya jambo jema maana hiyo elimu itamsaidia yeye na wewe mzazi wake katika maisha yao ya baadaye,” alisema.
Alisema ukitaka kufaidi matunda ya nchi hii ni kusomesha mtoto wako kwa sababu baadaye atakusaidia.
DC aliwaambia wafugaji hao kuwa uwekaji chapa kwenye mifugo yao kuna manufaa mengi sana.
Alitaja manufaa hayo kuwa ni kudhibiti wizi wa mifugo, kujua idadi ya mifugo iliyoko katika halmashauri hiyo, kufuga kisasa kulingana na maeneo ya malisho na kuweka mikakati madhubuti ya kuihudumia mifugo hiyo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Janeth Mayanja, na aOisa Mifugo katika Halmashauri hiyo, Rick Kaduri, walisema kabla ya kuanza uwekaji chapa ng’ombe, kwanza walitoa elimu kwa wafugaji wote waweze kufahamu umuhimu wa hatua hiyo.
Ofisa mifugo huyo wa halmashauri ya mji wa Bunda alisema uwekaji wa chapa kwenye ng’ombe linakwenda na usajili wa mifugo yote iliyoko katika halmashauri ya mji huo.
Nao baadhi ya wafugaji hao walifuraishwa na uwekaji chapa kwenye ng’ombe wao.
Walisema serikali inatambua mchango wa wafugaji katika maendeleo ya nchi kwa sababu wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali za kuchangia miradi ya maendeleo katika maeneo yao.